Prime
Mbinu kudhibiti kelele za matamasha -3
Muktasari:
- Wadau wanasema kudhibiti kelele za matamasha si suala la kuzuia burudani, bali ni kutafuta uwiano kati ya haki ya kufurahia muziki na haki ya wananchi kupata usingizi, afya njema na maisha bora
Dar es Salaam. Ukuaji wa kasi wa sekta ya burudani, hususani matamasha ya muziki katika manispaa za Ilala, Kinondoni, Ubungo na Temeke jijini Dar es Salaam, umeibua mjadala kuhusu athari za kelele zilizopitiliza kwa afya ya umma na ustawi wa jamii.
Wadau wa sekta hiyo wanasema ongezeko la matamasha limechochewa na kukua kwa kasi kwa tasnia ya muziki nchini na kuongezeka kwa mahitaji ya maonyesho ya muziki wa moja kwa moja.
Hata hivyo, mwenendo huo pia umeibua malalamiko kutoka kwa wananchi wakieleza mifumo ya sauti yenye nguvu huendelea kupigwa hadi usiku wa manane na wakati mwingine hadi alfajiri, licha ya kuwapo kwa kanuni zinazoweka mipaka ya muda wa burudani.
Kwa mujibu wa kanuni za Serikali za mitaa na miongozo ya kudumisha utulivu wa umma, matukio ya burudani yanapaswa kuheshimu utulivu wa jamii, hasa nyakati za usiku.
Kwa mfano, shughuli za kijamii kama harusi kwa kawaida humaliza muziki karibu saa sita usiku, utaratibu unaofuatwa na waandaaji wengi ili kuepusha usumbufu kwa jamii zinazozunguka, kwa kuzingatia masharti hayo.
Hata hivyo, wakosoaji wanahoji kwa nini nidhamu hiyo haitumiki kwa kiwango sawa katika matamasha makubwa ya muziki.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Viwango vya Kudhibiti Uchafuzi wa Kelele na Mitetemo) za mwaka 2015, kiwango cha kelele katika maeneo ya makazi hakipaswi kuzidi desibeli 60 mchana na desibeli 40 usiku.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, mtu binafsi au taasisi yoyote itakayozalisha kelele zinazozidi kiwango kinachoruhusiwa bila kibali inaweza kutozwa faini ya kati ya Sh2 milioni na Sh10 milioni au kuhukumiwa kifungo jela.
Maofisa wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) waliozungumza na gazeti dada la The Citizen wanasema muda wa kumalizika kwa matamasha ya muziki haujawekewa saa moja ya kitaifa, kwani utoaji wa vibali hutegemea aina ya tukio na hadhira inayokusudiwa.
Basata inaeleza kuwa matamasha yanayowalenga watoto yanapaswa kumalizika mapema jioni ili kulinda ustawi wa wao.
"Iwapo tukio linawahusisha watoto, haliwezi kuendelea hadi usiku wa manane," anaeleza ofisa mmoja wa Basata na kuongeza:
"Lakini kama tukio limekusudiwa kwa watu wazima, linaweza kuruhusiwa kuendelea kwa muda mrefu zaidi kulingana na masharti ya kibali na maelekezo ya Serikali yaliyopo."
Mamlaka za Serikali za mitaa nazo zinasema udhibiti wa muda wa matukio pia huongozwa na sheria ndogo zinazowekwa na kila halmashauri ya manispaa.
Ofisa Mkuu wa Utamaduni wa Mkoa wa Shinyanga, Janeth Elias, akizungumza na The Citizen anasema kila halmashauri huweka taratibu zake za kudhibiti shughuli za burudani ndani ya eneo lake.
"Sheria hizi ndogo huziruhusu halmashauri kudhibiti matukio kulingana na hali halisi ya jamii zao," anasema.
Anasema shughuli za burudani zinazofanyika maeneo ya wazi bila mifumo ya kuzuia sauti kutoka nje kwa kawaida hutakiwa kusitisha muziki mkubwa ifikapo saa sita usiku.
"Baada ya saa sita usiku, mwandaaji anatakiwa ama kupunguza kwa kiasi kikubwa kiwango cha sauti au kuzima muziki kabisa ili kuepusha usumbufu kwa wakazi wa maeneo ya jirani," anasema.
Anaeleza mara nyingi maofisa hutumwa kufuatilia matukio makubwa ili kuhakikisha waandaaji wanazingatia masharti ya vibali.
