Chalamila apongeza ubunifu wa uongozi wa Tanesco Saccos kuanzisha visa kadi

Muktasari:
- Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila atoa kongole kwa uongozi wa Tanesco Saccos kwa kuja na ubunifu wa kuanzisha visa kadi itakayowanufaisha wanachama wao.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amezindua kadi ya Visa kwa ajili ya wanachama wa chama cha akiba na mikopo cha Tanesco Saccos, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa waadilifu katika utendaji wa kazi zao.
Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye uzinduzi wa matumizi ya kadi hiyo yaliyoenda sambamba na mkutano Mkuu wa 55 wa Tanesco Saccos, Chalamila aliwapongeza kwa kuanzisha huduma hiyo ya kadi na kusema kuwa watakuwa katika hadhi ya kimataifa.
"Nadhani nyie ni Saccos ya kwanza kuzindua kadi hii, mnatoka ndani na mnaingia kimataifa niwapongeze sana kwa hilo kwasababu popote unapokuwa hata nje ya nchi mnaweza kuhamisha fedha jambo ambalo ni zuri na hongereni sana,"alisema.
Pamoja na hayo, Chalamila aligusia suala la uadilifu kwa watendaji akisema wengi wanalinganisha na umaskini lakini ni muhimu katika utendaji kazi kuwezesha Saccos kuwa imara.
“Nahimiza umuhimu wa kutumia Saccos yenu kama chanzo cha kuongeza mapato na kubadilisha maisha yenu kiuchumi kwa kufanya vitu vinavyoonekana,”alisema.
Awali, Mwenyekiti wa Tanesco Saccos, Somoe Nguhwe amesema ni mkutano mkuu wa mwaka na tukio muhimu la kisheria lianalowakutanisha viongozi, watendaji wa chama na wawakilishi na kutoa ripoti mbalimbali zinazoonyesha utendaji wa chama kwa mwaka uliopita.
Amesema kupokea na kujadili taarifa ya makadrio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024 na kupitisha maazimio kwa ajili ya utekelezaji kwa mwaka fedha ujao.
"Mwaka 2022 ulikuwa na changamoto nyingi za kiutendaji iliyozalisha matokeo mchanganyiko yakiwemo hasi na chanya katika utendaji wa shughuli za chama ikiwemo changamoto ya ukwasi katika chama iliyosababishwa na kuimarika kwa wigo wa kukuopesha kwa wanachama imepelekea utoaji wa huduma za mikopo kuwa na foleni kusababisha wanachama kutofikia malengo ya mikopo,"amesema.
Alisema Tanesco Saccos idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 6,063 mwaka 2021 hadi kufikia 6,354 sawa na asilimia 4.8.
Aidha amesema akiba za wanachama zimekua kutoka Sh41.1 bilioni kwa mwaka 2021 hadi kufikia Sh41.9 bilioni mwaka 2022 na kufanya ongezeko la asilimia 5.2 na chama kimetoa faida juu ya akiba na hisa za hiyari kiasi cha Sh1.5 bilioni.
"Jumla ya mkopo yote iliyotolewa katika mwaka 2022 ilifikia Sh57.1 bilioni ikalinganishwa na mwaka mwaka 2021 ilikuwa Sh48.9 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 16.8," alisema.
Aliongeza kuwa mpango mkakati wa chama kwa kipindi cha miaka mitano mwaka 2024/28 ikiwa ni mpango wa tatu kutekelezwa na chama umejikita kulinda na kukuza mafanikio yote yaliyopatikana katika mipango ya kabla.