Prime
Mchuano wa mawakili kesi mkataba uwekezaji wa Bandari ya Dar– 2

Muktasari:
- Katika sehemu ya kwanza ya simulizi hii ya mchuano wa mawakili katika kesi ya mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), pamoja na mambo mengine tuliona hoja (viini vya kesi) tano ambazo pande zote zilikubaliana kuwa ndizo hoja zinazobishwaniwa.
Mbeya. Katika sehemu ya kwanza ya simulizi hii ya mchuano wa mawakili katika kesi ya mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA), pamoja na mambo mengine tuliona hoja (viini vya kesi) tano ambazo pande zote zilikubaliana kuwa ndizo hoja zinazobishwaniwa.
Huu ni mkataba unaohusisha uwekezaji katika bandari za Tanzania, miundombinu yake na maeneo ya maalumu ya kiuchumi, na kampuni ya Dubai Ports World Limited (DP World au DPW) inayomilikiwa na Serikali ya Dubai.
Katika sehemu hii ya pili tutangalia jinsi mawakili walivyovutana kuhusu hadhi ya walioingia mkabata huo na hatimaye uchambuzi wa hoja moja baada ya nyingine.
Wakili wa walalamikaji, Mpale Mpoki baada ya kusoma hoja tano ambazo pande zote walikubaliana kisha aliitaja hoja ambayo walishindwa kukubaliana kuwa ijumuishwe kama sehemu ya hoja zinazopaswa kuamuriwa na mahakama, na kila upande utoe hoja zake kabla ya mahakama kutoa uamuzi.
Wakili Mpoki: Waheshimiwa majaji, jambo ambalo halijakubaliwa ambalo limetolewa na upande mmoja (walalamikaji) na upande mwingine (Serikali/walalamikiwa) haujaikubali, ni kama wahusika katika mkataba bishaniwa walikuwa na nguvu ya kisheria kuingia kwenye mkataba.
Jaji Mustafa: Katika hilo ambalo hamjakubaliana ni kwa nini hamjakubaliana, maana kama kuna ubishi hiyo ndio issue (hoja).
Wakili wa Serikali, Kalokola: Waheshimiwa majaji, hoja tulizokubaliana tumeangalia hoja zilizoletwa kwenye madai na sisi tumeona kuwa ni kweli haya ndiyo yanayobishaniwa.
Hoja kama pande husika walipoingia kwenye mkataba walikuwa na nguvu hatujaiona kwenye hati ya madai lakini, wenzetu wanasema kuwa ukisoma nyaraka zao ni kama wameiweka.
Lakini sisi tunasema haipo na hii ni kama kutushtukiza, maana msingi wa mambo yanayolalamikiwa ni yale yaliyoletwa kwenye madai.
Mpoki: Hapo ndipo ubishani ulipoanzia, sisi tunasema kwenye affidavity (kiapo cha walalamikaji) ukiisoma utayaona.
Ni rai yetu kwamba hili si kama shauri la madai ya kawaida ambapo kuna hati ya madai na WSD (majibu ya maandishi ya utetezi).Katika hili ( la kikatiba) fact (taarifa) zinapatikana kwenye affidavit (hati ya kiapo), na kwenye affidavit yetu hiyo ipo.
Kalokola: Waheshimiwa majaji bado ni msimamo wetu kuwa mtaona hoja inayoibuliwa inatoka kwenye kiapo ambacho ni ushahidi na hoja zinazobishaniwa hazitoki kwenye kiapo isipokuwa kwenye originating summons (hati ya madai)
Ndiyo maana hata katika nafuu na amri wanazoziomba halipo hili.
Mpoki: Waheshimiwa majaji, originating summons ni document (nyaraka) ya mahakama ambayo unaeleza ni nini unataka. Kwa hiyo hili huwezi kuweka kwenye originating summons, bali kwenye affidavit na ndiyo maana nao wamejibu. (kwenye kiapo kinzani cha Serikali)
Wakili Boniface Mwabukusi (wadai): Waheshimiwa majaji kwa unyenyekevu pleadings (nyaraka za madai) zinakuwa constituted (zinaundwa) na originating summons na affidavit. Huwezi kuleta originating summons tu bila affidavit, hizo ni nyaraka ambazo zinaambatana kwa pamoja.