"Katika matukio mengi, tunatuma maofisa kufuatilia shughuli hizo moja kwa moja ili kubaini changamoto zinazoweza kuathiri jamii zinazozunguka na kuhakikisha waandaaji wanazingatia masharti waliyokubaliana nayo," anasema.
Baadhi ya wakazi wanakiri kuwa matamasha yanachangia ukuaji wa uchumi na kutoa ajira kwa vijana, lakini wanasisitiza kuwa athari zake kwa afya haziwezi kupuuzwa.
Wengine wanasema mara nyingi hukosa usingizi, hali inayosababisha uchovu kazini, kupungua kwa ufanisi na kuongezeka kwa msongo wa mawazo.
Nini kifanyike
Mtaalamu wa sheria, Abeid Abeid anasema changamoto hiyo inaweza kutatuliwa kwa kuimarisha mfumo wa utoaji wa vibali kwa waandaaji wa matamasha, kwa kufuata mfumo unaotumika katika sekta nyingine.
"Kama viwanda na waendelezaji wa miundombinu wanavyotakiwa kupata kibali cha mazingira kabla ya kuanza shughuli zao, utaratibu huo unapaswa pia kutumika kwa matamasha ya muziki," anasema.
Anasema taasisi kama Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) zinapaswa kuhakikisha waandaaji wanapata vibali vya mazingira pale vinapohitajika na kuzingatia kanuni za kelele.
"Waandaaji wanapoomba vibali kutoka kwa mamlaka za Serikali za mitaa au taasisi husika, kunapaswa kuwapo mifumo madhubuti ya ufuatiliaji ili kuhakikisha wanazingatia masharti, ikiwamo hatua za utekelezaji wa sheria zitakazopunguza changamoto zinazotokana na kelele," anasema.
Abeid anasisitiza kuwa, taasisi za udhibiti zinapaswa kuhakikisha uzingatiaji wa sheria unaendelea hata baada ya vibali kutolewa.
"Wakati mwingine ni muhimu kuweka mfano kwa kutangaza hadharani na kuwaadhibu wanaokiuka sheria, kama inavyofanyika katika sekta nyingine ili kuhamasisha uzingatiaji wa sheria," anasema.
Anaeleza haiwezekani kuondoa kabisa kelele katika matamasha ya muziki, lakini zinaweza kudhibitiwa kwa ufanisi ikiwa sheria zitatekelezwa kwa umakini.
"Tamasha lazima liwe na sauti, hilo haliwezi kuepukika. Hata hivyo, kama mwandaaji hana kibali cha mazingira, hafuati kanuni za kiwango cha sauti au hana kibali kutoka mamlaka ya sanaa, basi hapaswi kuruhusiwa kuandaa tamasha," anasema.
Daktari bingwa wa masikio, pua na koo (ENT), Dk Salum Seif anasema vituo vya afya mara kwa mara hupokea wagonjwa ambao matatizo yao yanahusishwa na kuathiriwa kwa muda mrefu na kelele kubwa.
Anasema tatizo si matamasha yenyewe, bali namna yanavyosimamiwa, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya kuzuia sauti kutoka nje pamoja na uwekaji sahihi wa vifaa vya sauti ili kuzuia kelele kuenea katika jamii zinazozunguka.
"Tatizo kubwa ni kiwango kikubwa cha sauti, uwekaji usio sahihi wa spika na kuendelea kuathiriwa kwa muda mrefu," anasema na kuongeza:
"Sauti inapozidi kiwango salama, madhara yake yanaweza kujitokeza mara moja au taratibu kadiri muda unavyopita."
Dk Seif anasema kuathiriwa kwa muda mrefu na kelele kubwa kunaweza kusababisha upotevu wa uwezo wa kusikia, maumivu ya kichwa, shinikizo la damu na matatizo ya usingizi, hasa kwa wakazi wanaoishi karibu na maeneo ya matukio.
"Kukosa usingizi mara kwa mara kuna madhara makubwa kwa afya ya akili na mwili," anaonya.
Mwanasaikolojia, Yisambi Mbuwi anasema kelele za matamasha huwaathiri watu kwa namna tofauti kulingana na hali zao za kisaikolojia na kijamii.
"Baadhi ya watu hupata furaha na msisimko kutokana na muziki mkubwa, wakati kwa wengine kelele hizo huwa chanzo cha msongo wa kisaikolojia," anasema.
