Uchawa huu utawaumiza wabunge 2025

Katika mchakato wa uchaguzi mkuu, wapambe wa viongozi, hususan wabunge, wamekuwa wakicheza nafasi muhimu sana.
Hata hivyo, nafasi hii inaweza kuwa na athari hasi iwapo wapambe hawa watatumia vibaya madaraka yao.
Uchambuzi huu utaangazia jinsi wapambe wanavyoweza kusababisha pigo kwa wabunge katika uchaguzi mkuu ujao, hasa kupitia tabia yao ya kuwazuia wananchi kuonana na wabunge bila sababu za msingi.
Wapambe, au chawa kama wanavyojulikana kwa lugha ya mtaani, ni watu wanaomzunguka kiongozi wa kisiasa kwa lengo la kumsaidia kutekeleza majukumu yake.
Ingawa wanapaswa kusaidia kuimarisha uhusiano kati ya kiongozi na wananchi, mara nyingi wanaweza kuwa chanzo cha matatizo.
Moja ya tabia mbaya za wapambe ni kuwazuia wananchi kuonana na wabunge wao bila sababu za msingi.
Hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa mbunge mwenyewe na hata kwa chama chake kwa ujumla wake. Baadhi ya athari hizo ni pamoja na:
Kukatisha tamaa wananchi: Wananchi wanapokataliwa bila sababu za msingi kuonana na mbunge wao, wanapata hisia kwamba hawathaminiwi.
Kushuka kwa umaarufu wa mbunge: Umaarufu wa mbunge unategemea uhusiano wake na wananchi. Wapambe wanapowazuia wananchi, umaarufu wa mbunge hupungua.
Hii ni kwa sababu wananchi wanaona kwamba mbunge huyo hana muda nao au hawajali.
Kupoteza uaminifu: Wananchi wanapokuwa na matatizo au masuala wanayotaka kushughulikiwa, wanamtegemea mbunge wao. Wanapozuiwa kumwona, wanapoteza imani kwa mbunge huyo.
Uaminifu ni kitu muhimu katika siasa, na kukipoteza kunaweza kumgharimu mbunge ushindi katika uchaguzi ujao.
Kuchochea upinzani: Wapambe wanapowazuia wananchi kuonana na mbunge, wanachochea hasira na upinzani miongoni mwa wananchi. Hii inaweza kusababisha kuibuka kwa wagombea wapya wenye nia ya kukidhi mahitaji ya wananchi na kuwafikia kwa urahisi zaidi.
Sababu za kuibuka kwa tabia ya wapambe kuwazuia wananchi kuonana na wabunge hutokana na sababu zifuatazo:
Ubinafsi na maslahi binafsi: Wapambe wanaweza kuwa na nia ya kujinufaisha wenyewe badala ya kumsaidia mbunge kutekeleza majukumu yake.
Eneo hili ‘chawa’ wengi hawataki kuona watu wengine wanakuwa karibu na mheshimiwa ili watu hao wasipate maslahi kama wanayopata wao. Huu tunauita ubinafsi!
Ukosefu wa uelewa: Wapambe wengine wanaweza wasielewe umuhimu wa mbunge kuwasiliana moja kwa moja na wananchi wake. Huu tunaita upumbavu!
Hofu ya kukosolewa: Wapambe wanaweza kuhofia kwamba wananchi watamkosoa mbunge wao, hivyo wanajaribu kumkinga. Baadhi ya wapambe tumeshuhudia kwenye makundi sogozi ya mitandao ya kijamii wakiwashambulia watu wanaowaona wanawakosoa wabunge kwenye maeneo yao.
Kuna siku nikiwa kwenye kundi moja la mtandao wa kijamii, ‘chawa’ wa mbunge mmoja walikuwa wanashindana kutuma taarifa ya mbunge kupeleka walimu wa kujitolea kwenye baadhi ya shule za jimbo lake, ilhali huo ni mpango wa Serikali.
Cha kushangaza wakati ‘chawa’ hao wakilazimisha wananchi wamuone mbunge anaupiga mwingi, upande mmoja wa jimbo hilo lililoko kwenye mikoa ya kanda ya Kusini, wananchi wake wamekaa miezi mitatu bila mawasiliano kati yao na makao makuu ya wilaya kutokana na ubovu wa barabara.
Kutoka nauli ya Sh4,000/ mpaka mjini, wananchi wa maeneo hayo walikuwa wakilipa kati ya Sh15,000 mpaka 30,000 kwenda mjini, na hakuna mpambe yeyote aliyethubutu kumnong’oneza mbunge hali ngumu inayowakabili wananchi.
Ushauri wangu ili kuepuka athari hizi, ni muhimu kwa wabunge kwanza kuwa na mfumo wa uwajibikaji. Waruhusu wananchi kutoa malalamiko kuhusu wapambe.
Pili, wabunge wanapaswa kuwa na mikutano ya mara kwa mara na wananchi wao ili kuhakikisha wanapata fursa ya kusikiliza kero na changamoto zao moja kwa moja, sio wanafanya mikutano ya ujanja ujanja kutafuta sifa.
Tatu, wabunge wanapaswa kuwapa maelekezo wapambe wao kuhusu umuhimu wa kushirikiana na wananchi na kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki.
Wapambe wa viongozi, hasa wabunge, wanaweza kuwa na athari kubwa kwa ufanisi wa mbunge katika uchaguzi mkuu ujao.
Tabia yao ya kuwazuia wananchi kuonana na wabunge inaweza kusababisha hasira, kukatisha tamaa na kupoteza uaminifu wa wananchi.