Jaji Ismail: Sasa tunarudi issue (hoja) namba 4 kwamba Ibara ya 2 na ya 23 za IGA zinakiuka kifungu cha 25 cha Sheria ya Mikataba, tunataka kujua je, hivi huu ni mkataba? Ili tuweze kuona kama vinaendana kwa muktadha wa Sheria au mnamaanisha kitu kingine?
Sisi tunapendekeza issue namba 4 iwe, kama IGA ni contract; hoja ambayo ilikubaliwa na pande zote.
Hivyo jumla ya viini (hoja zinazobishaniwa) ambazo ndizo zitakazoamuriwa na mahakama zimekuwa sita na Jaji Ndunguru alirudia kuzisoma zote sita kuwa ndizo zilizokubaliwa, na alipendekeza hoja hiyo iliyoongezwa na mahakama ndiyo ya nne kwa mtiririko kwenye orodha hiyo.
Usikilizwaji rasmi
Katika hatua hii ulianza upande wa walalamikaji kuwasilisha hoja zake kwa kutoa ufafanuzi wa madai yake yaliyoko katika hati ya madai, ili kujibu hoja hizo sita zinazobishaniwa, moja baada ya nyingine kabla ya Serikali kujibu na kisha upande wa walalamikaji kujibu tena hoja zilizoibuliwa na Serikali kwa kila kiini.
Wakili Mpoki: Shauri hili limeletwa chini ya Ibara ya 108(2) ya Katiba ya Tanzania na kifungu cha 2(3) JALA (Sheria ya Usimamiaji Haki na Matumizi ya Sheria) vinayoipa Mahakama Kuu mamlaka kusikiliza suala kama hili.
Naomba nianze kiini namba mbili, kama umma uliarifiwa na kupewa muda wa kutosha.
Waheshimiwa majaji mkataba unaobishaniwa ulisainiwa Oktoba 25, 2022. Katika Ibara 25(2) wahusika wa mkataba walikubaliana ndani ya siku 30 upate ridhaa ya Bunge au Mahakama kuufanya uweze kutekeleza.
Kwa kufuata kifungu hiki mjibu maombi wa 4 (Katibu wa Bunge) Juni 5, 2023 alitoa taarifa kwa umma ufike kwa kusikilizwa kesho yake katika ukumbi wa Msekwa Dodoma, kwa muda wa saa 24 wananchi walitakiwa kwenda kutoa maoni yao.
Tangazo hilo halikuambatana na huo mkataba. Kwa hiyo kwa kifupi wananchi waliombwa kwenda kutoa maoni kwenye kitu ambacho hawakijui.
Logic (mantiki) ina demand (inataka) kwamba hilo tangazo lingeambatanishwa angalau na huo mkataba, hicho hakikufanywa.
Kutoa tangazo kwenye mitandao siyo njia sahihi kufikisha ujumbe kwa umma kwenda kutoa maoni kwa jambo ambalo linawahusu.
Saa 24 ni muda mfupi kuliona tangazo, kutafuta mkataba kuusoma kuuelewa kusafiri kutoka mtu aliko mpaka Dodoma kwenda kutoa maoni yake, ukizingatia kuwa pande husika zilikuwa na huu mkataba kuanzia Oktoba 25, ambao ni kipindi cha miezi 8.
Unakaa nao miezi 8 halafu unawapa wananchi saa 24 kutoa maoni, hilo ni jambo lisilowezekana.
Katika majibu ya kiapo cha waombaji, mjibu maombi wa nne anakubali kweli walitoa tangazo Juni 5, 2023 na wanakiri hawakuweka mkataba bali waliweka resolution (azimio) ya Bunge.
