Baraza la Sekta ya Afya EAC kukutana kujadili mlipuko wa Ebola
Picha na Mtandao
Muktasari:
- Kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC na Uganda, Baraza la Sekta ya Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) linatarajia kufanya mkutano maalumu wa kielektroniki kujadili hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.
Arusha. Baraza la Sekta ya Afya la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) linatarajia kufanya mkutano maalumu wa kielektroniki (virtual meeting) kwa siku mbili kuanzia leo Juni 1 na 2, 2026 kujadili mlipuko unaoendelea wa ugonjwa wa Ebola unaoathiri ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkutano huo utazingatia hatua za kikanda zilizopendekezwa kudhibiti mlipuko huo unaosababishwa na virusi vya aina ya Bundibugyo (Bundibugyo virus strain).
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na EAC, kuitishwa kwa mkutano huo wa ngazi ya juu ni sehemu ya mfululizo wa hatua za dharura ambazo Sekretarieti ya EAC imeanzisha kuratibu maandalizi ya kikanda kufuatia mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.
Hatua hizo ni pamoja na mkutano wa dharura wa EAC kuhusu janga hilo, mikutano ya Kikosi Kazi cha Kiufundi cha EAC (TWG) kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza, pamoja na mijadala kuhusu uwiano wa kanuni za chanjo zinazoweza kutumika dhidi ya Ebola, matibabu na vifaa vya uchunguzi.
Kikao hicho maalumu cha mawaziri kinatarajiwa kutoa mwongozo wa kimkakati na kuratibu mwitikio wa kikanda katika nchi wanachama. Mlipuko wa sasa ulitangazwa rasmi Mei 15, 2026 na unasababishwa na virusi vya aina ya Bundibugyo, ambavyo ni adimu na kwa sasa havina chanjo iliyoidhinishwa wala matibabu maalumu.
Hadi Mei 26, 2026, DRC ilikuwa imeripoti wagonjwa 121 waliothibitishwa, vikiwamo vifo 17. Aidha, kulikuwa na watu 1,077 wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huo na vifo 246 miongoni mwa wanaohisiwa.
Nchini Uganda, hadi Mei 25, 2026, kulikuwa na wagonjwa saba waliothibitishwa na kifo kimoja. Wagonjwa wawili wa kwanza walikuwa wamesafiri kutoka DRC na kutafuta matibabu nchini humo.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa mlipuko huo umeathiri zaidi DRC, hususan mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, huku Mkoa wa Ituri ukiendelea kuwa kitovu cha maambukizi, hasa eneo la Mongbwalu. Eneo hilo linajulikana kwa mwingiliano mkubwa wa watu na shughuli nyingi za kuvuka mipaka, hali inayoongeza hofu ya kuenea kwa ugonjwa huo katika ukanda mzima.
Katibu Mkuu wa EAC, Balozi Stephen Mbundi, amesema jumuiya hiyo inachukua hatua za haraka na zilizoratibiwa ili kuimarisha utayari wa kikanda na kusaidia nchi wanachama kukabiliana na mlipuko huo.
"Tunahamasisha mifumo ya kikanda na kufanya kazi kwa karibu na nchi wanachama, Afrika CDC, WHO (Shirika la Afya Duniani) na washirika wa maendeleo ili kuimarisha ufuatiliaji, uchunguzi wa maabara, uzuiaji na udhibiti wa maambukizi, mawasiliano ya hatari na uwezo wa kutoa majibu ya haraka," amesema Balozi Mbundi.
"EAC inahakikisha kwamba kila mlipuko unakuta jamii iliyojiandaa. Lengo letu ni kuziunga mkono nchi wanachama kuzuia maambukizi ya mipakani huku tukilinda afya, ustawi wa jamii na utulivu wa kiuchumi wa Waafrika Mashariki," ameongeza.
Sekretarieti ya EAC, kwa kushirikiana na wizara za afya za nchi wanachama, taasisi za kikanda, Afrika CDC, WHO na washirika mbalimbali, ikiwamo Serikali ya Ujerumani na Umoja wa Ulaya, inaendelea kutekeleza hatua za dharura kusaidia utayari na mwitikio wa Ebola katika ukanda mzima.
Miongoni mwa hatua hizo ni uanzishaji wa mtandao wa maabara zinazotembea za EAC. Mradi huo unatekelezwa na Sekretarieti ya EAC kwa ufadhili wa Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) na msaada wa kiufundi kutoka Taasisi ya Bernhard Nocht ya Tiba ya Kitropiki (BNITM).
“Sekretarieti ya EAC kwa kushirikiana na nchi wanachama inaratibu usambazaji wa maabara tisa zinazotembea katika maeneo ya kimkakati ya mipakani na sehemu za kuingilia ili kusaidia upimaji wa haraka na ufuatiliaji wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Maeneo yaliyopangwa kunufaika na maabara hizo ni pamoja na Beni katika Mkoa wa Kivu Kaskazini nchini DRC, mpaka wa Busia nchini Kenya, mpaka wa Nimule-Elegu nchini Sudan Kusini, mpaka wa Kobero nchini Burundi, mikoa ya Kagera na Kigoma nchini Tanzania, wilaya za afya za Kisenyi na Kihundwe nchini Rwanda, pamoja na Hospitali ya Bwera katika Wilaya ya Kasese nchini Uganda.
Wakati huohuo, EAC inaendelea na mazungumzo kuhusu utaratibu wa kikanda wa kuharakisha upitishaji na usajili wa chanjo za Ebola, matibabu na vifaa vya uchunguzi. Wakuu wa Mamlaka za Kitaifa za Udhibiti wa Dawa wamekutana Arusha kujadili uanzishwaji wa mfumo wa kwanza wa pamoja wa kikanda wa EAC wa kuidhinisha chanjo, kwa uratibu wa Wakala wa Dawa wa Afrika (AMA), WHO na mamlaka za afya za kitaifa.
Sekretarieti ya EAC imezitaka nchi wanachama kuimarisha ufuatiliaji katika maeneo ya kuingilia, kuimarisha uratibu wa mipakani, kuwezesha mipango ya kujiandaa kwa dharura na kuongeza uelewa wa umma pamoja na ushirikishwaji wa jamii katika kukabiliana na ugonjwa huo.