Carlos amgeuka Moukharbal, amuua (8)

Muktasari:
- Waliposhindwa kutekeleza majaribio mawili ya kulipua ndege mbili za Israeli katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Orly nchini Ufaransa, Carlos na Michel Moukharbal walikwenda kujipanga upya.
Kama tulivyodokeza katika toleo lililopita, Carlos alijituliza jijini Paris akitumia muda wake mwingi kutafuta maeneo mengine ya kushambulia wakati Moukharbal akifanya safari zake za kawaida kwenda makao makuu ya PFLP, Beirut, Lebanon.
Hata hivyo, Juni 7, 1975, Moukharbal alikamatwa na polisi wa Lebanon katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Beirut alipokuwa akijiandaa kupanda ndege kurejea Paris.
Baada ya mahojiano ya siku mbili mfululizo, Ijumaa ya Juni 13 walimwachia kuondoka kurejea Paris. Alipanda ndege kwenda Ufaransa bila kujua kuwa kulikuwa na polisi wa siri wa Lebanon aliyekuwa akifuatilia nyendo zake tangu alipopakiwa kwenye ndege.
Mara tu baada ya ndege kutua Paris, afisa huyo wa Lebanon aliwapa ishara maofisa wa Kurugenzi ya Upelelezi ya Ufaransa (DST) waliokuwa wakimngojea.
Maofisa hao walimfuata Moukharbal alipochukua teksi kwenda Latin Quarter hadi alipoingia kwenye nyumba moja ambayo muda mfupi baadaye alitoka na mwanamume mwingine aliyemsaidia kubeba mkoba. Muda wote huo maofisa wa DST walikuwa wakipiga picha.
Juni 20, wakati nyendo zake zinafuatiliwa, Moukharbal aliondoka Paris na kwenda London. Walipotambua kuwa mtu wanayemfuatilia amesafiri kwenda London, DST ililitaarifu tawi lao maalumu la London ambako walimkamata na kumrejesha Paris siku iliyofuata, Juni 21.
Maofisa hao walipomfikisha Moukharbal mjini Calais, kaskazini mwa Ufaransa, aliwekwa chini ya ulinzi mkali na kuhojiwa na kikosi cha ujasusi Ufaransa (RG).
Awali Moukharbal aligoma kutoa ushirikiano, lakini siku saba baadaye, baada ya kutishiwa kuwa atarejeshwa Beirut ambako wakubwa zake hawakufurahishwa na kitendo chake cha kutoa siri za PFLP kwa polisi wa Lebanon, Moukharbal alivunja ukimya na kuwapa taarifa za Nourredine.
Kitabu ‘Middle Eastern Terrorism: From Black September to September 11’ cha Mark Ensalaco kinasema “Moukharbal alitumia wiki yake ya mwisho ya maisha yake akihojiwa na wapelelezi wa French Direction de la Surveillance du Territoire, DST.
Juni 27 DST ilimtishia maisha yake kuwa hata kiongozi wake (Dk Wadi) Haddad ameshajua amevujisha siri na anatafuta kichwa chake.”
Katika mahojiano hayo aliwaambia maofisa hao wa upelelezi kwamba Nourredine alikuwa ni mshirika wake wa karibu na kwamba huyo Nourredine ndiye Carlos.
Maofisa wa DST walimwonyesha hata picha walizompiga akiwa na Carlos. Vitisho vilipokuwa vingi, Moukharbal alikubali kuwapeleka maofisa hao kwa Carlos.
Aliwaambia kuwa Nourredine (akimaanisha Carlos) mara nyingi alitembelea eneo la 9 Rue Toullier jijini Paris, ambako ndiko alikokuwa akiishi mpenzi wake.
Akifanyia kazi habari hizo, Kamishna wa DST wa Paris, Jean Herranz, na maofisa wengine watatu waliondoka haraka kuelekea eneo la 9 Rue Toullier kwa matumaini kwamba watamkuta Carlos.
Walipowasili walimkuta Carlos akiwaburudisha kwa vinywaji wanafunzi watatu kutoka Venezuela. Wanafunzi hao ni Leyma Palomares, Edgar Marino Muller na Luis Urdaneta Urbina.
Wakati polisi wakigonga mlango wa nyumba hiyo, Carlos alikuwa bafuni na mmoja wa wasichana, akimwonyesha bastola ambayo ilikuwa ni miongoni mwa silaha nyingi alizokuwa nazo kwenye nyumba hiyo, iliyokuwa ya mmoja wa wapenzi wake, Nancy Sanchez.
Walipoingia ndani ya nyumba hiyo walikutana na Carlos, lakini walipoanza kumhoji alikataa na kutishia kuwa atapiga simu ubalozini kulalamika wanamdhalilisha.
Mabishano yakaanza kuwa makali. Kuona hivyo Carlos akawaomba radhi kuwa anakwenda kujisaidia mara moja, akarejea bafuni alikokuwa, akachukua silaha aliyokuwa ameiacha humo na kuichomeka mfuko wa nyuma wa suruali yake.