Sasa waliombwa kutoa maoni ya mkataba lakini wanatoa resolution za Bunge.
Katika aya ya 7 (katika kiapo kinzani- cha walalamikiwa wajibu maombi wanaieleza Mahakama hii kwamba watu 72 ndio waliotoa maoni kati ya watu 60 milioni kuhusu maliasili yao.
Tunaomba mahakama hii ichukulie kwamba kujitokeza watu 72 tu ni kwa sababu walipewa taarifa kwa muda mfupi.
Kwenye hili majibu yao wameonesha jedwali la hao watu 72 waliotoa maoni yao. Nadhani hii haitoshi.
Sheria inasema kama unamtaja mtu kwenye kiapo basi lazima naye kiapo chake kiwepo. Kwa hiyo walipaswa pia walete na viapo vyao (kuthibitisha); kuwa walikuwepo, vinginevyo hii inakuwa ni heresay ( uvumi) na tunadhani hata hao 72 hawakuwepo, na hearsay haipokewi mahakamani.
Msimamo huu umeelezwa katika kesi ya Dianarose Spareparts Ltd dhidi dhidi ya Commissioner General of Tanzania Revenue Authority (Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, Civil Application number (shauri la maombi namba) 245 la mwaka 2021.
Mahakama ya Rufani (katika uamuzi wake Desemba 19, 2022) walisema kama mtu anatoa kiapo unamtaja mtu mwingine, mtu huyo pia anapaswa kutoa kiapo.
Waheshimiwa majaji notice (taarifa) ni suala ambalo linazungumziwa katika Kanuni za Bunge, kanuni 108(2), kwamba kamati itatoa mwaliko kwa mtu anayetakiwa kufika mbele ya kamati hiyo ili kutoa uchambuzi wa suala husika. Kwa hiyo notice isichukuliwe kama kitu kidogo.
Katika kusisitiza umuhimu wa notice hiyo, wakili Mpoki aliielekeza mahakama katika kesi mbili za nje, moja iliyoamuriwa na Mahakama ya Uingereza na nyingine Mahakama ya Marekani, ambazo alizisoma sehemu inayozungumzia sheria hiyo kisha akaendelea:
Notice ni mchakato ambao anayetakiwa kutoa ushauri, anatakiwa aelezwe ni kitu gani anatakiwa kuzungumzia, apewe muda wa kutosha kujitayarisha, aruhusiwe kushiriki na hata maoni yake yaoneshwe kwenye deliberation (majadiliano).
Hivyo muda anaotakiwa mtu kupewa ni kitu cha muhimu sana kumfanya kushiriki kama ambavyo sheria inataka.
Mkataba huu unahusu sea port, lake port (bandari za kwenye bahari na maziwa) na economic zones (kanda za kiuchumi) ambazo ziko Dar es Salaam, Bagamayo Mtwara (na kwingineko).
Tulitegemea mdaiwa wa 4 atoe taarifa ya kutosha kuwafanya watu wote wanaotoka katika maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa wangeshirikishwa katika mkataba huu, wafike kutoa maoni kuhusu maliasili zao. Kwa kuangalia jedwali hili ambalo tunasema ni heresay, hicho kitu hakikufanyika na tunaona kwamba participation (ushiriki) hata ya hao watu 72 hawakuwepo.
Kwa msingi huo notice ni suala la natural justice (haki ya asili) kwamba tunataka kubinafsisha kitu chako hiki, kwa hiyo inapofanyika bila kuzingatia principal ya natural justice (kanuni ya haki asili) mahakama haiwezi kulifumbia macho.
Ni rai yangu mahakama ione haikuwepo notice na participation ya wananchi na kama ilikuwepo basi haukutolewa muda wa kutosha na hivyo watu hawakushirikishwa katika maliasili yao.
Kesho tutaendelea na sehemu ya tatu ya uchambuzi wa kesi hii ambayo uamuzi wake umepangwa kutolewa Agosti 7, 2023.