Bei, upatikanaji wa gesi bado kikwazo kwa nishati safi
Muktasari:
- Kudhibiti uuzaji holela kwa mawakala wanaouza mitungi ya gesi hasa kupima kilo zinazostahili kuwapo kwa mtungi husika kabla ya kununua.
Dar es Salaam. Gharama kubwa na changamoto ya upatikanaji wa gesi katika maeneo mengi vijijini vimetajwa kuchangia baadhi ya wananchi kuendelea kutumia nishati isiyo salama kupikia, hivyo kuleta ugumu wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi na salama mathalani matumizi ya mitungi ya gesi.
Changamoto hio inafanyiwa kazi ili kuwezesha unafuu wa upatikanaji wa bidhaa hio na bei rafiki hasa maeneo ya vijijini.
Hayo yameelezwa leo Julai 17, 2026 na Mkurugenzi wa Chama cha Waingizaji na wasambazaji wa gesi ya mitungi (LPG) Tanzania (TZLPGA), Amos Mwansumbule katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam ukiwakutanisha waandishi wa habari na wasanii lengo kujadili njia zitakazotumika kuhamasisha matumizi ya mitungi hio kama nishati safi.
Pia, uholela wa uuzaji wa gesi unaofanywa na mawakala mitaani imetajwa kama changamoto nyingine inayowatatiza wananchi kwa sababu changamoto hiyo husababisha kuwapo matukio ya ajali za moto zinazotokana na kulipuka kwa mitungi ya gesi.
Mathalani inayotumika kama nishati safi ya kupikia katika sehemu mbalimbali hasa majumbani, hali hio imekuwa ikiwatia hofu watumiaji wa bidhaa hio.
“Kumekuwapo mawakala wengi mitaani wanaouza mitungi ya gesi kiholela bila kufuata sheria ya uuzaji wa bidhaa hio ikiwamo mizani ya kupima kilo halisi ya kiwango cha gesi unachonunua hatua inayoleta malalamiko kwa watumiaji hasa pale inapoisha haraka, burner za majiko sio salama hivyo kuhatarisha maisha ya mtumiaji wa bidhaa hio.” Amesema Amos.
Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Waingizaji na Wasambazaji wa Gesi ya Mitungi Tanzania, Amos Jackson akizungumza Jijini Dar es Salaam leo Julai 17, 2026 katika mkutano na wasanii wa maigizo na waandishi wa habari wenye lengo la kufikisha ujumbe kwa jamii. Picha na Michael Matemanga
Akibainisha changamoto ya watu kufanya wizi wa gesi kwa kuuza bei ya mtungi isiyolingana na kiwango halisi cha gesi iliyopo anasema kuna baadhi ya mawakala wanauza gesi ikiwa pungufu hii ni kutokana na baadhi kuanzisha biashara bubu ya kuhamisha gesi katika mitungi halisi kutoka katika bidhaa za kampuni husika na kuuza ikiwa haijakamilika kwa bei ileile ya bidhaa iliyokamilika.
Hivyo anaonya tabia hiyo kwa kuwataka wananchi kuwa waangalifu wakati wananunua mitungi ya gesi hasa kupima mtungi kwenye mizani ili kupata kilo zilizokamili na pia kuwafichua wote wanaohusika na njama hizo kwani zinahatarisha maisha ya watumiaji.
Pia, ameeleza kutokana na biashara ya mitungi ya gesi ya kupikia kuongezeka chama hicho kimekuwa kikishirikiana na taasisi za kiserikali wanachama wa chama hicho wakijitahidi kuboresha huduma hizo ili lengo la mpango wa Serikali kila Mtanzania atumie nishati safi ya kupikia ili kulinda afya, mazingira na kuboresha maisha, na asilimia 80 ya Watanzania watumie Nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Naye Mratibu wa kitaifa Women in LPG, Winner Joram amewaasa hasa wanawake kuwekeza nguvu katika kuhamasiha matumizi ya nishati safi kwa lengo la kuokoa afya na hivyo kuyaweka mazingira katika hali safi, akisema matumizi ya kuni na mkaa ni nishati isiyo salama.
Msanii wa filamu, Abdallah Said maarufu Muhogo Mchungu amebainisha madhara ya nishati isiyo salama hasa kwa maeneo ya vijijini imekuwa ikiwaathiri macho watumiaji hasa wanaotumia kuni moshi huyafanya kuwa na rangi nyekundu hali inayofanya wanajamii kuwahusisha wazee na imani za kishirikina na wakati mwingine kuuawa, bila kujua chanzo ni matumizi ya nishati hiyo.
Hivyo, ametoa wito kwa wananchi kuhamia katika matumizi ya nishati safi hasa mitungi ya gesi kupikia ili kuilinda jamii.