Bajaji, pikipiki vinara kutumia nishati ya umeme

Muktasari:
- Tanzania inaendelea kupiga hatua katika matumizi ya nishati safi hasa kupitia magari na bajaji zinazotumia gesi na sasa mwelekeo kuelekea usafiri wa umeme pia unazidi kuimarika.
Dar es Salaam. Ripoti ya mwaka 2023 kutoka Africa E-Mobility Alliance (AfEMA) imebainisha ongezeko la idadi ya kampuni na wajasiriamali wanaoingia katika soko la magari ya umeme nchini Tanzania.
Ripoti hiyo ilionyesha pikipiki na vyombo vya usafiri vya magurudumu matatu (bajaji) vinavyoongoza kwa kuunganishwa na mifumo ya umeme.
Tanzania inaendelea kupiga hatua katika matumizi ya nishati safi hasa kupitia magari na bajaji zinazotumia gesi na sasa mwelekeo kuelekea usafiri wa umeme pia unazidi kuimarika.
Hata hivyo, licha ya maendeleo haya, waendeshaji wengi wa bodaboda bado wanatamani kuona teknolojia ya nishati safi inapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu zaidi hasa kutokana na kupanda kwa gharama za mafuta.
Waendesha bodaboda wengi wamependekeza suluhisho hizi za usafiri wa umeme zitolewe kwa mfumo wa malipo kwa awamu ili kupunguza mzigo wa kifedha na kuwezesha upatikanaji mpana zaidi.
Akizungumza katika tukio la majaribio ya kuendesha pikipiki za umeme za Spiro lililofanyika katika ofisi ya kampuni hiyo, Mwenyekiti wa Chama cha Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Mkoa wa Dar es Salaam (CMPD), Michael Massawe amesema mifumo rahisi ya malipo inaweza kuwa suluhisho la kuwafikia waendeshaji wengi zaidi.
“Changamoto kubwa kwa Watanzania ni mtiririko mdogo wa fedha, kama kampuni hizi zitaweza kutoa huduma kwa malipo ya awamu, basi waendeshaji wengi zaidi wa bodaboda wataweza kumudu na kumiliki teknolojia hii ambayo inaweza kuchochea maendeleo ya taifa,” amesema Massawe.
Ameongeza kuingia kwa pikipiki za umeme nchini ni ndoto inayotimia kwa waendesha bodaboda wengi.
“Hili ni jambo ambalo tumekuwa tukilihitaji kwa muda mrefu, tayari tuna bajaji zinazotumia gesi lakini pikipiki za umeme ni kitu kipya kwetu. Teknolojia hii ina faida nyingini rafiki wa mazingira na inapunguza uchafuzi wa hewa,” amesema.
Kwa mujibu wa Massawe kubadilisha betri kwa Sh4,100 kunaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji ukilinganisha na kununua lita moja ya mafuta kwa Sh3,000 ambayo husafirisha umbali wa kilomita 30 hadi 40.
“Hii ina maana kwamba tutakuwa tunaokoa fedha nyingi kwenye gharama za mafuta. Hii itakuwa faraja kubwa ya kifedha si tu kwa waendesha bodaboda, bali pia kwa watumiaji wengine kama walimu na wafanyakazi wa usafirishaji wa mizigo,” ameeleza.
Afisa Mauzo, Anthony Mtatiro alieleza kuwa vituo vya kubadilisha betri vitarahisisha usafiri kwa kuondoa hitaji la kusubiri kuchaji.
“Badala ya kusubiri betri ichajiwe, dereva anaweza kufika kwenye kituo chetu cha kubadilishia betri na kubadilisha kwa nyingine kwa gharama ya Sh4,100, ambayo inamwezesha kusafiri hadi kilomita 130,” amesema.
Aliongeza kuwa mara tu betri inapofikia asilimia 85 ya maisha yake ya matumizi, itaondolewa kwenye mzunguko ili kuepusha matatizo ya utendaji kazi.
Wakati huohuo, Meneja Mauzo wa Spiro Tanzania Mobility Solutions amebainisha faida nyingine kuwa ni kupungua kwa wizi.
“Ili kuboresha matumizi kwa mtumiaji, kila pikipiki ya umeme itakuwa na mfumo wa GPS uliojumuishwa bila gharama ya ziada kwa dereva. Kipengele hiki kitasaidia kuzuia wizi na kuboresha usalama,” amesema.
Kadri Tanzania inavyoendelea kusukuma mbele ajenda yake ya nishati safi, wadau wanasema kuwa ushirikishwaji wa waendeshaji wa bodaboda kupitia mfumo wa fedha unaowezesha na miundombinu mahiri utakuwa muhimu katika kuendesha mabadiliko ya nchi kuelekea usafiri wa umeme.