Biteko aipa ujumbe Jumuiya ya Wazazi CCM

Muktasari:
- Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameendelea na ziara Zanzibar ambapo ameitaka Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia rasilimali ilizonazo kujenga na kueneza mafanikio ya chama hicho.
Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ameitaka Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutumia rasilimali ilizonazo kukijenga na kukieneza chama hicho katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuzungumza na wananchi kuhusu kazi kubwa za maendeleo zinazofanyika.
Dk Biteko ambaye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM-Kundi la Wazazi, ameyasema hayo leo Jumapili, Januari 7, 2024 wakati akizungumza na viongozi wa Jumiya ya Wazazi ya CCM Zanzibar katika Ofisi Kuu ya CCM iliyopo, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
“Kama wewe ni mwenyekiti wa mkoa, katibu wa mkoa au kiongozi yoyote yule, kwa kutumia rasilimali ulizonazo tembelea maeneo ya mkoa wako, wilaya na vijiji hata mara moja, zungumza na makundi mbalimbali ikiwemo wajumbe wa kamati za utekelezaji za jumuiya yetu na waeleze kuhusu masuala ya kujenga na kueneza chama," amesema Dk Biteko.
"Hii inawezekana. Tujipange, tufanye ziara hata kama ni kidogo, polepole tutafanya makubwa kadri tutakavyoendelea, tuwe mstari wa mbele kueleza mafanikio ambayo CCM na Serikali yake wameyafanya,” amesema.
Amesema Jumuiya ya Wazazi ni kubwa ndani ya chama, hivyo inapaswa kufanya kazi za kukijenga chama kwa ukubwa huo kwa kuwa inabeba makundi yote ndani ya CCM na haina mipaka wala ukomo wa mtu kuwa sehemu ya Jumuiya.
“Nikitolea mfano, Jumuiya yetu ya wanawake, inahusu wanawake katika chama, Jumuiya ya vijana ina umri fulani ukifika unakuwa hauna vigezo, lakini Jumuiya hii haina mipaka, hivyo inapaswa kuwa na nguvu kubwa.
Tutumie ukubwa wa Jumuiya hii kuwasaidia mwenyekiti wetu na makamu mwenyekiti upande wa Zanzibar katika kujenga chama na kuzungumza kwa ukubwa yale yaliyofanyika na yanayoendelea kufanyika,” amesema Dk Biteko.
Amesema Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wake upande wa Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi wanataka kuona viongozi wa chama katika ngazi mbalimbali wanawasaidia kazi, ikiwemo ya kueleza mafanikio ya kimaendeleo yanayoendelea kufanyika na kazi kubwa inayofanywa na viongozi hao katika kuwaunganisha Watanzania, kuwa na maridhiano na kujenga uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Dogo Mabrouk amemshukuru Dk Biteko kwa kuithamini jumuiya hiyo na kuiwezesha kwa vitendea kazi ambavyo vitaboresha utendaji wake kwenye mikoa sita ya Zanzibar na kuahidi kuwa wataendelea kumpa ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yake.
Kabla ya kikao hicho, Dk Biteko alizuru katika kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume lililopo Kisiwandui Zanzibar.
Pia, Dk Biteko amekabidhi pikipiki sita pamoja kofia ngumu kwa ajili ya Jumuiya ya Wazazi Zanzibar kwenye mikoa ya Zanzibar.
Amesema pikipiki hizo ni mali ya Jumuiya ya Wazazi na ameelekeza zfanye kazi ya siasa kama ilivyokusudiwa.