Chalamila azungumzia katikakatika ya umeme, ubovu wa barabara

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amezungumzia tatizo la umeme na ubovu wa barabara mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan kwenye utoaji wa tuzo za Rais kwa wazalishaji bora.
Dar es Salaam. Wakati wananchi wakilalamika katikakatika ya umeme, ubovu wa barabara na mambo mengine, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila amesema changamoto hiyo inakwenda kutatuliwa baada ya kukamilika baadhi ya miradi.
Chalamila amesema hayo leo Jumapili usiku, Desemba 17, 2023 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya utoaji tuzo za Rais kwa wazalishaji bora zinazofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema kulikuwa na barabara ambayo ilikuwa inasumbua kutoka Kibada, Mwasonga hadi Kimbiji katika Wilaya ya Kigamboni imeshapata mkandarasi na itatengenezwa kwa kilometa 41 na itahudumia hadi Kisarawe II.
Amesema umeme umekuwa ukikatika lakini mradi wa kituo cha Kinyerezi I ambao unazalisha megawati 185 umekamilika kwa hiyo tatizo la umeme litakwisha hivi karibuni.
"Rais uliagiza transifoma kubwa mbili moja ya MVA 175 na hii itasaidia kuhakikisha umeme unasafirishwa kirahisi, vizuri kwenye msongo wa usafirishaji umeme wa kilovolti 132 na hivyo kusaidia maeno ya Dege, Mbagala na Gongolamboto," amesema Chalamila.
Amesema maeneo hayo yamekuwa na tatizo kubwa la umeme, hivyo tatizo linakwenda kupungua kwa kasi na itakuwa ni mchango kwa wamiliki wa viwanda.
Pia, mkuu huyo wa mkoa amesema yale yaliyoagizwa na Rais Samia ni kuongeza vituo vya umeme vya kuhudumia viwanda vyote vilivyopo eneo la Kisarawe II.
Mbali na hicho, kituo kingine ni cha Tazara ambacho kitasaidia maeneo yaliyopo karibu na eneo hilo na kituo kingine cha Gongolamboto ambacho kitasaidia baadhi ya maeneo mengine yenye ukuaji mkubwa wa viwanda ikiwepo Chanika.
Chalamila amewakaribisha watu wote kuendelea kuwekeza katika jiji hilo akisema bado kuna maeneo yenye fursa nyingi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirikisho la Viwanda Tanzania (CTI), Leodegar Tenga amesema lengo la tuzo hizo ni kutambua, kuenzi na kuthamini umuhimu wa mchango wa sekta ya viwanda katika maendeleo ya nchi.
"Mchakato wa kuwapata washindi wa tuzo unachangia kuongeza ushindani viwandani na ushindani wa bidhaa zetu katika soko la ndani na nje ya nchi," amesema Tenga.
Amesema vigezo vya mshindi wa tuzo hizo ni ufanisi katika uzalishaji, mauzo ya nje na uzalishaji wa fedha za kigeni, uwekezaji katika teknolojia ya kisasa, matumizi bora ya nishati, utunzaji wa mazingira, afya, usalama wa wafanyakazi.