270,000 kukosa nafasi sekondari za umma

Muktasari:

  • Siku mbili baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba, imebainika wanafunzi 274,671 waliohitimu na kupata daraja D na E, hawana nafasi ya kujiunga na sekondari za umma katika mwaka wa masomo 2023.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba, imebainika wanafunzi 274,671 waliohitimu na kupata daraja D na E, hawana nafasi ya kujiunga na sekondari za umma katika mwaka wa masomo 2023.

Idadi hiyo ni wastani wa mwanafunzi mmoja kati ya watano waliohitimu. Kwa mujibu wa Necta, watahiniwa walikuwa 1,348,073 na wenye matokeo asilimia 20.4 yaani 265,892 na 8,779 walipata daraja D na E.

“Hawa wanafunzi waliopata daraja D na E hawana vigezo vya kuchaguliwa sekondari za Serikali kwa kuwa utaratibu unataka wawe na ufaulu wa daraja A hadi C,” Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi aliliambia gazeti hili jana. Mwaka 2021 wanafunzi 125,325 walipata daraja D na E.

Hata hivyo, alifafanua zaidi kuwa si jukumu la Necta kupanga hatma ya wanafunzi hao, badala yake inachokifanya ni kuwasilisha matokeo kwa mamlaka nyingine kisha zitaamua.

“Sisi ni kama madaktari tunawapima tunatoa majibu, kuhusu waende wapi ni kazi ya mamlaka nyingine, tunawasilisha matokeo kwa mamlaka nyingine kisha zitaamua kama waende vyuo vya ufundi Stadi (VETA) au wapi,” alifafanua.

Mwananchi lilifanya jitihada la kuwatafuta viongozi wa wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, akiwamo Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahaba aliyesema hafahamu lolote kwa kuwa yupo nje ya ofisi.

“Mimi sijui lolote labda nikiwasiliana na Necta nitakuwa na cha kujibu lakini kwa sasa sina la kusema,” alieleza kwa ufupi.

Naye, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Francis Michael alijibu kwa ujumbe mfupi akitaka waulizwe Necta kwa kuwa ndio wenye mamlaka na hilo.

“Huyo (Katibu Mtendaji Necta) ndiye mhusika mkuu wa mambo ya mtihani, muulize maswali yako yote,” alijibu kwa ujumbe mfupi.


Maoni ya wadau

Kundi hilo la wanafunzi waliopata madaraja hayo lipo hatarini kukosa mwelekeo na hatimaye kuwa watoto wa mtaani, inaelezwa na Dk Oscar Magava, mkuu wa idara ya misingi ya elimu na utawala wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE).

Kwa karne ya sasa, alisema wahitimu wa darasa la saba, ni watoto bado hivyo hawamudu maisha yao binafsi iwapo wataachwa mtaani.

“Kwa kundi hili tunakwenda kuzalisha watoto wa mtaani na panyarodi kwa sababu wameshindwa kufaulu katika elimu na kama wazazi wao hawana uwezo wa kuwapeleka shule binafsi watabaki mtaani,” alieleza.

Kwa mujibu wa Dk Magava, yanahitajika mabadiliko ya haraka katika mfumo wa elimu, utoe nafasi mbadala kwa mwanafunzi akishindwa katika taaluma kuwe na fursa za ufundi shuleni.

“Siamini kwamba hawa waliopata madaraja D na E hawana uwezo kabisa, hawa wana vipaji vingine kungekuwa na utaratibu wa kugundua vipaji vyao shuleni wangefanya vema katika maeneo hayo,” alisema mhadhiri huyo aliyebobea katika sera, mipango, uongozi na utawala kwenye elimu.

Mwalimu wa sekondari ya Dar es Salaam Islamic, Musa Badi aliwataka wazazi wenye wanafunzi ambao wameshindwa kupata daraja A hadi C kama kigezo cha uchaguliwa katika shule za Serikali, kutowakatia tamaa watoto wao kwani wanaweza kuchukuliwa katika baadhi ya shule binafsi wakaendelea na masomo yao na hata kufanya vizuri zaidi katika mitihani inayofuata katika ngazi ya sekondari

“Kuteleza siyo kuanguka, wazazi wasiwakatie tamaa watoto hao bado wanaweza kusoma na wakafanya vizuri hapo mbele,”alisema.


