Siku 14 za usafirishaji SGR ya mizigo watumiaji waeleza mafanikio, changamoto

Muktasari:
- Juni 27, 2025 treni ya kwanza ya mizigo ya reli ya kisasa (SGR) ilianza safari ikitokea Dar es Salaam, kwenda stesheni ya Ihumwa, Dodoma ikiwa na mabehewa 10 na kubeba tani 700 ya mzigo.
Dar es Salaam. Wakati treni ya kwanza ya mizigo ya reli ya kisasa (SGR) ikitimiza siku 14 tangu kuanza usafirishaji wadau wa sekta hiyo nchini wameeleza mafanikio na changamoto ambazo Shirika la Reli Tanzania (TRC), linapaswa kuzifanyia kazi ili kuboresha huduma hiyo.
Kwa mara kwanza Juni 27, 2025 treni ya kwanza ya mizigo ya reli ya kisasa (SGR) ilianza safari ikitokea Dar es Salaam, kwenda stesheni ya Ihumwa, Dodoma ikiwa na mabehewa 10 na kubeba tani 700 za mzigo.
Kwa mujibu wa mkuu wa kitengo cha Habari na Uhusiao TRC, Fredy Mwanjala tangu kuanza kwa treni hiyo, TRC ina safari moja kila siku huku usafirishaji ukitarajiwa kuongezeka kulingana na mahitaji.
Mwanjala amesema hivi sasa wasafirishaji wakuu wa treni hiyo ni Azania na Dangote huku wakiendelea kuhamasisha wengine kutumia usafiri huo.
Alipoulizwa kuhusu tathimini ya usafiri huo tangu umeanza hadi sasa, Mwanjala amesema, "SGR ya mizigo imeanza kama tulivyoanza kwenye ile ya abiri, ilianza kidogokidogo hadi sasa usafirishaji ni wa kiwango cha kuridhisha.
"Kwenye SGR ya mizigo napo tunakwenda hivyo, tulianza kwa majaribio ya kiufundi, kisha tumekuja kwenye operesheni, ambayo nayo ni kama majaribio ya pili, tunabeba mizigo kidogokidogo," amesema.
Amesema katika operesheni mwitikio ni mzuri, walianza kubeba mizigo ya Azania na sasa Dangote pia anasafirisha mizigo yake ya Dodoma kutumia SGR.
"Kadri tunavyoendelea tutaongeza ruti na mabehewa kulingana na mahitaji ya usafirishaji yatakayokuwepo, kwa sasa wasafirishaji wetu wakuu ni hao," amesema.
Wasemavyo wadau
Mkurugenzi wa Biashara na Mawasiliano wa Azania Group, Joel Laiser akizungumzia usafirishaji wa treni hiyo, ameeleza kuwa imekuwa msaada wa kusafirisha mizigo mingi kwa wakati mmoja.
Amesema kwanza ni uwezo wa kubeba tani nyingi katika behewa moja, akibainisha kwamba behewa moja la SGR linabeba hadi tani 75.
"Pia imeturahisishia kwenye muda, kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kwa SGR tunatumia saa nne, tofauti na njia ya barabara tulitumia hadi siku tatu," amesema.
Amesema eneo la kusushia mzigo pia ni la kiwango bora na nafasi ya kutosha kupaki malori mengi.
"Changamoto iliyopo ni kutokuwa na eneo la kuhifadhia mizigo baada ya kushushwa, mfano sisi Azania kutoka Ihumwa hadi kufika warehouse (ghala la kuhifadhi mizigo) ni kama kilomita 20, kunakuwa na kazi ya kushusha Ihumwa, kisha kupakia hadi lilipo ghala kabla ya kuisambaza maeneo tofauti.
Laiser amesema kama TRC itaweza kujenga maghala jirani na Ihumwa itasaidia kupunguza usumbufu kwa wasafirishaji.
Hata hiyo ameeleza kwamba kuanza kwa treni hiyo ya mizigo kumesaidia pia ufikishaji wa mizigo kwa wateja wa mikoa ya Singida, Tabora, Kahama, Shinyanga ambao sasa wanachukulia mizigo Dodoma.
"Hii imesaidia kupungua kwa bei na muda na kuongeza mzunguko wa biashara na viwanda kuongeza uzalishaji.
Naye mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shaban amesema kuanza kwa SGR ya mizigo kwao wanaichukulia ni fursa ya kuongeza usafirishaji.
"SGR haiwezi kubeba mizigo yote, hivi sasa inaishia Dodoma, sisi Tamstoa tunaombea ifike nchi nzima, ikibeba mizigo mingi ndipo na sisi wenye malori itatufungulia fursa kwani kuna ile mizigo inayokwenda kwenye nchi takriban nane tulizopakana nazo, hivyo bado wote tutafanya biashara," amesema.