Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

’Uchawa’ bomu linalosubiri kulipuka

Dar es Salaam. Ingawa vijana wamegeukia ‘uchawa’ kama njia ya kipato, wadau wametahadharisha tabia hiyo wakisema ni hatari kwa ufanisi wa viongozi, thamani ya elimu na hata uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa wadau hao, kwa hali ilivyofikia jamii itaamini uchawa ndio njia ya kipato na hivyo watu wataacha kijibidiisha katika kazi, badala yake watawekeza kwenye tabia hiyo, hatimaye Taifa kushindwa kuzalisha.

Licha ya wadau wa kada mbalimbali kuwa na mitazamo hiyo, machawa wenyewe wanasema uchawa ni kazi kama zilivyo nyingine na zinawaingizia kipato hawajali wanavyotafsiriwa na jamii.

Asili ya neno uchawa ni mdudu chawa, ambaye aghalabu hung’ang’ana kwenye mwili wa binadamu. Tabia ya mdudu huyo ndiyo iliyonasibishwa na watu wanaowaganda wenye vipato kuwasifu ili kutengeneza kipato.


Hatari kwa ufanisi

Akizungumzia hilo, Mtaalamu wa saikolojia, Ramadhan Masenga anasema uchawa unachochea kuporomoka kwa ufanisi wa utendaji kwa viongozi wa kisiasa na Serikali.

Hilo linatokana na kile alichofafanua, viongozi hao wanaamini hata wakifanya vibaya watatumia fedha kuwalipa machawa kuwasifia, hivyo utendaji duni wao hautajulikana.

“Uchawa unasababisha watu wasijitume na hata wenye nguvu ya maamuzi wasiogope kufanya ya ovyo kwa sababu wana watu watakaowasifia,” anasema.

Anasema kwa sasa wanasiasa wamekuwa maarufu sio kwa sababu wamegusa maisha ya watu, bali wanaweza kulipa fedha watu wa kuwasifia wakasikika.


Uchawa unaua thamani ya elimu

Kwa mujibu wa Masenga, hali ya uchawa ilipofikia itashusha thamani ya elimu na molari ya ufanyaji kazi katika jamii, kwa kuwa watu wameshajua mzizi wa kupata fedha ni kusifia sio kufanya kazi.

“Tumeondoa dhana kwamba ili kuendesha maisha yako vizuri unapaswa kufanya kazi kwa bidii, badala yake siku hizi unaweza usijitume na ukawa na maisha mazuri kwa kuwasifia viongozi,” anasema.

Athari za uchawa kwa mujibu wa Masenga, zinagusa hata maisha kwenye jamii kwa watu kuona ndio njia rahisi ya kutengeneza kipato bila kuvuja jasho.

Kwa sababu watoto wanaozaliwa wanayaona maisha hayo, anaeleza hatari yake, watakapokua hawatoona umuhimu wa kusoma, kufanya kazi kwa bidii, badala yake wataamini uchawa unalipa.

“Iwapo mtu anajisifu kutengeneza fedha nyingi kwa kumsifia mtu, halafu kuna anayefanya kazi kwa nguvu na hapati hata robo ya anachopata chawa, moja kwa moja hatoona thamani ya kazi anayoifanya.

“Tukiwa wadogo tuliambiwa soma kwa bidii na fanya kazi kwa bidii kwa kuwa ndio mambo yanayojenga thamani ya maisha yako, lakini hilo limebadilika kwa sasa, wenye maisha mazuri na walio karibu na wanasiasa na wasanii ni machawa,” anafafanua.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sabatho Nyamsenda amedai baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikieneza uchawa kama tunu mpya ya Taifa.

"Wanaojiita machawa huonekana mara kadhaa wakidhihaki elimu kwa husambaza video wakiwakejeli vijana wenye elimu wasio na ajira au wenye mshahara mdogo, huku wakisema kuwa kusoma ni kupoteza muda," anasema Nyamsenda na kuongeza:

"Sijawahi kuona waziri wa elimu akikemea tabia hii, cha kushangaza, machawa hawa hualikwa kusherehesha dhifa za kitaifa, jambo linalosababisha wengi kudhani ujumbe unaoenezwa na machawa hawa una baraka za viongozi, sio ajabu kuwa hata vijana wa vyuo vikuu wameanza kuiga mtindo huu."


