Bodi NHIF yaagizwa kuharakisha mchakato bima kwa wote

Waziri wa Afya, Jenister Mhagama akizungumza na vyombo vya habari wakati akizundua Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) jijini Dodoma. Picha na Habel Chidawali
Muktasari:
- Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, ilisainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan Desemba mosi, 2023 na kutangazwa kwenye gazeti la Serikali, baada ya Novemba 2, 2023 Bunge kupitisha muswada huo kwa asilimia 100.
Dodoma. Waziri wa Afya, Jenister Mhagama, ameiagiza bodi mpya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kuharakisha mchakato wa kuandaa bima ya afya kwa wote, huku akiipa miezi sita kushughulikia sheria hiyo.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Januari 21, 2025, wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, kusisitiza bodi hiyo isimamie mifumo ya bima na kuacha kuagiza mifumo inunuliwe ndani ili kujiepusha kuingia matatani.
Bodi ya sita ya wakurugenzi ya NHIF itaongozwa na Mwenyekiti Eliud Sanga, pamoja na wajumbe wengine Zubeda Chande, Profesa George Ruhago, Profesa Kaushik Ramaiya, Veronica Kishula, Dickson Kaambwa, Shaaban Kabunga, na Armoury Amoury.
Waziri Mhagama ameipa maagizo matatu bodi hiyo, ikiwemo kuhakikisha wanaanza na suala la sheria mpya ya bima ya afya kwa wote, ambayo inasubiriwa kwa hamu kubwa.
“Mna kazi kubwa kuhakikisha Watanzania wanapata bima ya afya kwa wote haraka. Kila jambo mnalopewa kulifanya, naamini mnaweza kulifanya ndani ya kipindi cha miezi sita tu,” amesema Mhagama.
Maagizo mengine aliyowapa wajumbe hao ni kulinda mafanikio yaliyofikiwa, kuachana na habari za mipango na michakato katika jambo linalokwenda kuwasaidia Watanzania walio wengi, badala yake wafanye kazi kwa weledi lakini kwa haraka.
Kuimarika kwa NHIF
Serikali imesema kwa sasa ina uwezo wa kulipa madai ya madeni ya matibabu ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa kipindi cha miezi 14 bila kukusanya michango kutoka kwa wanachama wake.
Akizungumza, Waziri Mhagama amesema alikosa usingizi kuhusu hali ya NHIF, na hivyo anataka watumishi kufanya kazi kwa haraka badala ya kutembea kama ilivyokuwa mwanzo.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, hadi Januari 2025, Serikali ilishatoa Sh8.9 trilioni ambazo zimewekezwa katika sekta ya afya kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo kusomesha wataalamu.
Awali, Mkurugenzi wa NHIF, Irene Isaka, amesema kwamba mfuko huo katika kipindi cha miezi sita iliyopita walikuwa na nakisi ya Sh47 bilioni, lakini hadi Novemba 2024 walikuwa na akiba ya karibu Sh111 bilioni, huku wakipunguza muda wa kulipa madai.
Mkurugenzi Isaka amesema kwa sasa wanaweza kulipa madeni ndani ya siku 14 hadi 60, kutoka siku 120 za awali, huku wakilenga kuwa na wastani wa siku 45 za kulipa madeni hayo.
Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF, Eliud Sanga, amesema maagizo waliyopewa na Serikali wanakwenda kuyafanyia kazi, lakini akaomba muda kwani ni lazima akakutane na wajumbe wenzake ili waweke mikakati ya utekelezaji.
Hata hivyo, Sanga amesema ili kufikia malengo hayo, wanahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau na taasisi, huku akiomba Watanzania kuondoa mashaka.