Wapelelezi wawili ndio walikuwa wametangulia ndani, Moukharbal na mpelelezi mwingine mmoja walibaki nje kwenye gari la polisi kabla hajaungana na wenzake baadaye.
Aliporejea tena ukumbini, Carlos aliwapatia polisi hao vinywaji na kumtaka mmoja wa wasichana aliokuwa nao aimbe wimbo. Maofisa hao walianza kupata vinywaji na hali ikaendelea kuwa ya utulivu hadi alipoingia askari aliyekuwa amebaki nje na Moukharbal.
Moukharbal alipoulizwa kama anamfahamu mtu yeyote kati ya waliokuwa ukumbini, alinyoosha mkono wake kwa Carlos na kusema “huyu ndiye.” Hali ya Carlos ikabadilika ghafla.
Alitoa bastola yake na kumpiga Moukharbal risasi shingoni, kisha akageuzia bastola yake kwa Kamishna Herranz na kumpiga ya shingo, akaangukia meza na kuvunjika meno mawili.
Kwa umakini na kasi, Carlos aliwapiga piaq risasi wapelelezi wengine wawili waliokuwa wamebakia kabla ya kutoroka kupitia nyumba iliyokuwa karibu.
Gazeti la ‘The New York Times’ toleo la Desemba 13, 1997 linasema Carlos alitoroka kwa kuruka dirishani.
Baadaye, Herranz ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya, alisaidiwa na wanafunzi wale na kupelekwa katika Hospitali ya Cochin ya mjini Paris.
Miongoni mwa maofisa wote wa DST walioingia kwa Carlos, ni Herranz peke yake aliyenusurika lakini akawa amejeruhiwa vibaya.
Kabla ya mauaji hayo, Serikali ya Ufaransa haikuwa na ufahamu wowote kuhusu Carlos wala shughuli zake, lakini maelezo ya mashuhuda yaliyotolewa na Herranz yaliwapa habari nyingi kuhusu Carlos na wakaanza kumsaka.
Usiku huohuo baada ya kukimbia eneo la tukio, Carlos alimpigia simu mpenzi wake mwingine raia wa Colombia, Amparo Silva Masmela,28, ambaye hata baadhi ya silaha alizokuwa akizitumia alizihifadhi kwake.
Amparo ambaye hakujua kilichotokea usiku huo, hakutaka kusumbuliwa. Alipopokea simu aa sita usiku, Carlos alimwambia alitaka kwenda kwake kuchukua baadhi ya nyaraka zake. Amparo akamtaka ampigie baadaye, kisha akakata simu kabla Carlos hajajibu. Alipokwama akampigia simu mpenzi wake mwingine wa London, Maria Nydia Romero de Tobon aliyejulikana kama Nydia Tobon.
“Halo, mpenzi wangu, ni mimi,” alisema Carlos, akipiga simu kutoka kwenye kibanda cha simu. “Ilibidi nifanye nilichofanya. Moukharbal alikuwa mwoga, polisi walimchukua na alituuza. Ilinibidi nijitetee kwa risasi. Hakukuwa na njia ya kuepuka ... Ilikuwa ni wao au mimi. Nadhani wangenikamata wangeniua.”
Saa tano baada ya tukio la mauaji hayo, Carlos akaingia nyumbani kwa Amparo, akafungua mlango kwa funguo ambazo aliwahi kupewa na mwanamke huyo. Bila hata salamu, aliwasha taa na kwenda kwenye kabati na kuchukua nyaraka alizotaka ikiwamo pasipoti ya Chile iliyokuwa na picha yake.
Kisha akamweleza Amparo kwamba amemuua rafiki yake, Moukharbal kwa sababu amemsaliti na aliwaua na polisi watatu waliokuja naye wakati huo alikuwa analazimika kukimbilia Brussels, Ubelgiji. Hakuwa amejua kuwa Herranz alinusurika.
Juni 28 mchana, Carlos alipanda treni mjini Paris kuelekea Brussels ambako kutokea huko alipanda ndege kwenda Beirut.
Serikali za Ufaransa na Uingereza, ambako Carlos alikuwa na makazi katika miji ya London na Paris, zilianza kufanya upelelezi wa kina kuhusu yeye.
Wapelelezi walipekua nyumba moja aliyokuwa akiishi Carlos jijini London. Miongoni mwa vitu vingi vilivyokutwa ni kitabu cha mtunzi wa riwaya, Frederick Forsyth kiitwacho ‘The Day of the Jackal.’
Tangu siku hiyo Carlos, ambaye jina lake halisi ni Ilich Ramirez Sanchez, alianza kujulikana kama Carlos the Jackal.
Baadaye Carlos alisafiri kwenda Beirut kuzungumza na Haddad kumweleza kilichomsababisha hadi akamuua Moukharbal.
Haddad alikubaliana naye kwamba Moukharbal alikuwa msaliti alipowapeleka wapelelezi wa Ufaransa kwa Carlos na akuwa wakala wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) tangu 1973 na ndiye aliyetoa habari zilizosababisha kifo cha Mohamed Boudia.
Baada ya kupata Baraka za Haddad, hatua iliyofuata ya Carlos ni ipi? Inaendelea kesho