ACT Wazalendo yashauri maeneo nane kibajeti

Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi wa chama cha ACT, Esther Thomas
Muktasari:
- Chama cha ACT Wazalendo kimesema kodi zilizoelekezwa katika vyombo vya usafiri zinakwenda kuongeza makali ya maisha, ikishauri marekebisho na kuanzisha kodi mpya.
Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimesema Bajeti Kuu ya Serikali ya Tanzania 2023/24 haikujibu changamoto za watanzania huku ikishauri maeneo nane ya kuboresha.
Akizungumza leo katika uchambuzi wa bajeti hiyo, Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi wa chama hicho, Esther Thomas amesema chama hicho kinashauri kuangalia upya tozo, kodi zinavyoathiri wananchi wengi.
Kwa mujibu wa ACT, gharama za maisha bado ziko juu, mzigo wa ajira ukiongezeka huku Serikali ikiwa na uwezo wa kutoa ajira 70,000 kati ya milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Katika ufafanuzi wake, Esther amesema kodi zilizoanzishwa kwenye vyombo vya usafiri na tozo ya Sh100 zinaenda kushuka kwa abiria ambao ni wananchi wengi wanaoendelea kukamdamizwa na gharama za maisha.
“Tunashauri pia Serikali ifute kabisa kodi ya mapato ya asilimia mbili kwa wachimbaji wadogo na ipanue wigo wa vyanzo vya mapato,” amesema Esther.
Miongoni mwa vyanzo vipya alivyoshauri ni pamoja na kuanzisha kodi itokanayo na posho za vikao katika sekta ya umma na binafsi.
Pia ACT Wazalendo kimeshauri kuongeza mauzo ya bidhaa nje ya nchi kwa kuongeza thamani ya mazao ikiwamo korosho na kuwekeza nguvu katika miradi ya Mchuchuma.
Aidha kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa LNG na kuongeza vivutio sekta ya utalii.
Kwa upande mwingine chama hico kimeitaka serikali kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo ili kukabiliana na wimbi la ukosefu wa ajira linalozidi kupanda kutokana na uzalishaji mdogo wa ajira nchini.
Esther amesema zaidi ya vijana 1,000,000 huingia kwenye soko la ajira kila mwaka huku wanaopata ajira wakiwa 70,000 pekee.
“Uchumi wetu unazidi kupunguza uwezekano wa kuzalishaji ajira zenye staha na shughuli za kueleweka za kuwapatia vijana vipato ili kumudu maisha yao,” amesema Esther.
Esther amesema ili kujibu changamoto hiyo serikali haina budi kutazama sera za kibajeti kwenye maeneo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi na kuona kama maamuzi ya kibajeti yanapeleka rasilimali kwenye maeneo hayo mfano kilimo, viwanda na utalii.
“Tanzania imekuwa na uchumi unaokua kwa kasi ya wastani wa asilimia 6 kila mwaka lakini uchumi huo hauzalishi ajira. Hii ni kutokana na ukweli kuwa sekta za uchumi zinazokua kwa kasi ni zile ambazo zinaajiri watu wachache sana, Mfano sekta za ujenzi, madini na mawasiliano zinaajiri watu asilimia 3 tu,” amesema Esther.
Ameongeza kuwa Serikali inatakiwa kubuni sera ambazo zitawezesha kuzalishwa kwa ajira nyingi nchini ambapo amesema sekta yenye uwezo wa kuajiri watu wengi ni Kilimo inayojumuisha Uvuvi na Mifugo.
“Uchumi usiozalisha ajira sio uchumi jumuifu na ni hatari kwa usalaama wa Taifa. Bajeti ya Mwaka huu haijaonyesha kabisa mpango wa kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Hata sekta yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi kama sekta ya nguo haijawekewa kivutio chochote,” amaesema.