Anabainisha kuwa tofauti hizo si rahisi kubadilika kwa kuwa zinatokana na mitazamo ya kijamii na tabia za watu.
"Iwapo kelele zinaathiri afya yako ya akili, wakati mwingine ni muhimu kuchukua hatua binafsi kama kuepuka mazingira hayo au kuchagua muda na maeneo mengine ya kupumzika," anasema.
Mkurugenzi wa Workspace Entertainment Company, Christopher Emmanuel, anasema waandaaji wanapaswa kuwashirikisha wataalamu wenye sifa, hasa katika uwekaji na usimamizi wa mifumo ya sauti.
"Waandaaji wengi hawawashirikishi wahandisi wenye taaluma ya sauti, wakati mwingine kutokana na bajeti ndogo au kutokuelewa umuhimu wa usimamizi wa kitaalamu wa sauti," anasema.
"Unaweza kuhudhuria tukio ambalo ndani ya eneo la tamasha muziki ni mkubwa sana, lakini ukitoka umbali wa mita chache nje sauti haisikiki vizuri. Hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa," anasema.
Anasema uwekezaji katika vifaa sahihi na utaalamu ni muhimu, huku taasisi za Serikali zikiweza kuwasaidia waandaaji kupitia mafunzo, miongozo na programu za kuongeza uelewa wa kiufundi.
"Basata inapaswa kuwa na nafasi kubwa zaidi ya kuwapa waandaaji maarifa ya kutosha kuhusu namna ya kuzuia uchafuzi wa kelele na kutafuta njia za kuwawezesha kupata vifaa vinavyofaa," anasema.
Ingawa wasanii hulenga kuburudisha, pia wanapaswa kuhakikisha maonyesho yao hayahatarishi jamii zinazowazunguka.
Msanii wa muziki wa hip hop, Mussa Mabumo maarufu kama Bando Mc, anasema elimu bado ni pengo kubwa katika uandaaji wa matamasha.
"Bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu katika eneo hili. Msanii anapokuwa jukwaani, jambo linalopewa kipaumbele mara nyingi ni namna sauti yake inavyosikika kwa hadhira," anasema.
Hata hivyo, anasema uzito huo unapaswa pia kuelekezwa kwenye athari za sauti kwa watu waliopo nje ya eneo la tamasha.
"Kama wasanii, tunapaswa pia kuwahamasisha waandaaji kudhibiti kiwango cha sauti na kuheshimu ustawi wa jamii," anasema.
Jumanne Ramadhani, ambaye ni DJ kitaaluma anasema wadau wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na mafundi wa sauti ili kutatua tatizo hilo.
"Wakati wa majaribio ya sauti, tunapaswa kutathmini namna sauti inavyosafiri nje ya eneo la tamasha na kutafuta njia za kupunguza athari zake. Elimu ndiyo kila kitu. Wengi wetu hatuelewi kikamilifu mifumo ya sauti. Ushirikiano na kujifunza kwa pamoja kunaweza kuleta mabadiliko makubwa," anasema.
Kwa upande wake, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limesema kudhibiti kelele zinazotokana na matamasha ya muziki kunahitaji juhudi za pamoja kutoka kwa taasisi mbalimbali, waandaaji na wananchi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria wa NEMC, Hamadi Taimuru, Mwongozo wa Kudhibiti Kelele wa mwaka 2021 umegawa majukumu kwa taasisi mbalimbali, zikiwamo NEMC, serikali za mitaa, Jeshi la Polisi Tanzania, Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha) na Basata.
"Tunachofanya NEMC ni kampeni za uhamasishaji, ambazo ni sehemu muhimu ya wajibu wetu. NEMC haijakaa kimya, lakini taasisi nyingine na wananchi pia wanapaswa kuunga mkono juhudi za utekelezaji wa sheria," anasema.
Anasisitiza kuwa, ingawa faini ni moja ya njia za utekelezaji wa sheria, elimu kwa umma ndiyo suluhisho bora la muda mrefu.
"Tunaweza kutoa faini bila kikomo, lakini elimu ndiyo kila kitu. Waandaaji, wasanii na jamii wakielewa hatari za kelele zilizopitiliza, tatizo litapungua kwa kiwango kikubwa," anasema.
Kutokana na hali hiyo, wadau wanasema kudhibiti kelele za matamasha si suala la kuzuia burudani, bali ni kutafuta uwiano kati ya haki ya kufurahia muziki na haki ya wananchi kupata usingizi, afya njema na maisha bora.