Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ajira za TRA ‘zatema’ 74,383 usaili wa awali

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA Aprili 26, 2025, waliochaguliwa kuendelea hatua na inayofuata ni 6,505 ambao sasa watafanya usaili kwa njia ya kuandika.

Dar es Salaam. Jumla ya watu 74,383 kati ya 80,888 waliofanya usaili wa awali kuomba nafasi za kazi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamekosa sifa ya kuendelea hatua inayofuata.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRA Aprili 26, 2025, waliochaguliwa kuendelea hatua na inayofuata ni 6,505 ambao sasa watafanya usaili kwa njia ya kuandika.

Idadi hiyo ya watu watakaofaulu mtihani wa mwisho wa mamlaka hiyo wanakwenda kujaza nafasi 1,596 baada ya Machi 12, 2025 TRA kutangaza watu 135,027 ndio walioomba nafasi hizo.

Nafasi zilizotangazwa ni ya msimamizi msaidizi wa kodi, waombaji walikuwa 5,491 na  waliofaulu mtihani huo wa awali ni 974.

Nafasi nyingine ni ya ofisa forodha daraja la pili, waombaji walikuwa 14,614 na walipita kuendelea na hatua inayofuata ni 862 pekee.

Katika kundi la madereva, waombaji walikuwa 3,480 na waliopenya hatua inayofuata ni 553.

TRA imetangaza hatua inayofuata ya mchakato wa ajira itatangazwa Aprili 29, 2025 kupitia tovuti ya mamlaka hiyo.

Nafasi zingine zinazokwenda kujazwa ni ya ofisa msimamizi ushuru daraja la II idadi ya watu wanaohitajika ni 573, ofisa forodha daraja la II 232, msaidizi wa usimamizi wa ushuru daraja la II, 253, msaidizi wa forodha daraja la II ni 154 na  mhadhiri msaidizi (15).

Wengine ni ofisa usimamizi data daraja la II  nafasi 20, ofisa rasilimali watu daraja la II (11), ofisa utawala daraja la II (3), ofisa usafirishaji daraja la II (5) na ofisa milki daraja la II (15).

Wapo pia, wahandisi daraja la II nafasi 12, wajiolojia daraja la II (2), ofisa hesabu daraja la II (12), mhasibu daraja la II (2), ofisa mambo ya ndani daraja la II (10), ofisa vihatarishi daraja la II (8) na wachumi daraja la II (6).

Nafasi nyingine zilizotangazwa ni watakwimu daraja la II nafasi 4, mwanasheria daraja la II (6), ofisa ununuzi na usambazaji daraja la II (5), ofisa maabara (3), mkutubi daraja la II (4), ofisa taaluma daraja la II (2).

Pia, kuna mkaguzi wa ndani daraja la II nafasi mbili, mlinzi daraja la II (2), ofisa uhusiano daraja la II (5), msaidizi wa mafunzo (2), katibu muhtasi daraja la II (12), mtaalamu wa maabara daraja la II (4), ofisa hesabu msaidizi (10) na  msaidizi wa usimamizi wa rekodi daraja la II (10).

Nyingine ni mafundi uashi na umeme daraja la II nafasi 10, mwendesha mfumo wa ulinzi daraja la II (9), nahodha daraja la II (8), fundi boti (8), mkutubi msaidizi daraja la II (2), nahodha msaidizi daraja la II  (2), mtu wa mapokezi daraja la II (20), dereva daraja la II (105) na msaidizi wa ofisi daraja la II (27).


Wachumi wanena

Akizungumza na Mwananchi kuhusu matokeo hayo ya usaili yaliyotangazwa na TRA, Mtalaamu wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo amesema idadi hiyo ya watu iliyojitokeza wakati haihitajiki, inaonesha wazi bado tatizo la ajira nchini ni kubwa.

“Haiwezekani kuita watu wengi ambao hawahitajiki. Hata aliyebuni utaratibu wa ajira anakumbwa na changamoto, kwa sababu kama unajua unayemhitaji, unaanzaje kufanya usaili kwa watu 80,000? Ilipaswa kuwe na mfumo wa ‘automatic elimination’ unaowaondoa wale wasio na sifa mapema, kwa kuwa tunaishi katika dunia yenye uhaba wa ajira,” amesema.

Ameeleza kuwa, kuna umuhimu wa kubuni mbinu mbadala za kupata watahiniwa badala ya kutoa matangazo kwa watu wote.

Profesa Kinyondo amesema kuwa kwa kufanya hivyo, watu wengi wangesikia kuwa kuna ajira TRA na kuomba bila kujali kama wana vigezo au la, wakiamini kuwa TRA inalipa vizuri.

“Kwa hiyo, mfumo wa ajira ulipaswa kuwa na utaratibu wa kuwawezesha wenye sifa tu kubaki na baadaye kutangazwa rasmi kwa kusema: Samahani, watu wengi wameomba lakini hawa ndio waliokidhi vigezo,” amesisitiza mtaalamu huyo.

Profesa Kinyondo ameongeza kuwa, hatua iliyochukuliwa na TRA imewaumiza watu kwa kuwapotezea muda ambao wangeweza kuutumia kutafuta fursa nyingine.

“Hili lililofanyika ni kuwaumiza watu na kuwapotezea muda. Hata hao 6,000 waliobaki bado watachujwa ili kupata wachache zaidi. Kwa nini kupotezea watu muda na kuwapa matumaini yasiyo na msingi? Badala yake, ingepaswa kusema wazi kuwa hata kama watu milioni moja wameomba, vigezo vinavyotakiwa ni hivi na waliohitimu ni watu 50 pekee, kisha kutoka hapo kuchagua wachache zaidi. Kwangu mimi, hii ni shoo isiyofaa; wanawajengea watu matumaini halafu wanawatupa,” amesema Profesa Kinyondo.

Ameeleza kuwa, kiuchumi idadi kubwa ya waombaji inaonesha changamoto kubwa  ambayo Serikali inahitajika kuunda ajira zaidi kwa ajili ya vijana.

Pia, amesema wingi huo wa waombaji unaonesha kuwa nafasi za ajira haziongezeki sambamba na ongezeko la vijana wasio na ajira.

“Idadi kubwa ya vijana nchini inakabiliana na soko dogo la ajira, hali inayosababisha kuongezeka kwa vitendo kama wizi, ulevi na matumizi ya shisha. Natarajia timu ya waziri mkuu inayoshughulikia ajira itaketi na kutafuta njia bora ya kuwawezesha vijana kujiajiri au kuajirika,” amesema.