Biteko: Maisha ya Askofu Kweka yawe somo

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiaga mwili wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Erasto Kweka.
Muktasari:
- Askofu Kweka ambaye amewahi kuwa mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini toka mwaka 1976 mpaka 2004, alifariki Novemba 25, 2023, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu, anatarajiwa kuzikwa kesho, Desemba 6, 2023, Kijiji cha Uswaa, wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Moshi. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk Doto Biteko ametaka maisha ya Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Erasto Kweka kuwa somo kwa kila mmoja kuishi na kuacha alama baada ya maisha ya duniani.
Dk Biteko ameyasema hayo leo Desemba 5, 2023, wakati akitoa salamu za Serikali kwenye ibada maalumu ya kuaga mwili wa Dk Kweka, katika usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kikutheri Tanzania (KKKT) mkoani Kilimanjaro.
Amesema Dk Kweka amekuwa kielelezo kwa watu wanaojibidiisha na kuwataka viongozi wa Serikali waliopewa kazi, kuifanya kwa bidii kubwa na hivyo kuacha alama.
"Tunatambua mchango wa Dk Kweka katika Kanisa na Taifa, baba yetu Mungu alimpa miaka mingi ya kuishi 89 siyo midogo, tukiangaliana wote huku ndani wengi wetu ni baba yetu na wengine ni wajukuu zake.
"Maisha ya baba huyu, yatupe somo wote tuliobaki kwamba wakati wa kuishi kwetu hapa duniani, pamoja na mambo mengine muhimu kuacha alama kwenye dunia hii na kwa watu tunaoishi nao,”amesema.
Aidha amesema kuishi miaka mingi au michache si kitu isipokuwa ni kitu gani mtu anafanya duniani, ufalme wa Mungu na kwa watu unaokaa nao kwa lengo la kuacha alama.
Dk Biteko ameongeza kuwa Askofu Kweka aliondokewa na baba yake akiwa na miaka 14, akabeba jukumu la kuhudumia na kulea familia yake akiwa na umri mdogo.
“Hakukaa chini akasikitika akasema sina baba mimi ni yatima, alichukua hatua ya kumlea mama, bibi na babu yake katika umri ule akiuza mayai ya kuchemsha kwenye masoko, nia yake ilikuwa ni kuihudumia familia yake.
“Hapo tunajifunza kwamba katika maisha, hata kama unapitia mazingira magumu hakuna kukata tamaa, wito wangu kwetu tunaacha mwandiko gani kwa wenzetu tunaoishi nao?
Baada ya kuagwa kwa mwili huo leo, utapelekwa nyumbani kwake Maili Sita ambapo pia kutafanyika ibada fupi ya kuaga na baadaye kupelekwa kijijini kwao Uswaa wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kidini, kisiasa na kiserikali.
Miongoni mwa hao ni pamoja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi.
Dk Kweka amekuwa kiongozi wa Dayosisi ya Kaskazini toka mwaka 1976 mpaka 2004 alipostaafu, alifariki dunia, Novemba 25,2023, katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu na anatarajiwa kuzikwa kesho, Desemba 6, 2023, Kijiji cha Uswaa, wilayani Hai, Mkoa wa Kilimanjaro.
Kwa mujibu wa historia ya marehemu Kweka, alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu, na kwamba ametibiwa katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Novemba 7, 2023 akiwa nyumbani kwake, hali yake ilibadilika ghafla, akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, ambapo baada ya matibabu, alipewa rufaa ya kwenda JKCI, na Novemba 25 saa 4:00 asubuhi alifariki dunia.