Askofu afariki akihubiri misa ya mazishi Tanga

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto
Muktasari:
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto amefariki dunia muda mfupi baada ya kutoa mahubiri katika ibada ya mazishi ya mke wa Askofu mwenzake, Hilda Lugendo iliyofanyika jana, Muheza mkoani Tanga.
Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa, George Chiteto amefariki dunia muda mfupi baada ya kutoa mahubiri katika ibada ya mazishi ya mke wa Askofu mwenzake, Hilda Lugendo iliyofanyika, Muheza mkoani Tanga.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa aliyeongoza misa hiyo katika Kanisa la Kristo Mfalme Muheza, amesema wamepewa taarifa kutoka hospitali kuwa Askofu Chiteto alipatwa na mshtuko wa moyo.
“Madaktari wametuarifu kuna kitu kinaitwa cardiac arrest. Alikuwa na shida ya pressure (shinikizo la moyo) na kisukari,” amesema.
Akizungumzia utaratibu wa mazishi, Askofu Mndolwa amesema Jumatatu watauaga mwili wake tayari kwenda Mpwapa mkoani Dodoma.
“Sasa Mpwapwa tutazika lini, tutajua kesho,” amesema.
Askofu Mndolwa amesema mahubiri ya Askofu Chiteto yaliwavuta watu, hivyo kifo chake kimeshtua.
“Yeye alikuwa mhubiri na kwa kweli mahubiri yake yaliwavuta watu na neno lake la mwisho ni mlango umeandaliwa twendeni, basi anakwenda kukaa na Mungu akamwita,” amesema.

Marehemu Askofu Chiteto aliwekwa wakfu kuwa askofu wa tatu wa Dayosisi ya Mpwapwa Agosti 28, 2022 na amefariki akiwa ameitumikia nafasi hiyo kwaa siku tano tu.
Akifafanua jinsi kifo cha askofu huyo kilivyotokea, msemaji wa kanisa hilo, Maiko Luoga amesema, Askofu Chiteto alihubiri katika misa hiyo na kumaliza, kisha alipokaa aliishiwa nguvu na kukimbizwa katika hospitali teule ya Muheza.
“Misa ile alitakiwa kuhubiri Baba Ndeza wa Kibondo, lakini kwa bahati njema au mbaya, alichelewa kufika, hivyo hekima ya maaskofu ilimtuma Baba Askofu George Chiteto kuhubiri katika misa hii kwa maana ya upya wake katika huduma ya kiaskofu, kwa hiyo alichaguliwa aliye mdogo kati ya wengi aweze kuhubiri,” amesema.
Amesema katika mahubiri yake, Askofu Chiteto alihubiri kwamba ‘Uwe upya katika kumtumikia Mungu, watu wote wamwamini Mungu’.
“Amesema kifo cha Hilda kimefundisha wengi kwa sababu alifariki ghafla akiwa amelala, naye Askofu Chiteto alisema pengine angetamani kifo chake kiwe cha namna ile kwa sababu ni kifo rahisi na hakina mateso kwa mtu yoyote, kwamba aone mwanga umefunguka, njia imefunguka.
“Wakati watu wanayatafakari, akiwa amekaa, ghafla akaishiwa nguvu, akapoteza fahamu na akaanguka chini,” alisema Luoga.
Amesema baada ya hapo walitafuta gari na kumkimbiza hospitali tteule ya Muheza ambako ndiko alikofariki.