Kutokuwepo kwa mpangilio wa ubora wa ufaulu

Katika matokeo ya mtihani huo mwaka huu, baraza halikutoa orodha ya mpangilio wa ubora wa ufaulu kuanzaia waliofanya vizuri hadi waliofanya vibaya kwa mwanafunzi mmoja mmoja, shule, wilaya, kimkoa na kitaifa kama ilivyo miaka mingine.

Alipoulizwa kuhusu hilo Amasi alijibu utaratibu huo utaendelea hata katika matokeo ya ngazi nyingine za elimu, kwa maana kidato cha pili, cha nne na cha sita.

“Hayo ni mazoea tu kwani unataka kuona nini huko, ukitaka kujua ubora wa shule kwenye matokeo tumezipa wastani kwamba hii ni daraja A kulingana na namna ilivyofaulisha, ukifungua matokeo ya shule utaona tumezipa wastani huo,” alifafanua.

Hata wazazi wanaotaka kuchagua shule za kuwapeleka watoto wao, alisema waangalie wastani wa ufaulu wa shule ndicho kilichofanywa na Necta kuonyesha uwezo.

Ingawa utaratibu huo unaziba mwanya wa kuzinadi baadhi ya shule, kwa upande mwingine unapunguza ushindani katika ufaulu kwa mujibu wa wadau wa elimu.

Mwalimu Gradius Ndyetabula alisema utaratibu huo utapunguza ari ya wanafunzi kushindana kuwania nafasi ya kwanza kitaifa, mikoa au wilaya.

Matokeo yake, alieleza juhudi zitapungua na itachukua muda mrefu hadi wazoee kwamba hawasomi kuwa wa kwanza.

“Hii ina athari hata kwa shule, ile kutambua waliofanya vizuri iliongeza ushindani, uwekezaji na ubunifu katika shule, lakini isipokuwepo kila mtu atafanya kawaida, hii ina athari.

“Lazima tukubali kuwa hatuko sawa, wapo waliotuzidi hii ipo hata katika utafutaji kwenye maisha ya kawaida, kilichofanyika ni sawa kwa sababu tuna mamlaka ya kufanya hivi lakini inapunguza ubunifu na ushindani,” alisema.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule alisema hiyo itakuwa na athari kwa wenye mtazamo wa kushindana, lakini haina madhara yoyote kwa wenye nia ya kufanya vema.

Bila kuwepo orodha hiyo, alieleza kama mkoa umefanya vibaya matokeo ya shule zake yataonyesha idadi kubwa ya wanafunzi waliofeli na hiyo pekee inatosha kuongeza kutafuta mbinu za kukabiliana na hali hiyo.

“Hakuna haja ya kujua umekuwa wa ngapi, ukiona F zimekuwa nyingi katika shule za mkoa wako fanya juhudi kuziondoa, si lengo la Serikali kujua nani amekuwa wa ngapi, dhamira ni kufaulisha wote,” alisema Rosemary.

Hoja hiyo inaungwa mkono na Dk Zainab Taleck, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, aliyesema kikubwa ni kuangalia namna gani kiongozi wa eneo husika amepunguza sifuri katika mkoa wake.

Alisema tathmini ya kupanda au kushuka kwa elimu haifanywi kwa kuangalia mkoa umekuwa nafasi ya ngapi kitaifa, bali inaangaliwa kwa msukumo na mikakati iliyowekwa kupunguza wanaofeli.

“Kama mimi najua kwamba kidato cha sita nina daraja la nne moja tu, naelewa nifanyeje ili kuliondoa sio kuangalia nani amekuwa wa ngapi, tunaangalia wanafunzi wamefaulu vipi,” alisema.