Bodaboda zilivyosaidia kupunguza wezi, vibaka mtaani

Muktasari:
- Takriban asilimia 80 ya waendesha pikipiki wamesema wamechagua kazi hiyo kutokana na kuwa na kipato kikubwa ikilinganishwa na kazi walizokuwa wakizifanya awali.
Dar es Salaam. Wakati asilimia 68 na asilimia 78 ya wanaume na wanawake wakishuhudia ongezeko la vipato kupitia kazi ya bodaboda, Katibu Tawala mkoa wa Dar es Salaam, Dk Toba Nguvila amesema sekta hiyo imesaidia kupunguza wezi mitaani.
Hiyo ni kwa sababu watu wengi ambao wangekuwa mtaani bila shughuli ya kufanya sasa wamekuwa wakijitafutia kipato kupitia bodaboda.
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Juni 5, 2025 wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Uchumi katika sekta ya pikipiki za abiria bodaboda uliofanywa jijini hapa chini ya Shirika la Fredrick Ebert Stiftung (FES).
Dk Toba amesema sekta hiyo ina watu wengi ambao walikuwa mtaani na wakati mwingine walipata mawazo ya kwenda kuiba lakini sasa ni bodaboda.
“Lakini sekta hii imesaidia sana kupunguza wimbi la wezi na vibaka mtaani na kitu kizuri ni kuwa wengi wanaelimishwa na kuelewa umuhimu wa hivi vyombo,” amesema.
Alitaka kuwapo kwa utaratibu wa kutoa mafunzo kwa madereva kila wanapokabidhiwa chombo waendeshe kwa uangalifu, kwani wamiliki wa bodaboda na bajaji wangetamani kupata watu wenye weledi na wanaojua kuwa chombo anachoendesha ni kwa ajili ya faida yake na tajiri wake.
Amesema anatambua kuwa familia nyingi sasa zinaendeshwa na biashara ya bajaji na bodaboda hivyo ni vyema kuwaheshimu madereva na wamiliki wa vyombo, ili uchumi wa mtu mmojammoja na Taifa uzidi kuuimarika.
Wakati ripoti hii ikiutaja unyanyapaa kama moja ya changamoto wanayokutana nayo, Dk Toba aliwataka bodaboda kutoumia pale wanapodharaulika barabarani, kwani sasa usafiri huo unaheshimika na umekuwa ukisaidia watu kufika maeneo yao ya kazi kwa haraka.
“Tutaendelea kuwatumia katika maeneo yenye masilahi kwenu na yanayowapa staha na heshima ninyi. Kamwe msitumike vibaya katika kuhujumu Taifa bali katika kujenga uchumi imara, utengamano wa jamii na kuisaidia Serikali kufikia malengo yake,” amesema.
Akielezea kilichomo ndani ya ripoti, Nice Mwasasu ambaye ni miongoni mwa walioshiriki katika kufanya utafiti huo amesema licha ya wanawake na wanaume kukiri kuongezeka kwa kipato chao tangu waanze kazi hiyo, lakini wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo riba zinazoumiza.
Riba hizi ni zile zinazotozwa katika kampuni zinazotoa mikopo ya pikipiki au bajaji sambamba na za kampuni za kuita usafiri kwa njia ya mtandao.
“Kwa mfano utafiti huu umebaini kuwa asilimia 53 ya madereva wanaume na asilimia 65 ya wanawake hawaridhishwi na programu za kuita usafiri mtandaoni, na hiyo ni kutokana na asilimia tofauti za riba wanazopaswa kulipa kwa kila safari,” amesema Nicce.
Katika upande wa kuendesha vyombo kwa mkataba kati ya dereva na mmiliki pia amesema ni moja ya njia ambayo inawaumiza kwani baadhi yao wanapopewa mikataba ya miaka hadi mitatu, inapofikia ukomo, vyombo vyao vinakuwa havina uwezo wa kufanya kazi kama zamani.
“Hivyo tunapendekeza kuwepo kwa udhibiti wa sekta binafsi ili kupunguza riba kwa mikopo na kuhakikisha majukwaa ya kutafuta abiria yanatoa malipo ya haki, ulinzi wa kijamii na matumizi ya data kwa uwajibikaji,” amesema.
Pia alitaka kuwapo kwa mpango jumuishi wa miundombinu kwa kuwashirikisha madereva katika miradi ya barabara, sehemu za kupumzikia na upangaji miji kwa muda mrefu ili kuepuka kuwaondoa kwenye maeneo yao ya kazi.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia na Wanawake na Makundi Maalum, Felissterr Mdemu amesema ni imani yake kuwa matokeo ya tafiti hizo yatasaidia katika kutambua mchango wa kiuchumi wa waendesha bodaboda nchini, changamoto na vikwazo wanavyokutana navyo.
Pia zitasaidia kutambua mahitaji ya waendesha pikipiki hasa wanawake na mikakati ya kuongeza ushirika mpana wa kundi hilo.