Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mwanzilishi wa TICTS azungumzia DP World

Muktasari:

  • Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi amesema anaunga mkono juhudi za Serikali kuipata kampuni DP World kuwekeza katika bandari.

Kagera. Aliyewahi kuwa Mbunge wa Bukoba Vijijini na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, amesema itakuwa ni jambo la ajabu kwa Tanzania kutochangamkia fursa ya kumpata mwekezaji mwingine katika bandari ili kuleta ufanisi wa utendaji na mapato.

Karamagi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera, ameyabainisha kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kanda ya Ziwa hivi karibuni na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Daniel Chongolo.

"Mimi ni Karamagi ambaye ni mwasisi wa kampuni ya TICTS ambayo wameizungumzia sana. Serikali zetu zote hazijafanya makosa katika uwekezaji ili Taifa letu linufaike. TICTS ilifanya kazi vizuri, ingawa kwa sasa tulipofikia Serikali imesema basi hebu tujaribu na wengine, jambo ambalo si baya,” amesema.

Amesisitiza kuwa uwezo wa TICTS kuhudumia bandari hiyo, hauwezi kumudu mahitaji ya sasa, huku akionesha umuhimu wa Tanzania kuchangamkia fursa ya mwekezaji mwingine atayakeboresha utendaji kazi na ufanisi wa bandari hiyo, huku ikitumika kimkakati kuongeza mapato ya nchi.

“TICTS wakati inaingia, bandari yetu ilikuwa na shehena ya makontena 70,000 kwa mwaka. Sasa hivi ni 700,000 kwa mwaka. Lakini tulipofika hapa, mkataba wetu ukafika mwisho. Sisi hatuna matatizo na hilo…nchi kwanza. Kwa sababu kuna mkakati mkubwa tunaweza kuwekeza sehemu nyingine,” amesema.

Akizungumza falsafa ya biashara, Karamagi amesema: “Serikali imewekeza zaidi ya Sh1 trililioni kwenye uboreshaji wa bandari gati 0 mpaka namba saba, mpaka leo hii, eneo hili linachangia kwa asilimia 15 ya makontena yote yanayotoka bandari ya Dar es Salaam.”

Mfanyabiashara huyo amesema kama hakuna jitihada za uwekezaji, mkopo huo hautalipika.

“Kwa mkopo mkubwa kama huu na watu binafsi wapo, ambao wana uwezo wa kuwekeza, kutulipa kodi na mafao mengine,  tukalipa deni hilo, alafu tukapata faida ya kuendeleza maeneo mengine, tutakuwa wajinga wa mwisho kama hilo hatutalichukua.”

Karamagi anayeamini katika falsafa ya biashara, alisema Tanzania inahitaji uwekezaji wenye manufaa utakaosaidia nchi kuitumia bandari kimkakati kuwa mojawapo ya vyanzo vitakavyoongeza mapato.

Sisi tulikaa pale (Bandari ya Dar Es Salaam) kwa miaka 22, tulinunua bandari? Si mkataba umekwisha, tunamwachia mwenye bandari, anatafuta wengine. Tulipokuwa pale tunaweza kusema bandari ni ya kwetu?” amehoji na kuongeza;

“Miundombinu ya bandari inabaki mikononi mwa Serikali. Kwa hiyo, hilo mtu asipolijua atachanganya uwekezaji, na ununuaji kama ilivyokuwa katika mashirika mengine.”

Kwa mujibu wa makubaliano ya Serikali ya Tanzania na Dubai yanayoweka msingi wa kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uboreshaji wa uendeshaji wa bandari ya Dar Es Salaam, mwekezaji atawekeza katika magati namba 0 hadi 7 pekee na siyo bandari yote.