Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Benki ya Exim kukusanya chupa za damu 1,500

Muktasari:

  • Wafanyakazi na wateja wa Benki ya Exim Tanzania pamoja na wananchi mbalimbali katika mikoa minne nchini wamejitokeza katika matawi ya benki hiyo kwa ajili ya kuchangia damu.

Dar es Salaam. Wafanyakazi na wateja wa Benki ya Exim Tanzania pamoja na wananchi mbalimbali katika mikoa minne nchini wamejitokeza katika matawi ya benki hiyo kwa ajili ya kuchangia damu.

Watu hao wamejitokeza katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Dodoma, hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji damu kuelekea maadhimisho ya siku ya uchangiaji damu ambayo hufanyika kila mwaka Juni 14.

Akizungumza na Waandishi wa Habari  leo Juni 13, 2023 wakati wa uchangiaji damu Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa benk hiyo Stanley Kafu amesema hatua hiyo ni muendelezo  wa juhudi ambazo wamekuwa wakifanya tangu 2010 lengo likiwa ni kukabiliana na upungufu wa damu salama nchini.

“Mara zote tunapoadhimisha siku ya uchangiaji damu Benki ya Exim tumekuwa tukihamasisha uchangiaji damu kwa kuwa tunaamini kwamba tunapata fursa ya kutimiza wajibu wetu kama sehemu ya jamii na hivyo kuokoa maisha ya wenzetu wakiwemo akina mama, watoto na watu wanaopata ajali na kupoteza damu nyingi,” amesema.

Kafu amesema kauli mbiu ya uchangiaji damu ya mwaka huu inayosema: “Changia damu, changia mazao ya damu, changia mara kwa mara,’’ inalenga kuonyesha namna maisha ya watu wenye uhitaji wa damu, huokolewa na wenzao wanaojitokeza kuchangia damu mara kwa mara.

Amesema kufuatia mafanikio makubwa na uungwaji mkono wanaoupata kwenye kampeni hizo, wamewashukuru wananchi wote wakiwasisitiza waendelee kujenga utaratibu wa kuchangia damu mara kwa mara kuokoa maisha ya wananchi.

“Ushirikiano huu baina yetu na wadau wetu unathibitisha uhusiano imara kati ya benki na jamii tunayoihudumia ambao kimsingi unakwenda nje ya mipaka ya biashara hadi kwenye hatma ya maisha yetu.’’ amesema.

Kwa upande wake Ofisa Uhamasishaji na Elimu kwa Umma  Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS)  Marry Meshy amesema uhaba wa damu nchini unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mtazamo wa wananchi kwamba wapo tayari kuchangia damu pale tu inapohitajiwa na mmoja wa wanandugu wa familia husika.

“Natoa wito kwa wananchi na taasisi nyingine kuiga mfano wa benki hii ambayo imekuwa na utamaduni wa kuchangia damu kila mwaka ili kuokoa maisha ya watanzania wote,’’

 Amesema kupitia maadhimisho hayo NBTS Kanda ya Mashariki wanategemea kukusanya chupa za damu 1,500 mafanikio ambayo yamefikiwa kwa asilimia 60 hadi kufikia jana.

“Tunaamini kwamba hadi kukamilisha kwa maadhimisho haya tutakamilisha lengo kwa kuwa muitikio unaridhisha,’’ alibainisha.

Nao baadhi ya wadau walioshiriki katika uchangiaji damu hili zikiwemo taasisi za kijamii wamesema wameguswa na kampeni hiyo ya uchangiaji damu hivyo wamejitokeza kuchangia damu kuokoa maisha ya wananchi wenzao.