Wahamiaji haramu na mbinu mpya ya kuingia nchini

Watuhumiwa wa uhamiaji haramu 20 raia wa Ethiopia waliokamatwa wakisafirishwa kwenye gari aina ya Land Cruiser lililokuwa likipeperusha bendera ya CCM.

Muktasari:

Mfululizo wa matukio kadhaa ya hivi karibuni yanaonesha magari ya kifahari yenye namba zinazodhaniwa ni za Serikali yanahusika katika kuwasafirisha wahamiaji haramu

Dar es Salaam. Wasafirishaji wa wahamiaji haramu wanaoingia au kupita nchini, wamebuni mbinu mpya ya kuwasafirisha watu hao kwa kutumia magari yenye namba za kughushi za Serikali, kwa lengo la kutokamatwa.

Mfululizo wa matukio kadhaa ya hivi karibuni yanaonesha magari ya kifahari yenye namba zinazodhaniwa ni za Serikali yanahusika katika kuwasafirisha wahamiaji hao haramu, jambo linaloibua maswali kuhusu matumizi ya magari hayo na wahusika wake.

Kwa muda mrefu, wahamiaji hao haramu hasa  kutoka Ethiopia, walikuwa wakisafirishwa kwa usafiri wa malori na hata magari yenye matenki ya mafuta matupu, lakini katika siku za hivi karibuni, hali imegeuka.

Wahamiaji hao wanasafirishwa kwa kutumia magari ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser V8 huku mengine yakiwa yanapeperusha  bendera za vyama vya siasa.


Gari aina ya Land Cruiser V8 lililokuwa likipeperusha bendera ya CCM lililokamatwa eneo la Minjingu wilayani Babati mkoani Manyara likiwa na watuhumiwa wa uhamiaji haramu 20 ambao ni raia wa Ethiopia.

Siyo rahisi kuyatilia shaka magari hayo yanayotumika kuwasafirisha wahamiaji hao kwa sababu mamlaka za usalama hudhani magari hayo yamebeba viongozi wanawahi kwenye kazi zao.

Hata hivyo, baada ya mfululizo wa matukio ya kukamatwa kwa wahamiaji hao haramu wakisafirishwa na magari hayo, wadau wameibuka na kuhoji kulikoni huku wengine wakishauri nini kifanyike kukomesha hali hiyo.

Baadhi wameitaka Serikali kuimarisha ushirikiano baina ya nchi wanakotoka wahamiaji hao haramu na kule wanakokwenda ili kuwadhibiti.


Kutoka kwenye malori hadi V8

April 8, 2024 Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Allan Bukumbi wa Mkoa wa Iringa alitangaza kuwakamata raia wa Ethiopia 16, wanaodaiwa kuingia nchini bila kibali.

Kamishna Bukumbi amesema wahamiaji hao waliwakamatwa wakiwa wametelekezwa katika shamba la mahindi baada ya kushushwa kwenye gari ambalo awali lilikuwa likisomeka namba za usajili wake ni STL 3999 Landcruiser V8 lenye rangi nyeupe

Watuhumiwa wa uhamiaji haramu wakishushwa kwenye lori lililokuwa likiwasafirisha  baada ya kukamatwa na vyombo vya ulinzi na usalama nchini.

Amebainisha kuwa uchunguzi wa awali ulibaini gari hilo limesajiliwa kwa namba T803 CVW na mmiliki wake ni Saidi Hassan, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam na jitihada za kumsaka mhusika alisema zinaendelea.

Pia, siku hiyo hiyo, Aprili 8, mwaka huu, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Lucas Mwakatundu alitangaza kuwashikilia raia wa Ethiopia 17 waliodaiwa kuingia nchini bila kibali wakitaka kuelekea Afrika Kusini kupitia mkoani Dodoma.

Wahamiaji hao walikamatwa  Aprili 7, 2024 Mtaa wa Maisaka, mjini Babati wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 VXR iliyobandikwa namba ya Serikali STL 1964

Tukio lingine ni la Machi 23, 2024, raia wengine wa Ethiopia 20 walikamatwa eneo la Minjingu mjini Babati wakielekea mkoani Mbeya kupitia Dodoma, lengo likiwa kufika Afrika Kusini.

Watuhumiwa hao wa uhamiaji haramu walikuwa wakisafirishwa kwa kutumia gari lenye namba za usajili T 774 BDL aina ya Toyota Land Cruiser likiwa linapeperusha  bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

Februari 14, 2022 Polisi Mkoa wa Kilimanjaro  kwa kushirikiana na Idara ya Uhamiaji, waliwakamata watu 11 wanaodaiwa kuingia nchini bila kibali wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser VX.

