Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Baa 13 zafungwa Kinondoni kisa kelele, ‘madanguro ya magari’

Muktasari:

  • Wananchi wamelalamikia uwepo wa vitendo vya ngono vinavyodaiwa kufanyika ndani ya magari yanayoegeshwa karibu na baa hizo pamoja na maeneo ya makazi ya watu



Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imezifungia kwa muda, baa 13 kutokana na kukiuka masharti ya Sheria ya Leseni za Biashara ya Vileo ya mwaka 1968.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia mfululizo wa malalamiko kutoka kwa wananchi wanaoathiriwa na kelele za muziki mkubwa unaopigwa katika maeneo hayo.

Mbali na kero ya kelele, wakazi wa maeneo jirani pia wamelalamikia uwepo wa vitendo vya ukiukaji wa maadili, ikiwamo biashara ya ngono inayodaiwa kufanyika ndani ya magari yanayoegeshwa kando ya baa hizo na kwenye maeneo ya makazi ya watu.


Chimbuko la operesheni hiyo

Hata hivyo, hatua hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada ya Gazeti la Mwananchi kuchapisha mfululizo wa ripoti maalumu iliyofichua ongezeko la uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele za matamasha na kumbi za burudani jijini Dar es Salaam na mikoani.

Katika ripoti hiyo, ilielezwa namna maelfu ya wakazi wanavyoteseka kwa ukosefu wa usingizi, msongo wa mawazo wa muda mrefu, kupanda kwa shinikizo la damu, pamoja na hatari kubwa ya kupoteza uwezo wa kusikia.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uamuzi huo leo Jumatano, Juni 24, 2026, Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge amesema wameamua kusimamia sheria kikamilifu ili kulinda haki ya wananchi kuishi katika mazingira salama na yenye utulivu.

Meya Mnyonge amezitaja baa zilizokumbwa na rungu hilo kuwa ni pamoja na Tips iliyoko Mikocheni na Tips iliyoko eneo la Coco Beach, Element na Hotea Bar ya Msasani.

Nyingine amesema ni Polosi (Mikocheni), Babiloni Kona ya Bwawani (Mwananyamala), Kwa Joyce,  Serengeti Bar, Raphael Kajubuli, Baikas Lounge (Makumbusho), Big Joe Velvet (Kijitonyama) na Uncle's iliyokoMasaki.

“Baa hizi zimekuwa zikilalamikiwa kwa muda mrefu kutokana na kupiga muziki kwa sauti ya juu sana na kusumbua majirani. Kutokana na wingi wa wateja, magari na pikipiki zimekuwa zikiegeshwa kiholela hadi mbele ya milango ya makazi ya watu, hali inayokwamisha wakazi wanaporejea majumbani mwao,” amesema Meya Mnyonge.

Amesema biashara hizo zimekuwa zikipiga kelele hadi usiku wa manane na wakati mwingine kukesha hadi asubuhi.

Licha ya maofisa wa mazingira kuwapa ushauri mara kadhaa wa kuweka mifumo ya kudhibiti sauti, Meya Songolo amesema wamiliki hao wameendelea kukaidi maelekezo hayo.

“Wameendelea kufanya ukaidi bila kujali kuwa maeneo hayo yana makazi ya wananchi wa kawaida na hata nyumba za mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini,” amesisitiza Mnyonge.

Amesema halmashauri imekuwa ikiwaita mara kwa mara wamiliki na kufanya nao vikao vya kuwashauri kuboresha mifumo yao ya sauti, lakini baadhi yao wameendelea kupuuza maelekezo hayo.

Amesema Sheria ya Vileo ya Mwaka 1968 bado inatumika na haijafanyiwa marekebisho, hivyo wamiliki wa baa wanapaswa kuzingatia kikamilifu masharti yote ya uendeshaji wa biashara hiyo, ukiwamo muda wa kufungua na kufunga shughuli zao.

Amesema baadhi ya baa hizo zinatumia vibali vya Night Club ambavyo havitolewi na halmashauri.

Hata hivyo, maombi ya vibali hivyo hupitia ngazi za halmashauri na huambatana na masharti maalumu, ikiwamo kuwa na mfumo wa kuzuia sauti kutoka nje na kuhakikisha shughuli zote zinafanyika ndani ya jengo.

Amesema baadhi ya wamiliki hawazingatii masharti hayo.

Mbali na tatizo la kelele, Mnyonge amesema halmashauri imebaini uwepo wa vitendo vya ngono vinavyofanyika ndani ya magari yanayoegeshwa katika maeneo ya baa hizo.

