419 wadanganya kuwa na ulemavu wapate ajira za Tamisemi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki akizungumzia matokeo ya nafasi za ajira zilizotangazwa Aprili 12,2023.
Muktasari:
- Kutokana na Serikali kutangaza nafasi za ajira na kuahidi kuwapa kipaumbele wenye mahitaji maalum, zaidi ya 419 wamejitokeza kudanganya kuwa ni walemavu.
Dodoma. Kati ya waombaji 171,916 walioomba ajira katika kada ya ualimu na afya kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, waombaji 1169 walijitambulisha kuwa walemavu lakini uchunguzi umebaini zaidi ya waombaji 419 hawana ulemavu wowote.
Hayo yameelezwa leo Juni 5,2023 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki wakati akizungumza kuhusu matokeo ya nafasi za ajira zilizotangazwa Aprili 12,2023.
Kairuki amesema kati ya waombaji 64 waliojitambulisha kuwa na ulemavu wa ngozi, ni waombaji 24 tu ndio walisema ukweli huku 40 wakidanganya kwani uchunguzi umebaini hawana ulemavu huo.
Hata hivyo kati ya waombaji waliojitokeza ni waombaji 18449 tu ndio wamechaguliwa na kupangiwa vituo vya kazi baada ya kukidhi vigezo vya kitaaluma na taratibu za uombaji.
Kairuki amesema waliochaguliwa na kupangiwa vituo vya kazi katika kada ya afya ni 5319 na ualimu ni 13,130 na kati yao wenye mahitaji maalum ni 111 sawa na asilimia 0.84.
Hata hivyo katika kada ya afya nafasi 8070 ndio zilizotangazwa lakini zilizopatikana na kukidhi vigezo ni 5319 na kufanya nafasi 2751 kuendelea na mchakato wa kutafuta wengine.
Akizungumzia kuhusu kutokukamilika kwa waombaji wa kada za afya Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi, Dk Ntuli Kapologwe amesema nafasi za ofisa fiziotherapia, radiolojia na maofisa matabibu wasaidizi imebidi zitangazwe tena.
Dk Kapologwe amesema ni kutokana na uzalishaji wa kada hizo kuwa mdogo lakini Serikali tayari imefanya uwekezaji wa ununuzi wa mitambo hivyo lazima mchakato wake uendelee.
“Kwa upande wa kada za maofisa tabibu wasaidizi hiyo ilikuwa kwa ngazi ya astashahada lakini uzalishaji wake umekuwa mdogo na vyuo vingine vimeacha, kwa hiyo kada za aina hiyo ndio zimepelekea kutangaza tena na nyingine kubadilisha kutokana kwamba uzalishaji wake umesimama,” amesema.