Prime
Kisa kelele baa na kumbi maarufu za starehe Masaki zafungiwa
Muktasari:
- Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa baa hizo wamelalamikia hatua hiyo wakidai kuwa walifungiwa ghafla bila kupewa notisi ya awali, jambo ambalo linaathiri biashara zao pamoja na wateja ambao mara nyingi hulipia meza (bucket) mapema.
Dar es Salaam. Baa na kumbi kadhaa maarufu za burudani zilizopo Masaki, Wilaya ya Kinondoni zimefungiwa shughuli zake kwa madai ya kukiuka kanuni na masharti ya sheria ya leseni za vileo, ikiwemo kupiga muziki kwa sauti kubwa na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa maeneo yanayozizunguka.
Miongoni mwa baa zilizokutana na kifungo hicho ni Element, Big Joe na Uncle's.
Zimefungwa huku milango yake ikiwekewa utepe mwekundu unaozuia shughuli za kawaida kuendelea.
Hata hivyo, baadhi ya wamiliki wa baa hizo wamelalamikia hatua hiyo wakidai walifungiwa ghafla bila kupewa notisi ya awali, jambo ambalo linaathiri biashara zao pamoja na wateja ambao mara nyingi hulipia meza (bucket) mapema.
Akizungumza na Mwananchi, Jumanne ya Juni 23, 2026 mmoja wa wamiliki wa baa hizo ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa kile alichodai tayari ameanza mazungumzo na uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ili kutafuta suluhu ya suala hilo ameeleza kutoridhishwa na namna walivyoshughulikiwa.
“Tulifungiwa bila kupewa notisi yoyote. Siku ya kwanza walifika wakiwa na gari la Serikali pamoja na bajaji kwa ajili ya kukagua mazingira. Hata hivyo, siku iliyofuata, ambayo ilikuwa jana (Jumatatu) saa tisa alasiri, walirejea na kuweka utepe wa kufunga eneo bila kutupatia notisi,” amesema mmiliki huyo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Kinondoni, hususan Masaki, umebaini baadhi ya baa maarufu, zikiwemo Element, Big Joe na Uncle's, zimefungwa huku milango yake ikiwekewa utepe mwekundu unaozuia shughuli za kawaida kuendelea.
Maeneo hayo yamekuwa yakifahamika kwa shughuli za burudani, ikiwemo uuzaji wa vinywaji laini na vileo, pamoja na kuvutia idadi kubwa ya watu, hasa nyakati za usiku.
Kwa kawaida, maeneo hayo hushuhudia msongamano wa wateja wanaowasili na kuondoka kwa wingi, huku magari binafsi na bodaboda zikitumika kama njia kuu za usafiri.
Hata hivyo, hali imebadilika baada ya kufungwa kwa maeneo hayo mazingira yameonekana kuwa tulivu tofauti na ilivyozoeleka, huku makundi machache ya watu yakionekana nje wakibadilishana mawazo, ndani ya baadhi ya maeneo hayo, wahudumu wachache walionekana kuwepo wakiwa wamekaa.
Nje ya baadhi ya baa hizo, walinzi wa jadi wa Kimasai waliendelea kuwepo kwa ajili ya kuimarisha usalama na kufuatilia magari yanayofika na kuegeshwa karibu na maeneo wanayoyalinda.
Akizungumza na Mwananchi, mmiliki wa Big Joe, Joseph Obengo, alipoulizwa kuhusu sababu ya baa yake kuwekewa utepe wa kufungwa, amesema hana taarifa rasmi kuhusu hatua hiyo kwa kuwa alikuwa safarini wakati tukio hilo linatokea.
“Sijajua kama baa imefungwa kwa sababu nipo safarini, lakini meneja wangu atakuwa anajua,” amesema Obengo.
Hata hivyo, alipoombwa kutoa mawasiliano ya meneja huyo, Obengo alikata simu na hakupatikana tena kwa maelezo zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa baadhi ya walinzi wa baa hizo, maeneo hayo yalifungwa kwa nyakati tofauti kuanzia juzi na jana, huku sababu rasmi za hatua hiyo zikisubiriwa kutolewa na mamlaka husika.
Mwananchi, ilizungumza na Ofisa Biashara na Uwekezaji Manispaa ya Kinondoni, Philipo Mwakibete kuhusu kufungiwa kwa baa hizo katika maelezo yake alidai huo ni mpango wa kiofisi na anayezumzia kwa ufasaha suala hilo ni bosi wake ambaye ni Mkurugenzi wa Kinondoni.
"Ni kweli operesheni hiyo imefanyika lakini atafutwe Mkurugenzi mwenye mamlaka ya kuzungumzia jambo hilo," amesema Mwakibete
Jitihada za kumtafuta Mkurugenzi wa Manispaa ya Kindoni zinaendelea.
Endelea kufuatilia Mwananchi