Februari 20 2024, Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Tanga, liliwakamata watu 16 katika Kijiji cha Mazinde Kata ya Mazinde wilayani Korogwe wakiwa wamepakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cuiser V8 yenye namba za usajili T888 CEA kwa madai ya kuingia nchini bila kibali.

Matukio hayo yalitokea pia Septemba, mwaka jana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro liliwakamata watu 18 waliokuwa wakisafiri kuelekea Zambia kwa kutumia gari la mizigo, mali ya kampuni ya Fredy Logistics ya jijini Dar es Salaam, kwa madai ya kuingia nchini bila kibali.

Mwaka 2018, takwimu mpya zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji (IOM) miaka 10 iliyopita zilionyesha asilimia 80 ya safari za wahamiaji haramu kimataifa walipita kwenye mipaka halali ikiwamo ya viwanja vya ndege, bandarini na vituo halali vya ukaguzi mipakani.

Biashara hiyo haramu inatajwa kuwa na mtandao mkubwa na wenye kuwaingizia fedha nyingi wahusika, takwimu za IOM zinaonyesha mhamaji haramu mmoja hulipa Dola  za Marekani kati ya 1,600 (Sh3,760,000) hadi Sh3,000 (Sh7,050,000) kusafirishwa kutoka maeneo ya mpaka wa Tanzania kutoka maeneo ya mpaka wa Kenya hadi Tunduma na wengine hulipa hadi Dola 5,000 (Sh11.750 milioni).


Kudhibiti mbinu mpya

Profesa wa Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Khoti Kamanga amesema  wahamiaji haramu wamekuja na mbinu mpya kwa sababu tayari wako hatua moja mbele ya sheria.

“Wanaosimamia sheria wanakuwa nyuma, wahamiaji wanakwenda waibadilisha mbinu, sasa tukiziba mwanya huu watatafuta mwanya mwingine. Kinachohitajika kufanyika ni kuwepo kwa ushirikiano baina ya nchi wanazotoka kwa sababu huko kuna kitu kinawasukuma, chanzo kisipodhibitiwa tutakuwa tunahangaika siku zote,” amesema.

Profesa Kamanga amesema udhibiti huo wa wahamiaji kutoka nchi wanakotoka usiwe wa kuwakataza, bali wa kuweka utaratibu wa kuwawezesha watu wanaotaka kusafiri nje ya nchi.

“Kuwazuia sio suluhu, lakini pia hizo nchi wanazokwenda wahamiaji hao kuwe na udhibiti wa watu, wasiruhusiwe kuingia kiholela na hili litawezekana tu, kama kutakuwa na ushirikiano wa dhati baina ya nchi wanazotoka, wanakopita na wanakokwenda,”amesema Profesa Kamanga.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, Dk Gaspardus Rwebangira amesema  biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu ni miongoni mwa zinazotengeneza faida kubwa duniani.

Amesema biashara ya kuuza silaha, dawa za kulevya na usafirishaji wa binadamu ndio biashara kubwa zinazoingiza fedha kwa haraka na wanaohusika na mtandao huo ni wafanyabiashara wakubwa.

“Wakati mwingine wafanyabiashara hawa wanahusiana na watu wengine hasa viongozi waliopo kwenye maeneo ya usalama na wanasiasa,” amesema.

Dk Rwebangira amesema njia zinazotumika zinabadilika kulingana na hatua ambazo Serikali inachukua akisema mbinu za kutumia magari ya kifahari aina ya Toyota Land Cruiser ni watu kutotilia shaka kinachofanyika.

Amesema mbinu ya kupambana na wahamiaji haramu lazima ishirikishe wadau wengi na wawepo watoa taarifa ndani ya Serikali au taasisi binafsi.


Njia zinazotumika kuwadaka

Msemaji Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji, Mrakibu Paul Msele amesema ukamataji wa wahamiaji hao  ni kutokana na udhibiti ambao umekuwa ukifanywa  na Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na vyombo vya usalaama na taarifa wanazotoa wananchi

Amesema kutokana na udhibiti wa wahamiaji hao, kwa sasa wamebadili uelekeo wa kusafiri na malori na wanatumia magari mengine.

Hata hivyo, amesema kila mbinu itakayobadilishwa na wahamiaji hao, Jeshi la Uhamiaji nalo linabadili mtindo wa kuwanasa.

