Biteko aongoza waombolezaji kuaga mwili wa Askofu Kweka

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akiaga mwili wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Erasto Kweka.
Muktasari:
- Askofu Kweka ambaye alikuwa mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini kutoka mwaka 1976 mpaka 2004 alipostaafu, alifariki dunia Novemba 25,2023 katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), alikokuwa akipatiwa matibabu, anatarajiwa kuzikwa kesho Desemba 6, 2023 Uswaawilayani Hai, mkoani Kilimanjaro.
Moshi. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko anaongoza mamia ya waombolezaji kuaga mwili wa Askofu mstaafu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk Erasto Kweka (89), katika ibada itakayofanyika usharika wa Moshi mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Viongozi wengine ambao tayari wamewasili kanisani hapo kwa ajili ya kuaga mwili ni Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi pamoja na viongozi wengine wa Serikali, dini na vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa historia, Askofu Kweka alikuwa akisumbuliwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu na ametibiwa katika hospitali mbalimbali za ndani na nje ya nchi na Novemba 7, 2023 akiwa nyumbani kwake hali yake ilibadilika ghafla, akapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambapo baada ya matibabu ya kina alipewa rufaa ya kwenda JKCI, na Novemba 25 saa 4:00 asubuhi alifariki.
Baada ya kuagwa kwa mwili huo, utapelekwa nyumbani kwake Maili Sita ambapo pia kutafanyika ibada fupi ya kuaga na baadaye kupelekwa kijijini kwao Uswaa, wilayani Hai kwa ajili ya maziko ambayo yatafanyika kesho Decemba 6, 2023.