Ni hatari kwa uchumi

Mwanazuoni wa uchumi, Profesa Abel Kinyondo anasema hali ya uchawa kwa sasa inaweza kuonekana kawaida kwa kuwa, bado wapo wanaoendelea kufanya kazi kwa bidii na zikaleta uzalishaji kwa Taifa.

Kadiri uchawa unavyoendelea, anasema utafika wakati hata wanafanya kazi kwa bidii watawekeza kwenye uchawa kwa kuamini kuwa unalipa zaidi.

Ukifika wakati huo kwa mujibu wa Profesa Kinyondo, hakutakuwepo tena shughuli za uzalishaji katika nchi, hawatakuwepo wazalishaji badala yake watu watabaki kuwa machawa.

Mwanazuoni huyo anaeleza uchawa hauzalishi na hauna matokeo chanya na watu wanapoacha kuzalisha na kusoma, Taifa halitazalisha chochote na ndio sababu ya anguko la uchumi.

“Mwisho wa siku tutabakia kuwa nchi iliyojaa machawa wasiozalisha chochote, hizo kodi zinazotumika kulipa machawa hazitapatikana, tutabaki kuangaliana kama maboya,” anasema.

Anatolea mfano wa Taifa la Singapore, akisema limeweka msingi wa maendeleo ya yeyote ni uwezo, bidii na ustadi wake.

“Ukifanya hivyo utamfanya yeyote aliyepo kwenye jamii afanye kazi kwa bidii, atafute uwezo ili kupata matokeo au atoboe kwa njia hiyo tutakomesha uchawa,” anasema.

Machawa wenyewe wanasemaje?

Ingawa uchawa unabeba tafsiri hasi, Revokatus Chipando, maarufu Babalevo, aliyejinasibu kwa uchawa, anasema hiyo ni kazi kama zilivyo nyingine.

 “Uchawa wenyewe ni kazi ni shughuli na tena ni shughuli nzito kweli kweli… kwa sababu kuna muda mwingine unatukanwa, unadhihakiwa na kusemwa vibaya, lakini ilimradi riziki inapatikana,” anaeleza.

Kwa mujibu wa Babalevo, kadri bosi anavyoona unapitia magumu kutokana na kumsifia, mara nyingi ndio anaongeza upendo na pengine kukulipa zaidi.

Hata hivyo, anaunasibisha uchawa na kile alichokiita upambe, akisema kazi za wawili hao zinafanana, lakini jamii ikaamua kuwaita machawa ili kuwadhihaki.

“Waliniita hivyo (chawa) kwa lengo la kunidharau na kunidhihaki, nikaamua ngoja niivae uchawa wenyewe. Nikasema sawa mimi ni chawa ilimradi riziki inaingia na inapatikana sio shida,” anaeleza.

Kwa sababu ya uchawa, Babalevo anasema vijana wengi wamejipatia riziki na hata yeye, kwa sasa anamalizia ujenzi wa nyumba yake ya tatu ya ghorofa kwa shughuli hiyo.

“Hapa ninavyoongea na wewe nipo eneo la ujenzi najenga nyumba yangu ya tatu ya ghorofa, ukiniita chawa nina hasara gani,” anasema Babalevo.

Jina la uchawa lilikuwa shubiri kwa Neema Karume aliyekuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Chawa wa Mama, anayesema walizongwa kiasi cha kubadili jina.

Kuzongwa kwao, anasema kulisababishwa na tafsiri ya jina husika, linalomaanisha kujipendekeza, ambayo kiuhalisia si nzuri mbele ya jamii.

“Chawa pia anatafsiriwa kuwa mtu anayesifia uongo, kwa hiyo viongozi na watu mbalimbali wakawa wanatusema tukabadili. Ilituathiri kwa sababu maneno yalikuwa mengi na viongozi walikuwa wanatushambulia na kuna wakati tulikuwa tunasumbuliwa kwa kuitwa chawa,” anasema.

Licha ya mitazamo hiyo, Neema anaeleza wakati wanajiita jina hilo waliona ni uzalendo na kupambana kuyasema mazuri ya kiongozi wao.