Amesema licha ya jitihada za kutokomeza madanguro, baadhi ya watu wamebadili mbinu kwa kutumia magari yaliyopaki karibu na baa hizo kufanya vitendo hivyo.

Aidha, wakati mwingine magari hayo huegeshwa kiholela na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara na njia za kupita.

Mnyonge amesisitiza kuwa, baa hizo hazitaruhusiwa kufunguliwa tena hadi wamiliki wake watakapowasilisha kwa maandishi uthibitisho wa kutekeleza masharti yote ya biashara.

“Baada ya hapo, timu ya halmashauri itafanya ukaguzi ili kujiridhisha kabla ya kutoa ruhusa ya kuendelea na shughuli zao,” amesema.

Amesema operesheni ya kufunga baa zinazokiuka sheria iliyoanza Juni 22, 2026, inaendelea katika Manispaa ya Kinondoni, baada ya kubainika kuwa baadhi ya maeneo hayo yanachangia kurejea kwa vitendo vya ukahaba kupitia matumizi ya magari.


Mwananchi yashuhudia

Jana usiku, waandishi wa Mwananchi walitembelea maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kinondoni na kushuhudia baa pamoja na kumbi kadhaa maarufu za burudani zikiwa zimefungwa, huku milango yake ikiwa imezungushiwa utepe mwekundu wa kuzuia shughuli kuendelea.

Miongoni mwa maeneo yaliyofungwa ni Element, Big Joe na Uncle’s yaliyopo Masaki.

Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa baa hizo waliozungumza na Mwananchi walipinga hatua hiyo wakidai walifungiwa ghafla bila kupewa notisi ya awali, wakisema linaathiri biashara zao pamoja na wateja waliokuwa tayari wamelipia huduma mbalimbali.

Akijibu malalamiko hayo, Mnyonge amesema kabla ya kufunga baa hizo, halmashauri iliwaita wamiliki wake na kuwapatia barua kadhaa za onyo kuhusu ukiukwaji wa masharti ya biashara.

“Baadhi ya wamiliki wa baa tulizozifungia niliwahi kuzungumza nao ana kwa ana, mfano Tips. Haya si malalamiko mapya; wamekuwa wakilalamikiwa katika ngazi mbalimbali. Wapo wengine ambao bado tutawafikia,” amesema.

Amesema hatua ya kwanza waliyochukua ilikuwa kuwashauri na kuwapa muda wa kurekebisha kasoro zilizobainika, lakini baadhi walishindwa kuchukua hatua stahiki.

“Bahati mbaya, wamiliki wengi wa baa hizi hawaishi katika maeneo hayo, hivyo hawafahamu changamoto zinazowakabili wananchi. Mara nyingi utakuta nyumba za makazi zilikuwepo kwanza ndipo baa zikafuata baadaye,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi mmoja wa wamiliki wa baa zilizofungwa ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema tayari ameanza mazungumzo na uongozi wa Manispaa ya Kinondoni ili kutafuta suluhu ya suala hilo.

“Tulifungiwa bila kupewa notisi yoyote. Siku ya kwanza walifika kwa ajili ya ukaguzi wa mazingira, lakini siku iliyofuata walirejea na kuweka utepe wa kufunga eneo bila kutupatia taarifa rasmi,” amesema.

Kwa kawaida, maeneo hayo hufahamika kwa shughuli za burudani na huvutia idadi kubwa ya watu, hasa nyakati za usiku. Wateja wengi huwasili kwa magari binafsi na bodaboda, jambo linalosababisha msongamano mkubwa.

Hata hivyo, baada ya kufungwa kwa maeneo hayo, mazingira yameonekana kuwa tulivu tofauti na ilivyozoeleka. Makundi machache ya watu yalionekana nje ya baadhi ya maeneo hayo yakibadilishana mawazo, huku ndani kukiwa na wahudumu wachache waliobaki.

Nje ya baadhi ya baa hizo, walinzi wa jadi wa Kimasai waliendelea kuwepo kwa ajili ya kuimarisha usalama na kufuatilia magari yanayoegeshwa karibu na maeneo hayo.

Akizungumzia kufungwa kwa baa yake, mmiliki wa Big Joe, Joseph Obengo amesema hakuwa na taarifa rasmi kuhusu hatua hiyo kwa kuwa alikuwa safarini wakati tukio hilo likitokea.

“Sijajua kama baa imefungwa kwa sababu nipo safarini, lakini meneja wangu atakuwa anajua,” amesema Obengo.