Bandari bubu 250 zinakomba asilimia 45 ya biashara TPA

Muktasari:
- Wakati serikali chini ya Rais John Magufuli ikitekeleza mradi wa upanuzi wa bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi na mapato, uwepo wa bandari bubu 250 katika maeneo mbalimbali nchini unatajwa kuwa kikwazo katika biashara hiyo kwa kuwa zinaminya nusu ya mapato yanayopatikana bandari ya Dar es Salaam.
- Juhudi zinafanyika kukabiliana na hilo ikiwamo kuzirasmisha ili ziingize fedha serikalini.
Kuna zaidi ya bandari bubu 250 nchini ambazo zinaweza kuingiza mapato nusu ya yanayopatikana katika bandari ya Dar es Salaam, anasema Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Deusdedit Kakoko.
Bandari ya Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa shughuli za kibiashara ikifanya hivyo kwa kati ya asilimia 90 hadi 95 ikilinganishwa na bandari zote nchini, huku bandari bubu 250 zilizopo zikikadiriwa kuwa na asilimia 45 hadi 47 ya biashara ya bandari nchini.
Kakoko anasema kwa kuwa bandari hizo hazitoi mapato serikalini wanaangalia jinsi ya kuzirasimisha na kusimamia usalama wake jambo ambalo ni nyeti kwa bandari.
Anasema mameneja wa bandari rasmi nchini wamepewa kazi ya kuzisaka bandari bubu na kuangalia zile zinazofaa kurasimishwa na zipi zifungwe ili mapato yaanze kuingia serikalini.
Meneja wa Bandari ya Tanga, Percival Salama akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea bandari hiyo anasema wamebaini kuna bandari bubu 40 kwenye mkoa huo ambapo Wilaya ya Nkinga ziko 12, Tanga Mjini, 22, Muheza moja na Pangani 15.
Anasema nne kati ya bandari hizo bubu wanaweza kuzirasimisha ili kupeleka huduma karibu na wananchi.
“Tunachotaka ni mizigo yote ipite kwenye bandari rasmi ambazo kwa sasa Tanga zipo mbili tu, hii ya mjini na ile ya Pangani,” anasema.
Akizungumzia wanachofanya kwenye maeneo hayo yenye bandari bubu, Salama anasema wanawaelimisha viongozi wa maeneo hayo na kuwaeleza jinsi tozo zilivyo ndogo katika bandari rasmi ili waepuke kuingia kwenye matatizo dhidi ya mkono wa sheria.
“Kutokana na jitihada hizo tumefanikiwa kupata faida katika makusanyo yanayopatikana kwenye majahazi kutoka Sh25 milioni hadi Sh63 milioni kwa mwezi,” anasema.
Anasema wataendelea na mkakati wa kuzifuatilia bandari bubu ili kuhakikisha zinaingiza mapato serikalini.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Tanga, Nelson Mlali anasema wamefuatilia bandari hizo Mtwara na Lindi na kugundua zipo 70.
“Tunashirikiana kuona ni jinsi gani tutazirasimisha au kuzifuta. Tunawapa elimu wananchi kuanzia ngazi ya mkoa hadi mtaa ili tuweze kukubaliana kwa pamoja,” anasema.
Mlali anasema bandari hizo zinaweza kuhatarisha usalama wa nchi kwa kuwa zinaingiza bidhaa ambazo hazikaguliwi wala kudhibitiwa huku zikipunguza shehena katika bandari rasmi.
Anasema kati ya hizo 70 bandari 40 ziko wilaya ya Kilwa.
Akizungumzia uamuzi wa TPA kuzisaka bandari hizo, Kakoko anasema huenda zikawa zinapitisha mizigo hatari kama silaha jambo ambalo si salama kwa nchi huku zikiminya mapato stahiki kwa Serikali jambo ambalo haliwezi kuachwa liendelee.
“Tunaangalia jinsi ya kuzirasimisha bandari hizo kwa utaratibu na kuhakikisha kuna usalama wa kutosha. Jambo hili ni muhimu na nyeti kwa nchi,” anasema Kakoko.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Itungi iliyopo Kyela, Abeid Gallus anasema katika eneo lake linalohusisha mikoa ya Mbeya na Ruvuma, kuna bandari bubu sita zote zikiwa mkoani Ruvuma.
Anasema shida ya bandari hizo ni kwamba zinapunguza mapato ya TPA. “Bandari bubu ni sawa na kuwa na mpaka usio na geti ambao unaweza kupitisha hata silaha.”
Anasema wanatumia njia ya kuwaelimisha wananchi katika maeneo hayo ili waweze kuelewa umuhimu wa bidhaa kupitishwa kwenye bandari rasmi kwa kuwa tozo ziko sawa na hakuna iliyo juu zaidi ya nyingine.
Katika Bandari ya Dar es Salaam, meneja wake Fred Liundi, anasema wilaya ya Kigamboni inaongoza kwa kuwa na bandari bubu, kati ya 35 zilizopo Dar es Salaam 24 zipo wilayani humo ikifuatiwa na Temeke yenye bandari bubu saba na nne za Kinondoni.
Anasema katika mwambao wa mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kuna bandari bubu 71 ambazo zimeshatambuliwa.
“Mamlaka ya usimamizi wa bandari ipo kwenye mchakato wa kuzifanyia tathmini bandari hizi ili kuona zipi zinaweza kurasimishwa na nyingine zifungwe,” anasisitiza.
Anatoa wito kwa wasafirishaji wa mizigo kuacha tabia ya kutumia bandari bubu kwani ni kinyume cha sheria, kosa la uhujumu uchumi na hatari kwa afya na usalama wa wananchi.
“Wanaotumia bandari bubu waachena badala yake watumie bandari rasmi ambazo zimeanishwa kwa mujibu wa sheria,” anasema.