Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uchawa saratani inayolemaza wasomi

Umewahi kujiuliza, kama wakoloni wangekuwa bado wanaendeleza unyonyaji Tanzania, tungepata vijana jasiri wa kuukataa ukoloni na kuwa tayari kufa kwa ajili ya taifa lao? Hali ilivyo sasa, ni vigumu kusema ndiyo.

Tukikumbuka mchango wa vijana waliopigania uhuru wa taifa letu na kuulinganisha na kizazi cha sasa, ama utalia au utashangaa kwa matendo yao.

Vijana wa sasa ni wasomi waliobobea,lakini mazungumzo yao mara nyingi hayana manufaa.

Kama si kujadili mapenzi, basi ni mpira au kuzunguka mitaani wakimsifia au kumkosoa kiongozi fulani aliyeonekana kuwa na fikra tofauti na watawala.

Vijana wa aina hii, enzi za ukoloni, wasingeweza kuongoza mapambano ya ukombozi badala yake, wangekuwa wakisaidia mkoloni kuendelea kunyonya rasilimali za taifa.

 Wengine wangetamani hata uzao wa wakoloni uendelee kwenye uongozi ili wao waendelee kufaidika na maslahi binafsi.

Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes, Oscar Kambona na wengine wengi walikuwa vijana wa mfano waliothibitisha kuwa uzalendo ni zaidi ya maslahi binafsi.

 Walihakikisha Watanzania wanapata uhuru wao, licha ya kuwa na fursa ya kupata maisha mazuri binafsi.

Pamoja na kuwa wachache wenye elimu wakati huo, vijana hao walionyesha uthabiti wa kupigania maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi.

Hawakuwa wachumia tumbo, bali walikuwa watu wenye dhamira ya kweli ya kuwakomboa wenzao kutoka kwa mkoloni.

Elimu waliyopata haikuwa daraja la kujitenga na wananchi, bali ilikuwa mwanga uliowaonyesha njia ya kupigania haki na uhuru wa nchi yao.

Hakuna aliyekuwa mnafiki kwa mkoloni; wote walikuwa na dhamira moja ya kuleta ukombozi wa kweli kwa Tanganyika.

Leo hii vijana wa sasa wanashindwa hata kutumia elimu yao kutatua changamoto zao binafsi, sembuse kupigania haki za wenzao.

Si kwamba mimi ni mzee nawaponda vijana wenzangu, hapana. Mimi mwenyewe ni kijana, lakini ninapobadilishana mawazo na vijana wenzangu, nabaini kuwa licha ya elimu waliyonayo, bado ujinga wao ni mwingi kila mmoja ni mpambanaji wa tumbo lake na ndio maana imekuwa rahisi kuwa chawa wa watawala na wamekuwa wakisifu kila kitu ilimradi kiwe kimefanywa na mwenye mamlaka.

Kundi hili limekuwa kubwa na linaongezeka kila siku kwasababu njaa nayo inaongezeka na mbinu za sifa zinaendelea kubuniwa hadi kuanzishwa taasisi ya machawa.

Hawa si wazalendo wa taifa, bali wanajipa jukumu la kutetea watawala kwa sababu tu wanapata chochote kitu.Kwa hali hii, ni vigumu kusema kuwa tungeweza kupata vijana wa kupigania taifa kama ilivyokuwa enzi za ukoloni.

Mwalimu Nyerere aliandika katika kitabu chake Tujisahihishe, akisema: “Ukiona nataka kulipiga teke jiwe kwa kuwa nafikiri kuwa ni dongo au mpira, natumaini utanionya. Lakini nikilipuuza onyo lako kwa sababu eti wewe ni mdogo au kwa sababu sikupendi, nikalipiga teke, basi litanivunja dole, japo ningekuwa nani.”

Vijana wa sasa tunafanya makosa na hatutaki kuelekezwa. Tumekuwa wakali tunapokosolewa, mithili ya mbwa mwenye kichaa. Tumeachwa tukisimama pasipo kuona mbele, tukitumiwa kama ngao ya kuwalinda watawala hata wanapokosea.

Uchawa ni saratani inayoendelea kututafuna. Saratani isipotibiwa mapema husambaa mwilini na hatimaye kuwa hatari zaidi.

Ikiwa imeathiri mguu, basi sharti mguu huo ukatwe ili kuokoa maisha. Hali yetu kama vijana imefikia hatua mbaya; tunahitaji tiba sasa kabla ya ugonjwa huu kutumaliza.

Ni wakati wa vijana kuamka. Tuondoe mgawanyiko wa vyama na itikadi zinazotugawa, tuangalie kwa makini viongozi tuliowachagua—wanatufanyia nini? wanachangia vipi maendeleo ya Taifa letu? Tusikubali kuwa vipofu wa kutumiwa kwa maslahi ya wachache.

Tupaze sauti zetu si kwa ajili ya matumbo yetu, bali kwa ajili ya Tanzania. Tuilinde nchi yetu kwa uzalendo wa kweli.

Tuwatambue viongozi kuwa ni wawakilishi wetu, si miungu wa kuabudiwa. Taifa hili linahitaji vijana wenye mawazo mapya, wenye ujasiri wa kusimama kwa haki na wenye dhamira ya kweli ya kulinda maslahi ya wengi.

Baraka Loshilaa ni mwandishi wa Mwananchi