Lori likiwa limesimamishwa kwenye kizuizi kilichopo Kijiji cha Kamsisi wilayani Mlele, Mkoa wa Katavi kwa ajili ukaguzi wa usafirishaji wa wahamiaji haramu. Picha na Maktaba

 “Raia wa Ethiopia wameondolewa Visa rejea, kwamba wanaweza kuja na pasipoti yao kama wanataka kupita kwenda nchi nyingine anaruhusiwa analipa Dola 30 za Marekani (Sh77,250) kama anataka kuja kuitembelea Tanzania anaruhusiwa atalipa Dola 50 za Marekani (Sh128,750) bila kuwa na kikwazo chochote,” amesema Mselle huku akisisitiza kuwa haoni sababu ya wao kuingia na kupita Tanzania kinyemela.

Hata hivyo, ofisa huyo amewaonya wanaoshiriki kwenye biashara hiyo haramu huku akisema yeyote watakayembaini ajue adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela kinamsubiri.

“Tunatoa elimu kwa wananchi kila siku ili watusaidie kutoa taarifa pale tu wanapowabaini watu walioingia nchini bila kufuata utaratibu na tumekuwa tukishirikiana na vyombo vingine vya usalama katika kuwadhibiti wahamiaji hao wanaojaribu kuingia nchini,” amesema.

Mselle amesema wanafanya doria na wahamiaji wengi wanaokamatwa ni kutokana na vizuizi walivyoweka katika maeneo mengi nchini.

Pia, amesema wameboresha sheria na kuweka adhabu ya kifungo cha miaka 20 kwa mtu anayebaini kuhusika na biashara ya kusafirisha watu kimagendo,

Jambo lingine amesema Serikali imefuta Visa rejea kwa raia wa Ethiopia kwa sababu  walikuwa hawezi kupata Visa wakati wa kuingia.

“Ilikuwa lazima aombe kwanza ndio aje kupata, lakini sasa anaweza kuomba wakati wowote hata kama anapita anaenda nchi nyingine anaweza kuomba na kuendela na safari yake,”amesema ofisa huyo.


Kauli ya Jeshi la Polisi

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema uhalifu wa usafirishaji haramu wa binadamu ni tatizo linaloikumba dunia kila kona na Tanzania ikiwamo.

Akizungumzia mbinu zinazotumika kuwasafirishia wahamiaji hao, Misime amesema zinabadilika kulingana na mazingira.

Hata hivyo, amesema kutokana na kubadilika kwa sayansi na teknolojia inayobadilisha utendaji wa uhalifu unaovuka mipaka hasa wa usafirishaji haramu wa binadamu, nao pia wanabadili mbinu ya kuwanasa kisayansi.

“Tumeshuhudia usafirishaji kwa njia za miguu, kwa njia ya maji, malori ya mizigo yakiwamo matenki ya kubeba mafuta, lakini kutokana na mafunzo ambayo Jeshi la Polisi limekuwa likitoa kwa maofisa, wakaguzi na askari tumekuwa tukibaini mbinu hizo na kuwakamata.

 “Wanaoshiriki katika usafirishaji walipoona hivyo, walibadili mbinu wakatumia pikipiki lakini nayo tukaibaini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

“Hivi sasa tunaona wamebadili mbinu wanatumia magari ya kifahari na kufikia hatua ya kufunga bendera ili kujificha wasikamatwe lakini nako tumewabaini na kuwakamata,”amesema.

Misime amesema ili kuendelea  kukabiliana na uhalifu huo, Jeshi la Polisi limejikita kubaini na kuzuia kwa kutoa mafunzo ya ndani na nje kwa askari ili kuwajengea uwezo  wa kuwabaini kila mara wahalifu watakapobadili mbinu.

Hatua ya pili ni kuendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kila wakati ili kukabiliana na uhalifu huu.

“Tatu tunaendeleza ushirikiano na nchi jirani ili kubadilishana taarifa na mbinu wanazotumia wahalifu. Nne kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wafahamu juu ya uhalifu huu na madhara yake endapo hautadhibitiwa.

 “Hapa tunawashukuru sana wananchi kwa taarifa zao ambazo zimetusaidia sana katika kudhibiti uhalifu huu,”amesema Misime.

Kwa mujibu wa IOM wakimbizi 20,000 kila mwaka huingia Tanzania, idadi kubwa ya wahamiaji hao wakitokea Ethiopia, Somalia kukimbilia Afrika Kusini.

Mtandao huu umewahi kuhusishwa na watumishi wa umma, aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omar Mgumba aliwahi kueleza kuwa katika uchunguzi wao wameweza kubaini baadhi ya watumishi wa Serikali kutumika katika biashara hiyo haramu kwa kutumia vyombo vya umma katika utekelezaji wa jambo hilo.

Hata hivyo, IOM inaonesha uwepo wa wahamiaji takribani milioni 281 duniani sawa na asilimia 3.6 ya watu wote duniani.