Chongolo ashusha kero kwa mawaziri wanne, awaita haraka kwenda kuzitatua

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo
Muktasari:
- Kero za maji, umeme, miundombinu ya barabara na uhaba wa watumishi wa sekta ya afya zimeibuliwa na wananchi na viongozi katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo mkoani Katavi.
Katavi. Kero za maji, umeme, miundombinu ya barabara na uhaba wa watumishi wa sekta ya afya zimeibuliwa na wananchi na viongozi katika ziara ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo mkoani Katavi.
Ni ziara ya siku tano na jana ilikuwa siku ya kwanza iliyoanzia wilayani Tanganyika kwa kukagua ujenzi wa Hospitali teule ya wilaya hiyo iliyopo Kata ya Ikola kisha kutembelea Bandari ya Karema itakayohudumia nchi za DR Congo, Burundi na Zambia.
Kutokana na kero hizo kuibuliwa kwa nyakati tofauti, Chongolo aliwataka mawaziri wanaohusika na changamoto hizo kufika mkoani humo kuzitafutia ufumbuzi akiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ashughulikie umeme wa Gridi ya Taifa.
Mawaziri wengine ni, Jumaa Aweso (Maji), Innocent Bashungwa (Ujenzi) na Mohamed Mchengerwa wa Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Tatizo la umeme lilianza kuibuliwa na juzi jioni katika kikao cha ndani kilichokuwa na lengo la kumpa taarifa ya mkoa za chama hicho na ile ya Serikali iliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Mkoa huo (RC), Mwanamvua Mrindoko.
Mara baada ya kumaliza, alipata wasaa wa kuwasalimia mamia ya wananchi waliojitokeza kumpokea ofisi za chama hicho mkoa akisema,
haiwezekani mkoa huo umeunganishwa na barabara nzuri ya lami kutoka Tabora hadi Katavi harafu ukakosa umeme wa uhakika ambao utachochea maendeleo ya mkoa huo ulioanzishwa mwaka 2012.
“Nimekuja kufuatilia utekelezaji wa Ilani yetu ya mwaka 2020/25 ambayo ndani yake ndio imebeba ahadi za barabara, afya, umeme, kilimo, pembejeo na mambo mengi. Tuliahidi hivyo tunakuja kutembelea na kukagua miradi hiyo,” alisema Chongolo
Akiendelea kutoa salamu zake, Chongolo alisema amepokea taarifa ya chama pamoja na ya Serikali iliyowasilishwa Mkuu wa Mkoa huo, Mwamvua Mrindoko ikiwa na masuala mbalimbali ikiwemo changamoto ya mkoa huo kutokuwa na umeme wa uhakika.
Alisema katika taarifa zao mbili ya CCM na Serikali walizowasilisha viongozi hao wa chama na Serikali alidai wamesisitiza kuhusu suala la umeme ambayo imekuwa kero kwa wananchi na wawekezaji wanaotaka kuwekeza mkoani humo.
Chongolo alisema ameelezwa kumekuwa na ahadi zinazotolewa na viongozi mbalimbali ili kuusukuma kukamilika kwake lakini utekelezaji wake unasuasua na wao kama chama tawala waliahidi mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa lakini mkapa sasa ni Rukwa na Kigoma pekee imeunganishwa.
“Kigoma wamekwisha kuunganishwa kwa sehemu kubwa, Rukwa tayari, bado mkoa wa Katavi, niwaahidi mimi natamani kuchanguliwa kwa kishindo ndani ya mkoa huu,” amesema Chongolo huku akishangiliwa na sauti zikisikika, “tumkwisha kushinda babaaaa.”
Baada ya kueleza hayo, aliuliza mradi huo upo chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) au Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)? Alijibiwa Tanesco.
“Basi niachieni mimi, nitakwenda kukaa na waziri anayehusika na hiyo Tanesco na bahati nzuri ampewa mamlaka makubwa kwa hiyo hana sababu ya kujitetea.
Nitakwenda kumwambia kwanza yeye mwenyewe aje aangalie uhalisia wa utekelezaji wa huu mradi lakini mbili ahakikishe anaweka nguvu zake zote hapo ili wananchi wa mkoa wa Katavi wajielekeze kupata umeme wa Gridi wa Taifa,” alisema Chongolo
Alisema, mkuu wa mkoa amemweleza watu wengi wanataka kuwekeza ikiwemo viwanda kama vya kuchakati alazeti lakini changamoto ni umeme wa uhakiki,”na sisi ni jukumu letu kuleta umeme na kazi yangu ni rahisi, kwenda kusimamia tuliyoyaahidi yanakwenda kutekeleza. Niwaambie tu nakwenda kusukuma mradi huu uwe historia.”
“Hatuwezi kuwa na barabara nzuri kutoka Tabora hadi hapa Katavi harafu nguzo tu za umeme zikatushinda, tutakuwa hatutendi haki dhamira zetu na Rais aliyetuamini kuwa wasaidizi wake kwenye maeneo mbalimbali,” alisema.
Mradi huo uliwekwa jiwa la msingi Oktoba 2019 na Rais wa wakati huo, John Magufuli (aliyefariki Machi 17, 2021) wa kuunganisha mkoa wa Katavi kwenye Gridi ya Taifa kwa njia ya msongo wa Kilovolti 132 kutoka mkoani Tabora.
Suala hilo likaibuliwa tena jana katika Bandari ya Karema na Mbunge wa Viti Maalum, Taska Mbongo aliposema bandari hiyo haitakuwa na maana kama hakutakuwa na umeme wa uhakika,"tunaomba sana katibu mkuu, tupate umeme wa Gridi ya Taifa. Katavi inahitaji sana umeme na hili linawezekana kabisa."
Akijibu hilo, Chongolo alisema, "jana usiku (juzi) nilizungumza na wziri (Biteko) amenihakikishia hili linakwenda vizuri. Ameniambia fidia kwa wale wanaopisha mradi, ameniambia hadi Oktoba 15 mwaka huu watakuwa wamelipwa na mimi niwahakikishie, umeme wa Gridi ya Taifa utafika, ili umeme unaotumika nchi nzima, utumike Katavi."
Mikataba isainiwe hapa
Kero nyingine ni ya barabara ya kilomita 112.9 ya kutoka barabara kuu ya Tanganyika kwenda Bandari ya Karema akasema, Waziri Bashungwa anapaswa kuisimamia ipasavyo ianze haraka.
Kabla ya maagizo hayo, Mbunge wa Tanganyika (CCM), Suleman Kakoso alimweleza Chongolo barabara hiyo imekuwa kero hususan nyakati za mvua hali inayosababisha adha kubwa kwa wananchi.
Kutokana na hilo, Chongolo alimwita Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara, Albert Laizer alisema kandarasi zimetangwa na hadi Novemba mwaka huu atakuwa amepatikana. Aliongeza ni wakandarasi wawili ambao mmoja atajenga kilomita 50 na mwingine zaidi ya 40.
Katika kusisitiza hilo, Chongolo alisema pindi wakandarasi watakapopatikana, mikataba ikasainiwe Karema mbele ya wananchi na si Dar es Salaam.
"Nimemwambia Waziri Bashungwa mkandarasi atakapopatikana waje kutia saini hapa Karema na wananchi washuhudie na siyo wafanyie Dar es Salaam. Wananchi waone hatua ambazo Serikali inafanya na hili nitalisimamia kuona linatekelezwa," alisema Chongolo
...Aweso aje ndani ya wiki mbili
Maji ni kero ambayo inaibuka kila eneo na ilianza katika Hospitali Teule ya Wilaya ambapo wananchi walilalamika kutokuwapo kwa maji licha ya chanzo chake kupatikana takribani kilomita saba.
Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi waazingira Vijijini (Ruwasa), Mkoa wa Katavi, Mhandisi Peter Ngunula alisema katika bajeti ya mwaka huu 2023/24 imetengwa Sh6 bilioni ambazo zitamaliza tatizo la maji.
Akiongeza katika hilo, Mbunge Kakoso ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bunge wa Kamati ya Miundombinu alisema msukumo unahitajika wa fedha hizo kutolewa na lakini eneo la Ikola kumekuwa na kusuasua kwani idadi ya wananchi imeongezeka tofauti na mahitaji yalivyo sasa.
Hoja ya maji ikaibuliwa tena akiwa katika mkutano wa Shina namba 5, Kata ya Kapalamsenga, Kata ya Kapalamsenga ambapo mwenyekiti wa shina hilo, Michael Lugelelo kuwa kuna tatizo kubwa la maji.
Kakoso akakazia akisema kuna mradi wa maji wa Sh1 bilioni, "lakini huu mradi hauendi vizuri kabisa."
Chongolo akamwita, Ngunula kuuzungumzia akasema unaendelea na umefikia asilimia 45,"na tunaendelea kumhimiza." Suala hilo lilimfanya Chongolo kumweleza kwanini wamuhimize wakati ni wajibu wake? Je, amekwisha kupewa fedha, akajibiwa hapana.
Kutokana na majibu hayo, Chongolo akasema,"mradi wa kwanza na huu wa pili naona kuna shida, nakwenda kumweleza Waziri (Aweso) ndani ya wiki mbili awe amekuja. Kama mkandarasi yuko asilimia 45 na hajapewa fedha, sasa namtaka waziri mwenyewe aje hapa na aje na fedha."
Alisisitiza,"wanawaziri kijana, mchapa kazi, sasa nataka kuona hili linafanyiwa kazi. Najua anajipenda, atajua cha kufanya mwenyewe katika hilo."
Uhaba wa watumishi
Hoja hii iliibuliwa na Mkuu wa Mkoa wa Katavi (RC), Mwanamvua Mrindoko wakati Chongolo akikagua ujenzi wa Hospitali teule ya wilaya ya Tanganyika kuwa ni Hospitali itakayohudumia wananchi wa mwambao wa ziwa Tanganyika.
"Hospitali hii ni muhimu sana. Lakini tukitegemea mapato ya ndani kuikamilisha itachukua muda mrefu sana, tunaomba usaidizi wa Serikali Kuu kupata fedha ili kuikamilisha," alisema RC Mrindoko huku akisisitiza mgawanyo wa watumishi wa afya waweze wapatikane.
Akijibu hilo, Chongolo alisema atazungumza na Tamisema wapeleke fedha haraka ili kuwawezesha kuikamilisha na wananchi waweze kupata huduma karibu zaidi kuliko kufuata huduma kilomita zaidi ya 100.
Kuhusu uhaba wa watumishi, alisema Tamisemi waige mfano wa wizara ya elimu kuwagawa walimu kwa uwiano sawa mijini na vijijini,"hili wameliweza, sasa mfumo huo utumike na kwenye kuwagawa watumishi wa afya. Sasa Tamisemi watafute watumishi kokote kule walete hapa Tanganyika."
“Najua tuna waziri wa mchakamchaka wa Tamisemi atasimamia hili. Tunataka mambo yaende na mimi nitasimamia," alisema Chongolo.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Iddi Kimanta alimkaribisha mkoani humo Chongolo pamoja na Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu kufuatilia utekelezaji wa Ilani na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kimanta aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha alisema, mengi yamefanyika mkoani humo na kupitia ziara hiyo, atayashuhudia.