Auawa kwa kushindwa kumalizia mahari ya mke

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro, Alex Mkama
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawashikilia watu 120 kwa tuhuma za kufanya mauaji na madawa ya kulevya kwa kipindi cha mwezi mmoja wa Agosti ya mwaka huu.
Morogoro. Watu wawili wamepoteza maisha katika matukio mawili tofauti kwa kushambuliwa katika miili yao huku Jeshi la Polisi likiwashikilia watu zaidi ya watuhuma 120 kwa tuhuma za mauaji ikiwemo la kumuua Hassan Ngema (51) anayedaiwa kushindwa kulipa mahari mkoani Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba Mosi mjini hapa, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema zaidi ya watuhumiwa 120 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya mauaji na madawa ya kulevya.
Kamanda Mkama ametaja tukio la mauaji kuwa watuhumiwa, Masele Machibya (65), Mwalu Hassan (18), Pawa Kema (16) na Rehema Masele (35) kwa pamoja wanadaiwa kula njama na kumuua Hassan Ngema (51) anayedaiwa kushindwa kulipa mahari ya mke.
“Katika kipindi cha mwezi mmoja wa Agosti ya mwaka huu jeshi limeendelea na majukumu yake ya kulinda maisha ya watu na mali zao, kubaini, kuzuia, kutanzua uhalifu na kukamata watu zaidi ya 120 ambao tumewatiwa nguvuni kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo za mauaji na kukutwa na madawa ya kulevya na lengo la operesheni hizi ni kuufanya mkoa wa Morogoro uwe na amani na utulivu,”amesema Kamanda Mkama.
Kamanda Mkama amesema katika matukio hayo wakazi wawili wa Kijiji cha Seregeta, Kata ya Kidugalo, Gasper Kosiana (15) na Hussein Kosiana (15) wanadaiwa kumshambulia kwa kumpiga na virungu na fimbo sehemu mbalimbali za mwili wa marehemu, Habibu Dakawa (26) mkazi wa Ngerengere aliyekuwa akijaribu kuzia mifugo iliyokuwa ikichungwa isiingie katika shamba la korosho.
“Tukio hili lilitokea Agosti 28 mwaka huu saa 11:30 jioni kwa watuhumiwa, Gasper Kosiana na Hussein Kosiana kumshambulia, Habibu Dakawa (26) wakati akizuia mifugo iliyokuwa ikichungwa isiingie shamba la korosho na kumsababishia kifo,”amesema Kamanda Mkama.
Kamanda Mkama amesema Jeshi la Polisi litatumia kila aina ya mbinu za kuzuia, kutanzua na kuwasaka wahalifu wote pale wanapofanya matukio ya kihalifu na kupitia mikono mirefu ya jeshi la polisi pia limewadhibiti watuhumiwa 102 wakiwa na kiasi cha kilo 508.6 za madawa ya kulevya aina ya bangi.
“Hatuishii tu katika kukamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani bali tunafuatilia mwenendo wa kesi zao na hukumu ambapo kesi 88 zimepata mafanikio kwa watuhumiwa kupewa adhabu mbalimbali za kutumikia magereza baada ya kupatikana na hatia za kesi zilizokuwa zinawakabili,” amesema Kamanda Mkama.