Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mchuano kesi ya Mkataba wa Bandari kuendelea tena leo

Muktasari:

  • Serikali kuendelea kujibu mapigo  ya hoja  katika kesi ya. mkataba wa bandari, lakini mawakili wa upande wa madai nao watapata nafasi kujibu hoja za Serikali.

Mbeya. Mchuano wa hoja baina ya mawakili wa pande zote katika kesi ya makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii, kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai (IGA) unaendelea tena mahakamani leo Alhamis Julai 27, 2023.

Usikilizwaji wa kesi hiyo leo uko hatua ya kupangua hoja. Serikali inaendelea kujibu mapigo kwa kujaribu kupangua hoja za upande wa wadai, zilizowasilishwa jana.

Jana Jumatano Julai 26, 2023 mawakili hao wa upande wa madai, Mpale Mpoki, Boniface Mwabukusi,Philipo Mwakilima na Livino Ngalimitumba walichambua Ibara zote za mkataba huo wanazozipinga na kuonesha kile wanachidai masharti mabovu yasiyo na maslahi kwa Taifa na jinsi unavyokiuka sheria na Katiba ya Nchi.

Katika hoja zao walitoa ufafanuzi wa madai yao ili kuishawishi mahakama kuwa mkataba huo ni batili kwa kuwa na ibara hizi zina masharti yanayokiuka Sheria za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili za Nchi, Katiba na kwamba unaondoa ukuu wa Nchi na kuiweka chini ya Dubai na vile vile kuathiri Maliasili za Taifa na kuhatairisha usalama wa Taifa.

Pia walifafanua madai yao ya mchakato wa kuridhiwa na Bunge ulivyoikuka Sheria kwa kutowapa wananchi kwanza nafasi ya kutoa maoni yao  kabla ya kuridhiwa kama Sheria zinavyoelekeza.

Vilevile walifafanua madai yao kuwa ni batili kutokana kwa madai kwamba Dubai haina mamlaka kuingia mkataba wa Kimataifa kama huu kwa mujibu wa Ibara ya 123 ya Katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kwamba jukumu hilo linapaswa kufanywa na Serikali ya Umoja huo.

Katika kujenga hoja zao kuishawishi mahakama.ikubakiane na hoja zao mawakili hao waliotumia nyaraka mbalimbali za kitaifa na za Kimataifa.

Nyaraka ni pamoja na  Katiba ya Tanzania, Sheria ya Manunuzi ya Umma, (R.E 2022), Kanuni za Kudumu za Bunge za mwaka 2023, Sheria ya Mikataba, Sheria ya Tafsiri ya Sheria na Sheria za Ulinzi wa Raslimali na Maliasili namba 5 na namba  6 za  mwaka 2017.

Nyingine ni hukumu mbalimbali za Mahakama Kuu ya Tanzania na za Mahakama ya Rufani, hukumu za mahakama za nje zinazotumia mfumo wa sheria zinazotumika nchini, Katiba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ya mwaka 1996 na Mikataba ya Kimataifa

Baada ya kuhitimisha hoja zao, Serikali nayo ilianza kujibu ikitoa ufafanuzi uliolenga kupangua  hoja za wadai ili kuishawishi mahakama kuwa hoja zao hazina mashiko.

Hata hivyo Serikali haikumaliza jana kujibu hoja zote za upande wa madai kwani kati ya hoja Sita zinazobishaniwa na ambazo ndizo zitakazoamuriwa na Mahakama, iliweza kujibu hoja mbili tu.

Hoja hizo ilizozijibu ni kama IGA (makubaliano hayo yaliyosainiwa yanayobishaniwa)  ni mkataba kwa muktadha wa Sheria ya Mikataba na kama Ibara ya 2 na 23 ya hiyo IGA inakiuka Sheria ya Mikataba Nchini.

Wakili Stanley Kalokola pamoja na mambo mengine alidai kuwa huo ni mkataba wa Kimataifa hivyo husimamiwa na Sheria za Kimataifa na kwamba Dubai ina mamlaka ya kuingia mkataba huo.

Naye alirejea Katiba ya UAE Ibara ya 116 inayoeleza kwamba mambo ambayo si ya Muungano yako chini ya Nchi wanachama.

Hivyo leo Serikali inaendelea kujibu hoja nne zilizobaki katika mwelekeo uleule wa kutoa ufafanuzi unaolenga kuzipangua na kuishawishi mahakama kuwa nazo hazina mashiko.

Hata hivyo wadai watakuwa na nafasi nyingine zao ya wao pia kujibu hoja zilizoibuliwa na Serikali wakati ikijibu hoja zao; nao wakitoa ufafanuzi kwa lengo la kupangua hoja hizo za Serikali.

Kesi hiyo imefunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya na  mawakili wanne kutoka mikoa tofautofauti, Alphonce Lusako, Emmanuel Chengula, Raphael Ngonde na Frank Nyalus dhidi ya Serikali.

Wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ambaye ni mshahri wa Serikali kwa mauslanya kisheria, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi,  Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na Katibu wa Bunge la Tanzania, ambaye ni mtendaji mkuu na mratibu wa shughuli za Bunge.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba namba 5 ya mwaka 2023 wanapinga makubaliano hayo  yanayohusha uwekezaji katika Bandari za Tanzania zilizoko katika mwambao wa bahari na katika maziwa, kuwa ni batili kwa kuwa yana Ibara zinazokiuka Sheria na Katiba ya Nchi.

Pia wanadai kuwa mchakato wa kuridhia Bungeni ni batili kwa kuwa haukufuata utaratibu wa kisheria na bila kuwapa nafasi ya kutosha wananchi kutoa maoni yao kama sheria za Nchi zinavyoelekeza.

Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la majaji watatu, Dunstan Ndunguru( Kiongozi wa jopo), Mustafa Ismail na Abdi Kagomba