Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ajali za bodaboda na ulaji nyama tishio jipya la kifafa

Ajali za bodaboda na ulaji nyama tishio jipya la kifafa

Muktasari:

  • Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kupambana na ugonjwa wa kifafa, taarifa zinaeleza kuwepo kwa ongezeko la vijana wanaumwa ugonjwa huo, chanzo kikubwa kikielezwa ni ajali za pikipiki maarufu kama`bodaboda’.

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya kupambana na ugonjwa wa kifafa, taarifa zinaeleza kuwepo kwa ongezeko la vijana wanaumwa ugonjwa huo, chanzo kikubwa kikielezwa ni ajali za pikipiki maarufu kama`bodaboda’.

Mbali na sababu hiyo, watalaamu wametaja pia minyoo inayotokana na ulaji wa nyama ya nguruwe kama moja ya sababu za ugonjwa wa kifafa.

Kulingana na taarifa za kliniki ya kifafa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa wiki huwatibia wagonjwa 30 na watano kati yao ni vijana ambao wamepata ugonjwa huo kutokana na ajali za bodaboda.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu siku hiyo inayoadhimishwa kila Jumatatu ya pili ya Februari, Daktari bingwa wa ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, Patience Njenje alisema ugonjwa huo unaathiri zaidi vijana wenye umri kuanzia miaka 15.

Daktari huyo alieleza kuwa ajali nyingi za bodaboda zinapotokea na mhusika akaumia kichwani mara nyingi husababisha kifafa.

Alisema tafiti za miaka michache iliyopita zinaonyesha Tanzania ilikuwa na wagonjwa milioni moja ila kulingana na idadi ya watu wanaofuata matibabu MNH upo uwezekano kuna ongezeko kubwa la watu wenye kifafa nchini.

“Vijana wamekuwa waathirika wakubwa kutokana na ajali za bodaboda. Mtu akipata ajali na kuumia kichwani, lile kovu kwenye ubongo ni chanzo kikubwa cha kifafa. Akitibiwa anapona ila ikitokea amepata ajali tena basi inaweza pia kujirudia,” alisema Dk Njenje.

Akizungumzia pia ugonjwa huo, daktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa fahamu, ubongo na uti wa mgongo wa hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Henry Humba alisema asilimia 65 ya wanaopata ajali na kupata majeraha kichwani wapo katika hatari ya kupata kifafa kwa asilimia 90.

“Ajali zinazosababisha jeraha kichwani zipo za aina tofauti, ila zinazochukua sehemu kubwa ni za bodaboda kutokana na shughuli zao na inapotokea ajali mara nyingi athari inakwenda kichwani.

Kifafa hiki kipo cha aina mbili, kuna cha awali ambacho hutokea ndani ya siku saba baada ya ajali na hiki hakina dawa ya kukizuia, tunatibu dalili na kumuweka chini ya uangalizi mgonjwa kwa muda. Pili ni kile kinachotokea baada ya siku saba tangu ajali itokee, hiki matibabu yake yanaweza kuchukua muda mrefu,” alifafanua Dk Humba.


Kifafa na nyama ya nguruwe

Dk Njenje alieleza kuwa wilaya za Haydom mkoani Manyara na Mahenge mkoani Morogoro zinaongoza kwa kuwa na watu wengi wanaougua kifafa, sababu kubwa ikiwa minyoo kutoka kwa nguruwe pamoja na shughuli za kilimo.

“Haydom ina wagonjwa wengi wa kifafa kwa sababu ya watu kule hula nyama ya nguruwe ambao wana minyoo. Mifugo kama nguruwe ikiachwa itembee hovyo inakutana na vitu visivyofaa kama hiyo minyoo.

“Mtu akila nyama ya nguruwe mwenye hiyo minyoo, tena ikiwa haijaiva vizuri, ni rahisi kuingia mwilini mwake na kwenda kushambulia ubongo. Hapo ndipo tatizo la kifafa linapoanzia, tunasisitiza nyama ya nguruwe ipikwe na kuiva kabisa ili kuondoa uwezekano wa minyoo hiyo kuwa hai,” alionya Dk Njenje.

Kwa upande wa wilaya ya Mahenge, Dk Njenje alisema shughuli za kilimo kwenye maeneo yenye majimaji huchangia kuzaliana kwa minyoo hiyo ambayo huingia mwilini kwa mtu kupitia miguu na kupanda hadi kwenye ubongo.

Alisema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watu 1,000 wilayani Mahenge 37 wana ugonjwa huo na tafiti zinaendelea kufanyika kupata namna ya kuwanasua katika tatizo hilo.

Dk Njenje alitaja chanzo kingine cha ugonjwa huo hususani kwa watoto ni kuiwa na homa kali kwa muda mrefu ambayo husababisha degedege na hatimaye kifafa.

Ili kumnusuru mtoto na hali hiyo, daktari huyo alishauri kupata matibabu ya haraka pindi anapopatwa na homa.

Hata hivyo, daktari huyo alieleza kuwa bado kuna changamoto ya watu kukosa uelewa kuhusu ugonjwa huo na kuhusisha na imani za kishirikina, jambo linalosababisha wagonjwa wengi kushindwa kupata matibabu.

“Ni asilimia tano hadi 10 pekee ya wagonjwa wa kifafa nchini ndio wanafika hospitali kupatiwa matibabu, wengi huamini ugonjwa huu unasababishwa na kurogwa, hii ni imani potofu tunapaswa kuondokana nayo.

“Kifafa kinatibika, dawa zipo hakuna sababu ya kumfungia ndani mgonjwa wa kifafa ni muhimu atibiwe ili aweze kuendelea na shughuli zake,” alisema Dk Njenje.

Kulingana na mtaalamu huyo kwa mujibu utafiti wao, asilimia 36 ya Watanzania wanahusisha kifafa na imani za kishirikina huku asilimia 50 wakiamini ugonjwa huo unaambukiza.

Alisema ukweli ni kwamba kifafa hakiambukizwi na inashauriwa kumsaidia mtu mwenye kifafa anapodondoka kwa kumlaza upande na kumuacha kwa muda hadi hali hiyo itakapotulia.

Suleiman Mfaume ambaye ni mgonjwa wa kifafa, alisema, “kwa kweli napitia kipindi kigumu, mkono wangu inaishiwa nguvu kabisa. Tatizo hili lilianza ghafla nilikuwa naanguka na kung’ata ulimi. Nashindwa kuelewa kwanini ugonjwa huu unikute ukubwani, nina miaka mitatu sasa tangu nianze kuugua.”


Kumsaidia mwenye kifafa

Dk Njenje alisema tofauti na wengi wanavyoamini kuwa ukimgusa mtu mwenye kifafa unaweza kuambukizwa, mgonjwa huyo anahitaji kusaidiwa ili asiumie.

Hatua ya kwanza ni kuwahi kumshika wakati anahangaika kutaka kuanguka. Baada ya hapo anatakiwa kulazwa upande na kuachwa kwa muda hadi hali ya kuhangaika itakapotulia.

Muhimu zaidi mtaalamu huyo anasisitiza mgonjwa wa kifafa asiwekewe kitu chochote mdomoni.

“Kuna watu huwa wanawawekea kijiko au kitu chochote kuzuia asikaze meno, hiyo inamuongezea hatari zaidi. Mlaze upande kisha muache. Muhimu kuliko yote hakikisha anapata matibabu na anatumia dawa sambamba na kuhudhuria kliniki,” aliongeza.