Chongolo atua Katavi, aanza na Dk Biteko

Muktasari:
- Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo atakuwa na ziara ya siku tano mkoani Katavi na kwa kuanza, amemtaka Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kwenda mkoani humo kufuatilia kwa kina mradi wa ujenzi wa njia za umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Mkoa wa Tabora hadi Katavi.
Katavi. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amemtaka Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko kwenda mkoani Katavi kufuatilia kwa kina utekelezaji wa mradi kuunganishwa mkoa huo katika Gridi ya Taifa.
Amesema, haiwezekani mkoa huo umeunganishwa na barabara nzuri ya lami kutoka Tabora hadi Katavi halafu ukakosa umeme wa uhakika utakaochochea maendeleo ya mkoa huo ulioanzishwa mwaka 2012.
Chongolo ametoa maagizo hayo kwa Dk Biteko wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho waliojitokeza kumpokea katika ofisi za chama mkoani humo, leo jioni Jumatatu, Oktoba 2, 2023.
Amewasili mkoani humo kuanza ziara ya siku tano kuanzia kesho Jumanne Oktoba 3-7, 2023. Atatembelea majimbo yote matano ya Kavuu, Mpanda Vijijini, Nsimbo na kumalizia Mpanda Mjini ambayo wanayaongoza.
Baada ya kufika ofisini hapo na kupokea na vijana wa chama kwa kumvalisha skafu maalum ya CCM, kuangalia vikundi vya utamaduni kama vilivyokuwa Uwanja wa Ndege wa Mpanda alipowasili, Chongolo alifanya kikao cha ndani na viongozi mbalimbali.
Kikao hicho hakikuwahusisha waandishi wa habari, ambapo alipokea taarifa ya chama na Serikali iliyowasilishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mwamvua Mrindoko. Baadaye alitoka kuzungumza kwa ufupi lengo la ziara yake na taarifa hizo alizopewa.
“Nimekuja kufuatilia utekelezaji wa Ilani yetu ya mwaka 2020/25 ambayo ndani yake ndio imebeba ahadi za barabara, afya, umeme, kilimo, pembejeo na mambo mengi. Tuliahidi hivyo tunakuja kutembelea na kukagua miradi hiyo,” amesema Chongolo
Akiendelea kutoa salamu zake, Chongolo amesema amepokea taarifa ya chama pamoja na ya Serikali iliyowasilishwa Mkuu wa Mkoa huo, Mrindoko ikiwa na masuala mbalimbali ikiwemo changamoto ya mkoa huo kutokuwa na umeme wa uhakika.
Amesema katika taarifa zao mbili ya CCM na Serikali walizowasilisha viongozi hao wa chama na Serikali amedai wamesisitiza kuhusu suala la umeme ambayo imekuwa kero kwa wananchi na wawekezaji wanaotaka kuwekeza mkoani humo.
Chongolo amesema ameelezwa kumekuwa na ahadi zinazotolewa na viongozi mbalimbali ili kuusukuma kukamilika kwake lakini utekelezaji wake unasuasua na wao kama chama tawala waliahidi mikoa ya Katavi, Rukwa na Kigoma itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa lakini mkapa sasa ni Rukwa na Kigoma pekee imeunganishwa.
“Kigoma wamekwisha kuunganishwa kwa sehemu kubwa, Rukwa tayari, bado mkoa wa Katavi, niwaahidi mimi natamani kuchanguliwa kwa kishindo ndani ya mkoa huu,” amesema Chongolo huku akishangiliwa na sauti zikisikika, “tumkwisha kushinda babaaaa.”
Mara baada ya kueleza hayo, aliuliza mradi huo upo chini ya Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) au Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco)? Alijibiwa Tanesco.
“Basi niachieni mimi, nitakwenda kukaa na waziri anayehusika na hiyo Tanesco na bahati nzuri amepewa mamlaka makubwa kwa hiyo hana sababu ya kujitetea.
Nitakwenda kumwambia kwanza yeye mwenyewe aje aangalie uhalisia wa utekelezaji wa huu mradi lakini mbili ahakikishe anaweka nguvu zake zote hapo ili wananchi wa mkoa wa Katavi wajielekeze kupata umeme wa Gridi wa Taifa,” amesema Chongolo
Amesema, mkuu wa mkoa amemweleza watu wengi wanataka kuwekeza ikiwemo viwanda kama vya kuchakati alazeti lakini changamoto ni umeme wa uhakiki,”na sisi ni jukumu letu kuleta umeme na kazi yangu ni rahisi, kwenda kusimamia tuliyoyaahidi yanakwenda kutekeleza. Niwaambie tu nakwenda kusukuma mradi huu uwe historia.”
“Hatuwezi kuwa na barabara nzuri kutoka Tabora hadi hapa Katavi harafu nguzo tu za umeme zikatushinda, tutakuwa hatutendi haki dhamira zetu na Rais aliyetuamini kuwa wasaidizi wake kwenye maeneo mbalimbali,” amesema
Mradi huo uliwekwa jiwa la msingi Oktoba 2019 na Rais wa wakati huo, John Magufuli (aliyefariki Machi 17, 2021) wa kuunganisha mkoa wa Katavi kwenye Gridi ya Taifa kwa njia ya msongo wa Kilovolti 132 kutoka mkoani Tabora.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Iddi Kimanta amemkaribisha mkoani humo Chongolo pamoja na Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Ussi Gavu kufuatilia utekelezaji wa Ilani na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kimanta aliyewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Arusha amesema, mengi yamefanyika mkoani humo na kupitia ziara hiyo atayashuhudia.
Katika hilo, Chongolo aliwaeleza anachohitaji zaidi kusikia ni kuelezwa changamoto zilizpo “kuliko kusikiana ili changamoto hizi tuzichukue na kuzitafutia ufumbuzi.” Kauli hiyo iliwafanya wanachama waliokuwa wanamsikiliza kushangilia.