Baadhi ya wafuasi Chadema wataka polisi waondoke mkutanoni, wenyewe wajibu

Muktasari:
- Mkutano Mkuu wa Chadema unafanyika leo Jumanne, Januari 21, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Askari Polisi wameimarisha ulinzi eneo lote la kuzunguka ukumbi huo.
Dar es Salaam. Wakati ulinzi wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ukiwa umeimarishwa katika mkutano mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baadhi ya wafuasi wa chama hicho wametaka waondoke kwa kile walichoeleza wanaweza kujilinda wenyewe.
Mkutano huo unafanyika leo Jumanne, Januari 21, 2025, katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam, ambapo wanachama hao watawachagua viongozi mbalimbali wa ngazi za juu, akiwemo Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti Bara na Zanzibar.
Mchuano upo katika nafasi ya uenyekiti, ambapo kuna wagombea watatu: Charles Odero, Freeman Mbowe, na Tundu Lissu. Mvutano mkubwa upo kati ya Mbowe, anayetetea nafasi hiyo, dhidi ya Makamu wake Bara, Lissu.
Tayari Polisi wapo eneo hilo wakiwa na magari na silaha za moto huku wakiongozwa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro. Pia, askari polisi wengine wapo na pilipiki wakirandaranda huku na huko.
Mwananchi imeshuhudia uwepo wa magari zaidi ya 10 ya polisi yakiwa yanazunguka maeneo mbalimbali, huku polisi wengine wakiwa wamevaa kiraia. Hatua hiyo imeibua mijadala miongoni mwa wafuasi wa chama hicho, wakitaka polisi waondoke eneo hilo.
Katika chaguzi za mabaraza ya Chadema ya vijana (Bavicha) na Wanawake (Bawacha) zilizofanyika ukumbi wa Ubungo Plaza, jijini humo, kulishuhudiwa vurugu za wafuasi wa timu Lissu na Mbowe, kila mmoja akipambania kambi yake ili ibuke mshindi.
Vurugu kubwa zilitawala hususani katika uchaguzi wa Bawacha nyakati za usiku, na baadhi ya wafuasi walikamatwa na polisi.
Kamanda Muliro akizungumza eneo hilo amesema ulinzi katika eneo hilo sio kwa ajili ya Chadema tu, bali kwa wananchi wote.
"Hili eneo ukiliangalia ni la kibiashara, kuna watu mbalimbali wanafika hapa, wakiwemo mabalozi wa nchi mbalimbali.
"Hivyo tumekuwepo hapa kuhakikisha kuwa kuwepo kwa mkutano huu hakuharibu shughuli nyingine zinazoendelea eneo hili," amesema Muliro.
Akijibu shtuma kwamba mbona siku nyingine hakujawahi kuwa na ulinzi wa aina hiyo, amesema sio kweli, kwani eneo hilo lina historia ya matukio na mara kwa mara wamekuwa wakipiga doria hapo.
Kwa upande wa wafuasi wa chama hicho, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mtwara, Daudi Joseph, amesema kuna haja ya polisi kukaa mbali kwa kuwa chama hicho kinaamini katika nguvu ya umma na kuahidi uchaguzi utakuwa wa haki na utamalizika salama.
Naye Meshack Lenjima, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mpwapwa, amesema ana miaka mitatu akishiriki chaguzi za Chadema kuanzia mwaka 2019, na hajawahi kuona ulinzi mkali wa polisi kama wa mwaka huu, jambo linalowapa maswali.
"Sisi hatuoni haja ya polisi kuwepo hapa kwa kuwa tuna vikosi vyetu vya ulinzi ambavyo tunaamini vita linda amani na uchaguzi utamalizika salama," amesema Lenjima.
Naye Shukuru Isaka, mjumbe wa Kamati Kuu kutoka Mpanda, amesema wao ni chama cha demokrasia na wanafanya uchaguzi wao wa ndani, hivyo wanapoona polisi wametanda kama vile kuna vita, wanashindwa kuelewa shida ni nini.
"Ndio maana tunaweza kusema uchaguzi huu unafanyika kati ya wapinzani na dola, kwa sababu kwa nini polisi waje wengi?" amesema mjumbe huyo.
Viongozi mbalimbali wa dini, asasi za kiraia, vyama rafiki, na mabalozi wameshafika kwenye mkutano huo mkuu, na viongozi wa meza kuu wakiongozwa na Mbowe wameingia ukumbini kuanza mkutano huo.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi.