Aliyemuua mkewe ahukumiwa kunyongwa hadi kufa
Muktasari:
- Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba imemhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa Elias Cravery baada ya kumkuta na hatia ya kumuua mkewe, Jovitha Elias, licha ya mshtakiwa kudai anaamini mkewe hajafariki,baada ya kujiridhisha kuwa alimuua mkewe kwa kumchoma kisu kisha kukimbilia katika kisiwa kingine.
Arusha. Licha ya kusimama kizimbani na kudai kuwa anaamini mke wake hajafa bali bado yuko nyumbani, Elias Cravery ameshindwa kuishawishi Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Bukoba, iliyomtia hatiani kwa kumuua mkewe, Jovitha Elias na kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Mahakama hiyo, baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, iliridhika kuwa ushahidi wa shahidi aliyeshuhudia tukio hilo pamoja na ushahidi wa mazingira ulithibitisha pasipo kuacha shaka kuwa mshtakiwa ndiye aliyemchoma mkewe kwa kisu hadi kufariki dunia.
Mahakama ilieleza kuwa baada ya tukio hilo, mshtakiwa aliondoka kijijini Rukole na kwenda Kisiwa cha Kerebe ambako alidaiwa kutumia jina la Frenk badala ya jina lake halisi la Elias Cravery, hatua ambayo Mahakama imesema ilionyesha jitihada za kuficha utambulisho wake.
Hukumu hiyo ilitolewa Julai 10, 2026 na Jaji Ferdinand Kiwonde aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na nakala ya hukumu hiyo ikiwekwa kwenye mtandao wa Mahakama ya Tanzania.
Ushahidi wa mashtaka
Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi sita ili kuthibitisha shtaka la mauaji ya Jovitha Elias yaliyotokea Septemba 23, 2024 katika Kijiji cha Rukole, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Miongoni mwa mashahidi hao alikuwa Anitha Emmanuel, ambaye alikuwa shahidi wa pili wa upande wa mashtaka na aliyedai kushuhudia tukio hilo kwa macho.
Anitha alieleza kuwa alimfahamu mshtakiwa kabla ya tukio hilo kwa kuwa waliishi katika kijiji kimoja cha Rukole.
Amesema siku ya tukio alimwona Elias akiwa pamoja na mkewe wakitokea barabarani na kuelekea nyuma ya nyumba yake katika eneo la shamba lililokuwa wazi.
Amedai akiwa umbali wa takribani hatua 10 kutoka eneo hilo, aliwaona wawili hao wakianza kugombana na baadaye alimwona Elias akitoa kisu na kumchoma mkewe.
Ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea asubuhi na eneo hilo lilikuwa wazi kwa kuwa mazao yalikuwa yamevunwa, hali iliyomwezesha kumuona vizuri mtu aliyekuwa akifanya kitendo hicho.
Baada ya tukio hilo, Anitha alidai kuwa alimsogelea marehemu na kumwona mshtakiwa akikimbia kutoka eneo hilo na kuwa alijaribu kumfuata lakini Elias alifanikiwa kutoroka na kutoweka msituni.
Shahidi huyo pia alieleza kuwa baada ya tukio hilo alimweleza mwenyekiti wa kijiji, Jacobo Protase, kuwa Elias ndiye aliyemchoma mkewe kisu na kukimbia.
Mbali na ushahidi huo wa shahidi wa macho, upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi wa mazingira uliotolewa na Advera Deus, mama wa marehemu.
Advera alieleza kuwa kabla ya mauaji hayo, binti yake alimweleza kuwa alikuwa anakwenda kwa mumewe baada ya kuambiwa kuwa amepata shamba jipya na alitaka warudiane.
Amesema alimtaka asiende kwani walikuwa wametengana ila binti yake alisisitiza kwenda, ndipo alipomsindikiza hadi sehemu ya kupandia gari Septemba 23, 2024 kuelekea kwa mumewe.
Baada ya tukio hilo, ushahidi wa upande wa mashtaka ulionyesha kuwa mshtakiwa aliondoka kijiji cha Rukole na kuelekea Kisiwa cha Kerebe.
Mahakamani ilidaiwa kuwa akiwa kisiwani humo, Elias alikutana na mfanyabiashara mmoja aliyefahamika kwa jina la Mnyonge aliyempokea na kuanza kufanya naye biashara ya kukausha dagaa.
Ilielezwa kuwa baada ya Mnyonge kufariki Julai 30, 2024, mshtakiwa aliendelea kuishi kisiwani humo kwa kukodi chumba hadi alipokamatwa Novemba 10, 2024.
Katika kipindi hicho, Tyson Anthony, ambaye alikuwa akiishi na kufanya biashara Kisiwa cha Kerebe, alieleza mahakamani kuwa mshtakiwa alijitambulisha kwake kwa jina la Frenk badala ya jina lake halisi.
Shahidi huyo alisema baadaye wakati wa kukamatwa kwake ilibainika kuwa jina lake halisi lilikuwa Elias Cravery.
Jofrey Raphael, aliyeshiriki katika mchakato wa kukamatwa kwa mshtakiwa, alitoa ushahidi kuwa Elias alimweleza kuwa alibadili jina lake ili kuficha utambulisho wake na kuepuka kukamatwa kutokana na tuhuma za mauaji.
Utetezi wa mshtakiwa
Akitoa utetezi wake, Elias alikana kuhusika na mauaji ya mkewe na kuiambia mahakama kuwa hakutenda kosa hilo.
Amedai kuwa anaamini mkewe hajafa na kwamba bado yuko nyumbani ambako alimwacha katika kijiji cha Rukole.
Mshtakiwa alieleza kuwa hakuwa eneo la tukio siku ambayo mauaji hayo yalidaiwa kufanyika kwa sababu alikuwa tayari ameondoka kijijini hapo na kwenda kuishi Kisiwa cha Kerebe.
Amedai kuwa aliondoka Rukole Agosti 5, 2023 na kuelekea Kisiwa cha Kerebe ambako alipokelewa na mfanyabiashara mmoja aliyefahamika kwa jina la Mnyonge na kuanza kufanya biashara ya dagaa.
Amesema baada ya Mnyonge kufariki Julai 30, 2024, aliendelea kuishi kisiwani humo kwa kukodi chumba hadi alipokamatwa Novemba 10, 2024.
Pia, alipinga madai kuwa alibadili jina lake ili kuficha utambulisho wake, akisema hakuwahi kutumia jina jingine wala kujitambulisha kama Frenk kama ilivyodaiwa na mashahidi wa upande wa mashtaka.
Aidha, alipinga ushahidi wa Anitha akisema madai yake hayakuwa ya kweli na kwamba ushahidi uliotolewa dhidi yake haukuwa na msingi wa kumtia hatiani.
Uamuzi wa Mahakama
Jaji Kiwonde amesema baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na pande zote mbili, suala kuu lililokuwa mbele ya mahakama lilikuwa kubaini kama upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha shtaka la mauaji dhidi ya Elias bila kuacha shaka yoyote.
Kuhusu kama mshtakiwa ndiye aliyesababisha kifo hicho, Jaji amesema ushahidi wa Anitha, ambaye alishuhudia tukio hilo, ulikuwa na uzito mkubwa kwa kuwa alimfahamu mshtakiwa kabla ya tukio na alieleza kwa undani namna alivyomuona akimchoma mkewe kisu.
Jaji amesema ushahidi huo uliungwa mkono na mazingira yaliyokuwepo kabla na baada ya tukio, ikiwemo maelezo ya mama wa marehemu kuwa Jovitha alikwenda kwa mumewe baada ya kuambiwa amepata shamba, pamoja na hatua ya mshtakiwa kutoroka na kwenda Kisiwa cha Kerebe ambako alitumia jina la Frenk.
Kuhusu utetezi wa mshtakiwa kwamba alikuwa Kisiwa cha Kerebe wakati mauaji yakitokea, Jaji alisema haukuweza kuibua mashaka katika kesi ya upande wa mashtaka na kuwa kitendo cha mshtakiwa kutumia jina tofauti baada ya kufika Kisiwa cha Kerebe na baadaye kubainika kuwa jina lake halisi ni Elias Cravery kiliongeza uzito wa ushahidi uliowasilishwa dhidi yake.
Katika suala la nia ya kuua, Jaji amesema matumizi ya kisu na kulenga sehemu nyeti za mwili wa marehemu, ikiwemo shingo, yalionyesha kuwepo kwa nia ovu iliyokusudiwa.
Kutokana na uchambuzi huo, Jaji Kiwonde alihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulithibitisha kesi yake bila kuacha shaka yoyote na hivyo kumkuta Elias Cravery na hatia ya kumuua mkewe, Jovitha.
Mahakama ilimhukumu mshtakiwa kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Kanuni ya Adhabu, kikisomwa pamoja na kifungu cha 341(1) (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai.