Biteko ataka Mapinduzi Zanzibar yaenziwe

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko (wa kwanza kulia) akiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume(AAKIA) mjini Unguja leo Jumamosi Januari 6, 2024.
Muktasari:
- Ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuyalinda na kuyaenzi ili kukuza uchumi na uzalendo kwa maendeleo ya Taifa
Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku sita kabla ya Watanzania kusheherekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amewataka wananchi kuendelea kuyaenzi, kuyalinda na kuyaishi kwa dhamira ya dhati.
Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, amesema waasisi wa nchi walifanya mapinduzi hayo ili kuwa na Taifa huru ambalo kila mtu anakuwa na hadhi, kuondoa dhuluma iliyokuwepo na kufanya wananchi kuishi kwa amani na furaha.
Ametoa wito huo leo Jumamosi Januari 6, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mkoani, mkoani Kusini Pemba mara baada ya kuzindua ofisi ya Uhamiaji na makazi ya askari wilayani humo.
“Wananchi tuna wajibu wa kuyaenzi Mapinduzi Zanzibar kwa kuyaishi, kuyaheshimu, kukuza uchumi wa nchi na kukuza uzalendo ili baada ya muda mrefu hata miaka 100 mbele, watakaokuja kusherehekea Mapinduzi haya wakute Zanzibar iliyo bora zaidi na waseme Mapinduzi haya yalitufaa,” amesema Dk Biteko.
Dk Biteko amesema moja ya tunu za Taifa ni mshikamano, hivyo wasiruhusu mtu yeyote kuwagawanya kwa misingi yoyote ile, bali maendeleo yaunganishe wananchi wa vyama vyote bila itikadi za vyama, dini na kabila.
‘’Katika kuelekea kilele cha sherehe za mapinduzi Januari 12, Watanzania wote waungane kuwaombea Rais wa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, ili kuendelea kuongoza vyema, kuimarisha ustawi wa Taifa na kuwaunganisha wananchi,’’ amesema.
Kuhusu Jengo hilo jipya la ofisi ya Uhamiaji, Dk Biteko amesema ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, kwa sababu kabla ya hapo watu walinyimwa haki zao za kimsingi zikiwemo za uhamiaji kwa kukosa hati ya kusafiria.
“Mapinduzi yamewezesha wananchi kupata uhuru wa kusafiri nje ya mipaka ya nchi, ofisi hii ilianza mwaka 1979 ikiwa ni ndogo lakini sasa kuna jengo la kisasa litakalowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa wilaya hiyo na viunga vyake,”amesema Dk Biteko.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini amesema taasisi ya Uhamiaji imeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato akisema kwa mwaka 2022/2023, idara hiyo ililenga kukusanya Sh 56.5 bilioni lakini ilifanikiwa kukusanya Sh 67.679 bilioni.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Islam Seif, amesema ofisi ya uhamiaji ilianza kujengwa Agosti mwaka 2022 na kukamilika Novemba, 2023.
Amesema jengo hilo la kisasa lenye thamani ya zaidi ya Sh1bilioni litakidhi mahitaji ya sasa ikiwemo uwepo wa mifumo ya Tehama ambayo ni muhimu katika utendaji kazi wa taasisi hiyo.
Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala amemshukuru Rais Samia na Rais Mwinyi kwa kuboresha maslahi ya wafanyakazi na pia kuboresha huduma mbalimbali za wananchi.
Dk Makakala amesema idara hiyo inaendelea na ujenzi wa jengo jingine la ofisi katika Mkoa wa Mjini Magharibi, huku akiipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kutoa maeneo ya ujenzi huo.