Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

‘Sera mpya ya elimu haina budi kutekelezwa’

Muktasari:

  • Mwandishi Mwandamizi wa habari za elimu kutoka magazeti ya The Citizen na Mwananchi, Jacob Mosenda amesema sera ya elimu ilikuwa ikingojewa kwa muda mrefu japokuwa katika utekelezaji changamoto hazitokosekana, lakini lengo litafikiwa.

Dar es Salaam. Mwandishi Mwandamizi wa habari za elimu kutoka magazeti ya The Citizen na Mwananchi, Jacob Mosenda amesema sera ya elimu iliyokuwa ikingojewa, sasa inapaswa kutekelezwa pamoja na changamoto zitakazojitokeza.

Amesema mabadiliko ya sera yamefanyika mara kadhaa, lakini kwa muda mrefu wadau walikuwa wanaamini kuna mambo mengi muhimu hayakuwa yakitekelezwa kwenye sera ambayo inatumiwa.

Hivi karibuni Serikali ilitoa waraka wa elimu Namba 5 ambao pamoja na mambo mengine unazungumzia ufundishaji wa masomo ya mtalaa mpya kwa wanafunzi wa msingi na sekondari na unaanza kutumika mwaka huu kuanzia darasa la tatu.

Akizungumza kwenye mjadala wa mtandao wa X wa Mwananchi leo Jumatano Januari 3, 2024 wenye mada iulizayo ‘Kuanza kutumia mtalaa mpya wa elimu je, tumejipanga kikamilifu?’ Mosenda amesema nchi haijakurupuka ila kilichopo sasa utekelezaji unaanza kwa hatua.

Amesema hatujaanza kutekeleza kila kitu kwenye sera na lengo ni kumfanya mtoto wa Kitanzania ajitegemee kupitia mtalaa huo mpya.

Mosenda amesema hatua iliyofikiwa ni kubwa na haikuwa ya kukurupuka kwa sababu mchakato umehusisha wadau. Hivyo anaamini nchi imejipanga. Amesema kwa muda mrefu wadau wa elimu wamekuwa wakiingojea sera mpya kiasi cha kukata tamaa.

 “Kinachotakiwa ni kuisaidia Serikali ili kutimiza azma ya kuboresha elimu kwa Watanzania. Hivyo kuanza kutumia mtaala mpya wa elimu ilikuwa ni kilio kwa wadau kuhakikisha tunapata mtalaa unaokwenda na wakati.

“Utekelezaji wake kuanzia ngazi ya awali ni jambo la hatua kwa hatua kwani hatujaanza kutekeleza mambo yote yaliyopo kwenye sera. Hadi ifikapo mwaka 2027 ndipo tutaanza kupata picha,” amesema Mosenda.

Ameongeza kuwa popote kwenye mabadiliko au mapinduzi hakukuwa na muda maalumu wa maandalizi, kwa hiyo kama Taifa kilio cha wadau kilikuwa kuhakikisha tunapata sera mpya na mitaala basi imepatikana na utekelezaji wake utakuwa hatua kwa hatua.

“Kwa mwanzo huu changamoto zitakuwepo lakini tuamini mwisho wa siku wote tutakutana stendi na kuanza safari bila kumuacha mtu nyuma, mapinduzi haya yalikuwa ya muhimu hivyo utekelezaji wake ni hatua muhimu,” amesisitiza.

Mosenda amesema kinachotakiwa kufanywa sasa ni uelimishaji kwa umma namna gani utekelezaji utawaathiri ili wajipange kisaikolojia.

Mosenda anaungwa mkono na mdau wa elimu, Mwalimu Ivan Magembe aliyesema kuanza kwa mtaala mpya ni jambo la msingi kwa sababu unaendana na mazingira ya sasa.

Amesema unavyotengeneza mfumo wa elimu ni lazima uupe thamani huku akisisitiza kuwa kwa sasa elimu sio jambo la sifa bali ni uwekezaji.

“Jambo la msingi ni mfumo wa utawala wa hizi shule zetu,  ukiwa mbovu hata umlete malaika huwezi kupata matokeo.  Ni muhimu kuboresha mifumo ya utawala wa shule mfano kama inahusika na mkondo wa kilimo basi ihusike kusimamia rasilimali zake,” amesisitiza.