CCM yataka Serikali kuweka mikakati ya kuongeza ajira, kipato

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi (wa kwanza kulia) wakati akikagua nyanya za umeme katika cha Tanga Cable Limited leo Juni 8, 2024.
Muktasari:
- Katibu Mkuu wa CCM Dk Emmanuel Nchimbi ametoa maelekezo hayo, wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha nyaya za umeme mkoani Tanga.
Tanga. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeitaka Serikali kuendelea kuweka mikakati madhubuti na wezeshi kwa sekta binafsi ili ichochee ajira na pato la wananchi na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Jumamosi, Juni 8, 2024 na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi wakati akizindua kiwanda cha kwanza cha kuzalisha nyaya za umeme ukanda wa kaskazini mwa Tanzania, kilichopo Mkoa wa Tanga kinachoitwa 'Tanga Cable Limited.'
Katika uzinduzi wa kiwanda hicho uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali, imeelezwa kitapunguza gharama kwa wahitaji kwa maana ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na au Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) na makandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme katika mikoa ya kaskazini (Tanga, Manyara, Arusha na Kilimanjaro).
"Sisi katika chama tunatambua hakutakuwa na mafanikio ya kweli kama sekta binafsi haitashirikishwa kikamilifu na sisi tunafurahi kuona wazawa wanawekeza," amesema Dk Nchimbi.
Amesema kwa sasa kuna changamoto ya kuagiza bidhaa nyingi nje ya nchi lakini kuanzishwa kwa viwanda kama hivyo mbali na kupunguza gharama za kuagiza nje, vinaongeza ajira kwa vijana wetu na kuongeza pata la Taifa.
Dk Nchimbi amesema ilani ya uchaguzi ya CCM inaeleza kuweka mazingira mazuri kwa kujenga viwanda vidogo na vikubwa.
Akijibu wito wa kiwanda hicho kuwezeshwa kwa bidhaa hizo kununuliwa, Dk Nchimbi amesema:"
‘’Kwa taasisi mbalimbali za Serikali na sekta binafsi, jitihada za wazawa kama hawa, tusiwarudishe nyuma, tutumie bidhaa zetu kama ni bora na viwanda kama hivi havijaanzishwa kama mapambo."
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tanga Cable, Murtaza Dossaji amesema zaidi ya Sh1 bilioni zimetumika kuanzisha kiwanda hicho ambacho kinatarajia kutoa ajira zaidi ya 50.
"Hiki ni kiwanda pekee kwa mikoa ya kaskazini mashariki, Tanesco kanda ya kaskazini na makandarasi wa Rea ambao wamepata kazi katika kanda hizo watapata nafuu ya kupata nyaya hizo karibu na kwa bei nafuu," amesema Dossaji na kuongeza:
"Tunaiomba Serikali, wahandisi na makandarasi wanunue nyaya zetu ili kuongeza mapato, ajira na kukuza mapato ya Taifa."
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batlida Burian amesema kiwanda hicho ni miongoni kwa viwanda wanavyotaka wavilee, kwani mwanzo kulikuwa na viwanda vingi mkoani humo lakini vikabaki magofu.
Awali, Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdulrahman amesema wao wanaosimamia utekelezaji wa Ilani, wanaridhika jinsi Rais Samia Suluhu Hassan anavyotekeleza kwa vitendo ikiwemo sekta ya viwanda.
Amesema kwa sasa mkoa wa Tanga wamewaita wale wote waliokuwa na viwanda na kuvifunga.