Chalamila ataja manufaa ushirikiano Dar, Shaanxi

Muktasari:
- Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila ameeleza faida itakazozipata Dar es Salaam kufuatia kutia saini makubaliano ya awali ya mashirikiano kati ya mkoa huo na mji wa Shaanxi wa China, zikiwemo faida za kiuchumi.
Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameeleza mafanikio yanayotazamiwa kufuatia makubaliano ya awali yanayohusu mashirikiano kati ya Dar es Salaam na mji wa Shaanxi wa China.
RC Chalamila ameeleza hayo Jumatatu, Novemba 27, 2023 Dar es Salaam, kwenye hafla ya utiaji saini makubaliano hayo. Amesema makubaliano hayo ya awali yanalenga ushirikiano kwenye sekta ya viwanda na biashara.
"Tumeona ni muhimu kuendelea kupanua wigo wa ushirikiano na majiji mengine ili kuongeza uwezo wetu katika nyanja mbalimbali," amesema Chalamila.
Amesema Shaanxi, mji anaotoka Rais wa sasa wa China, Xi Jinping ni wenye rasimali nyingi, hivyo Dar es Salaam ina mengi ya kujifunza kutoka mji huo.
"Tunatarajia wimbi kubwa la viwanda hapa nchini na wafanyabiashara zaidi kutoka China kuja Dar as Salaam na kwa mantiki hiyo, fursa nyingi za kiuchumi zitafunguka," amesema Chalamila.
Amesema hatua hiyo ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufungua mikoa, kukaribisha uwekezaji ili kuongeza fursa kwa wakazi wa mikoa.
"Ushirikiano unakuwa kwenye sekta nyingi ikiwemo uchimbaji madini, kilimo, elimu, afya, miundombinu, biashara na viwanda," amesema.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa, kinachosubiriwa sasa ni kupitiwa kwa makubaliano hayo ya awali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kabla ya kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema Dar as Salaam ni sehemu muhimu katika ushirikiano hayo kwani sehemu ambayo wawekezaji kutoka Shaanxi wangependa kuwekeza.
"Ninaamini Dar es Salaam ni sehemu ambayo wafanyabiashara wa Shaanxi watachagua kuwekeza, ikizingatiwa ni mji ulio ukingoni kwa Bahari ya Hindi ambayo ni muhimu kwa ajili ya uwekezaji," amesema
Pia, amesema Dar es Salaam itapata fursa ya kupata uzoefu kutoka katika sekta ya elimu na viwanda, maeneo ambayo Shaanxi imefanikiwa.
"Tunaamini makubaliano haya yatakuwa ya manufaa kwa pande zote mbili kwani kila upande utanufaika kutokana na rasilimali zilizoko kwenye miji yote miwili," amesema Mingjian