Dawa ya malaria kwa watoto wachanga yaidhinishwa

Muktasari:
- Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria Tanzania, Dk Abdallah Lusasi amesema watoto ni kundi lililo katika hatari ya kupata maambukizi ya malaria, hivyo ujio wa dawa ni faraja.
Dar es Salaam. Baada ya muda mrefu wa kukosekana dawa ya malaria iliyoidhinishwa kwa ajili ya watoto wenye uzito chini ya kilo tano, Kampuni ya Novartis ya Uswisi imetangaza kuidhinishwa kwa dawa ya Coartem (artemether-lumefantrine) Baby kwa ajili yao.
Watoto hao walikuwa wakipewa dawa zilizokusudiwa kwa wenye umri mkubwa, hali iliyoongeza hatari ya kuzidisha dozi au sumu mwilini. Chanjo za malaria pia bado hazijaidhinishwa kwa watoto wachanga.
Dawa hiyo inayojulikana pia Riamet Baby katika baadhi ya nchi ikiwamo Uswisi, imetengenezwa kwa msaada wa kisayansi na kifedha kutoka Shirika la Medicines for Malaria Venture (MMV), taasisi isiyo ya kiserikali ya Uswisi inayojihusisha na utoaji wa dawa za kutibu, kuzuia na kutokomeza ugonjwa wa malaria unaoenezwa na mbu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa jana Julai 8, 2025 kwenye tovuti ya Novartis, dawa hiyo maalumu kwa ajili ya watoto wachanga na walio na umri mdogo imeidhinishwa na Wakala wa Uswisi wa Bidhaa za Tiba (Swissmedic).
Dozi mpya mahususi kwa watoto wachanga inaelezwa huyeyuka kwa urahisi hata ndani ya maziwa ya mama na ina ladha ya cherry tamu.
Nchi nane za Afrika zilizoshiriki tathmini ya dawa hiyo zinatarajiwa kutoa vibali haraka kwa ajili ya matumizi ya tiba hiyo kupitia mpango maalumu wa afya ya kimataifa unaoendeshwa na Swissmedic.
Mataifa hayo manane yaliyoshiriki kwenye tathmini ni Burkina Faso, Ivory Coast, Kenya, Malawi, Msumbiji, Nigeria, Tanzania na Uganda.
Novartis inapanga kuanza usambazaji wa Coartem Baby kwa misingi isiyo ya kibiashara ili kuongeza upatikanaji wa tiba katika maeneo yenye maambukizi ya malaria.
“Kwa zaidi ya miongo mitatu, tumeendelea kupambana na malaria, tukifanya kazi bila kuchoka kuhakikisha tunafanikisha mafanikio ya kisayansi kule yanapohitajika zaidi,” amesema Vas Narasimhan, Mkurugenzi Mtendaji wa Novartis na kuongeza:
“Kwa kushirikiana na wadau wetu, tunajivunia kuendeleza tiba ya kwanza ya malaria iliyothibitishwa kitabibu kwa watoto wachanga na wenye umri mdogo, kuhakikisha hata walio dhaifu zaidi wanapata huduma wanayostahili.”
Taarifa hiyo inaeleza kuwa hapakuwa na dawa yoyote ya malaria iliyoidhinishwa kwa watoto walio na uzito wa chini ya kilo 4.5, jambo lililosababisha pengo la tiba.
Kila mwaka, takribani watoto milioni 30 huzaliwa katika maeneo yenye hatari ya malaria barani Afrika.
Kampuni hiyo imeeleza kuwa, utafiti mkubwa katika Afrika Magharibi ulionyesha viwango vya maambukizi kati ya asilimia 3.4 hadi 18.4 kwa watoto chini ya miezi sita. Hata hivyo, bado kuna uhaba wa takwimu kuhusu malaria kwa watoto wachanga kwa sababu mara nyingi hawajumuishwi katika majaribio ya dawa za malaria.
“Dawa zilizopo za malaria zimejaribiwa ipasavyo kwa watoto kuanzia miezi sita na kuendelea, kwa sababu watoto wachanga mara nyingi huachwa nje ya majaribio hayo,” amesema Profesa Umberto D'Alessandro, Mkurugenzi wa kituo cha MRC Unit, Gambia.
Amesema: “Hii ni muhimu kwa sababu watoto wachanga huwa na ini lisilokomaa, hivyo huchakata dawa tofauti na watoto wakubwa (ambao hawajakomaa kiumri) na dozi yao inaweza isiwe sahihi kwao.”
Kuhusu utafiti
Kibali cha Swissmedic kinatokana na matokeo ya utafiti wa CALINA wa awamu ya II/III, uliolenga uhusiano mpya wa viambato na dozi ya Coartem ili kuzingatia tofauti za kimetaboliki kwa watoto chini ya kilo tano.
Tiba hiyo imelenga watoto wachanga (waliwamo wa siku chache baada ya kuzaliwa) wenye uzito kati ya kilo mbili hadi chini ya kilo tano.
Novartis ilizindua Coartem kwa ajili ya kutibu malaria mwaka 1999 na sasa imetengeneza dozi mpya mahususi kwa ajili ya watoto wachanga.
Akizungumza na Mwananchi leo Julai 9, 2025 Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria, Dk Abdallah Lusasi amesema watoto ni kundi lililo katika hatari ya kupata maambukizi ya malaria, hivyo ujio wa dawa hiyo ni faraja.
“Tuna mikoa mitano yenye maambukizi ya juu ya malaria ambayo ni Tabora, Mtwara, Kagera, Shinyanga na Mara. Watoto wanapata madhara na dawa zetu zinaanzia watoto wenye kilo tano, sasa kuna watoto wana uzito chini ya kilo 4.5 wanazaliwa wadogo wakiwa na malaria hivyo dawa hii itakuwa msaada,” amesema.
Dk Lusasi amesema dawa hiyo itakuwa na manufaa kwa nchi ambazo malaria bado ipo juu, akibainisha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa huo nchini ni asilimia 8.1 ikiwa kati ya wagonjwa 1,000 miongoni mwao 53 wana maambukizi ya malaria, huku vifo vikiwa ni asilimia 2.4 kati ya watu 100,000.
Amesema mama anapokwenda kliniki hupewa chandarua ambacho hushauriwa kukitumia kwa miaka miwili lakini mtoto akipata malaria hutibiwa, hivyo ujio wa dawa za watoto kutibu malaria ni faraja.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, mwaka 2021/22, malaria ni miongoni mwa magonjwa 10 yaliyoongoza kwa wagonjwa kulazwa kwa watu wenye umri wa miaka mitano au zaidi na wa pili kwa kulaza watoto chini ya miaka mitano.