Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Anne Makinda akumbuka maisha ya Msuya, mkewe 

Muktasari:

  • Mwili wa  Msuya (94) umeagwa kitaifa leo katika Uwanja wa Karimjee, Dar es Salaam katika hafla iliyoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kesho utasafirishwa kwenda  Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ndege tayari kwa maziko keshokutwa Jumanne kijijini kwake Usangi.

Dar es Salaam. Nguvu ya baba nafikiri ilitokana na nguvu ya Mama! Ni kauli ya aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda akiyaelezea maisha ya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa kwanza Rais, Cleopa Msuya.

Makinda ambaye amebainisha kuwahi kuishi jirani na kiongozi huyo na familia yake eneo la Seaview ameyaelezea maisha ya Msuya na mkewe akisisitiza yalikuwa ya kumvutia kila aliyefika nyumbani kwao.

Msuya alifariki dunia Jumatano, Mei 7, 2025 saa 3 asubuhi katika Hospitali ya Mzena, Kijitonyama jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya moyo, mwili wake umeagwa leo kitaifa, utazikwa keshokutwa Mei 13,2025 kijijini kwao Usangi Mwanga mkoani Kilimanjaro.

Akimuelezea Msuya, Makinda amesema maisha yake na mkewe marehemu Rhoda Mshana enzi za uhai wao yalikuwa ya kipekee.
"Ukifika nyumbani kwao utawa- admire (wakubali) mkewe alikuwa msafi sana, niliishi nao jirani pale Seaview.

"Kingine ambacho waheshimiwa wanapaswa kujua, mkewe ilikuwa kama kuna wagonjwa wamelazwa Muhimbili wametoka Mwanga, basi alikuwa anakwenda kuwajulia hali asubuhi na jioni, alipofariki (miaka 20 iliyopita) mzee Msuya aliona nani mwingine atakuwa kama mkewe?.

Amesema katika maisha yao ya ujirani, hakuwahi kuona mfanyakazi nyumbani kwa Msuya zaidi ya mkewe Rhoda.

"Alikuwa smart, strong na mwenye mapenzi kwa familia, maisha ya Msuya yanatupa funzo kwa namna pia alivyowalea watoto wake.

"Sijui ni kwa vile alikuwa baba maendeleo! Maama alikuwa afisa maendeleo mkuu wale wa mwanzoni kabisa, akiwa yeye na Anna Abdallah hivyo yale aliyokuwa akifanya kwenda kwa watu, kudili na watu moja kwa moja imechangia," amesema.

Amesema nguvu ya Msuya hata baada ya kifo cha mkewe ilichangizwa pia na maisha yake ya nyuma namna alivyoishi katika familia yake.

"Nafikiri nguvu ya baba ilitokana na nguvu ya mama, kama nilivyosema ilikuwa ukienda nyumbani kwao utayapenda maisha yao," amesema Spika mstaafu Makinda.

Mbali na Makinda, Balozi Ombeni Sefue amemuelezea Msuya kama  mtu aliyekuwa na ufahamu mkubwa wa mambo enzi za uhai wake.

"Alifahamu mambo mengi ya uchumi, ya kisiasa na ya kimataifa, mzee Msuya pia alipenda sana na alipenda kuwa current (kwenda na wakati) na kinachotokea," amesema.

Amesema Msuya alikuwa tayari kushauri pale ulipohitajika ushauri wake na alikuwa mkweli kwenye kile alichokiona.

"Tumesikia namna familia ilivyomzungumzia, Mzee Msuya alikuwa ni mzalendo na aliitumikia nchi na alitambua uzito wa wadhifa aliopewa, hii ni sifa ambayo alitaka kupitisha kwa watoto wake pia, kama walivyosema aliwaambia wasijione tofauti na wengine," amesema Balozi Sefue aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi katika Serikali ya Awamu ya Nne.

Mwandishi nguli, Theophil Makunga amemtaja Msuya ni kati ya viongozi wa juu ambaye alikuwa rafiki wa wanahabari.
Amesema alikuwa akijali wengine na kumuelezea namna alivyofanya naye kazi akiwa mwandishi wa habari Msuya akiwa Waziri Mkuu.

"Tulikuwa kwenye ziara yake Mwanga, bahati mbaya waandishi katika ziara ile tuliondolewa katika orodha ya kupata chakula.
Hakuwa anafahamu, alipomaliza kula ametoka nje ili kuendelea na ziara alituona tumesimama akauliza kulikoni? Tukamueleza hatujala, alirudi na kuhakisha tunakula ndipo akaendelea na ziara,” amesema Makunga.

Amesema hata namna waombolezaji na familia yake ilivyomzungumzia inadhihirisha ni namna gani Msuya alijali watu na alitaka mtu ajijenge na kusimama mwenyewe.

Kiongozi wa ACT -  Wazalendo, Dorothy Semu amegusia maisha ya kiongozi huyo hususani katika elimu ambako alihakikisha watoto wake wanasoma shule za Serikali kama alivyoeleza mmoja wa watoto wake, Joyce Msuya.

"Miaka hiyo tunakuwa, sisi tuliokuwa tukiwaona hawa wazee wetu wakichapa kazi, tunadhihirisha namna ambavyo hawakuwa wakipendelea watoto wao.

"Ili ni funzo kwetu kwamba ukishika hatamu basi uhakikishe unaweka mazingira bora katika mifumo ya elimu ili kusiwe na tofauti kubwa kati ya mtoto wa kiongozi na wengine," amesema.


Saa 4 Karimjee

Mamia ya waombolezaji walijitokeza kuaga mwili wa Msuya, huduma iliyochukua takribani saa 4 kuanzia jeneza lenye mwili kuwasili uwanjani hapo hadi lilipoondolewa saa 8:10mchana.

Jeneza lenye mwili wa Msuya liliwasili Karimjee saa 4:16 asubuhi, ikiwa zimepita dakika nane tangu Rais Samia Suluhu Hassan aliyeongoza waombolezaji kuaga mwili huo kuwasili kwenye uwanja huo saa 4:08 asubuhi.

Likiwa limefunikwa bendera ya taifa, jeneza hilo ambalo lililetwa kwenye gari la wazi la jeshi, lilishushwa na kisha kubebwa na wanajeshi kadhaa wa jeshi la wananchi (JWTZ) kulipeleka eneo maalumu lililoandaliwa huku askari wengine wenye sare wakipiga saluti wakati  mwili huo ulipokuwa ukiingizwa kwenye viwanja vya Karimjee.