Ajali ya basi Njombe yaua saba, yumo mtoto wa miaka minane

Njombe. Jumla ya watu saba akiwemo mtoto wa kike anaekadiriwa kuwa na miaka nane, wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wamepanda kupinduka katika Kijiji cha Igando kilichopo wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe John Imori amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambapo amesema basi la New Force lenye namba za usajili T173DZU lilikuwa linaipita roli na kuingia mtaroni.
Amesema mpaka sasa idadi kamili ya majeruhi katika ajali hiyo haijafahamika na wapo katika taratibu za uokoaji zikiwa zinaendelea.
Amesema ajali hiyo imetokea leo imetokea majira ya saa nane na nusu mchana wakati basi hilo likiwa linatokea Dar es salam kuelekea mkoani Rukwa.
"Kwa taarifa za awali basi la New Force lilikuwa linatoka Dar es salaam kwenda mkoani Rukwa, Sumbawanga lilipofika Igando kuna sehemu ya daraja likawa linataka kuovartake likapoteza uelekeo likaja wa likaingia mtaroni,” amesema Kamanda huyo.
Amesema wanaume waliofariki katika ajali hiyo ni watano akiwemo dereva wa basi hilo huku wakike wakiwa ni wawili pekee.
Amesema idadi ya majeruhi kwenye ajali hiyo ni 48 kati ya hao wanawake ni 21 na wanaume ni 27.
Amesema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi kulipita lori bila ya kuchukua tahadhari hivyo likamshinda na kugonga daraja kisha kupinduka na kusababisha vifo na majeruhi.
"Kwahiyo chanzo ni dereva kutochukua tahadhari wakati analipita gari lingine naye amefariki," amesema Imori.
Amesema mpaka sasa majima ya waliofariki kwenye ajali hiyo hayajafahamika jitihada zinafanyika ili waweze kutambuliwa.