‘Polisi imarisheni ushirikiano na Jamii’

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai akizungumza katika hafla ya kutoa vyeti na zawadi kwa Askari waliofanya vizuri 2024. Picha na Hawa Kimwaga.
Muktasari:
- Umuhimu wa kuboresha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii utarahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu zinazohusu usalama.
Tabora. Ushirikiano baina ya polisi na wananchi umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kuimarisha ulinzi na usalama wa jamii.
Akizungumza leo Jumatano, Mei 7, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora amesema Jeshi la Polisi linapaswa kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia misingi ya sheria ili kuhakikisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuboresha uhusiano kati ya Jeshi la Polisi na jamii ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa muhimu zinazohusu usalama.
“Kaeni karibu na wananchi. Iwe ni kwenye misiba au sherehe, polisi nao ni sehemu ya jamii. Hili litawawezesha kupata taarifa kuhusu vitendo vya ukatili, biashara haramu ya dawa za kulevya na uhalifu mwingine,” amesema Tukai.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Richard Abwao amesema katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, jumla ya makosa ya jinai 16,553 yaliripotiwa, ikilinganishwa na 17,203 kwa kipindi kama hicho mwaka 2023, hivyo kupungua kwa makosa 650 sawa na asilimia 3.5.
Kamanda Abwao aliongeza kuwa makosa makubwa ya jinai kwa mwaka 2024 yalikuwa 1,592, yakilinganishwa na 1,602 kwa mwaka 2023, ikiwa ni punguzo la makosa 10 sawa na asilimia 0.6.
Hata hivyo, makosa ya usalama barabarani amesema yaliongezeka na mwaka 2024 kuliripotiwa matukio 75,732, ikilinganishwa na 73,197 kwa mwaka uliotangulia, ongezeko la matukio 2,535 sawa na asilimia 3.5.
Kamanda huyo amesema hali hiyo ni matokeo ya elimu kwa jamii na operesheni mbalimbali za usalama barabarani wanazozifanya kila mara.
Mmoja wa wananchi wa Tabora, Hussein Nkumilwa amesema licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado Jeshi la Polisi linapaswa kuongeza juhudi kw sababu wahalifu hubadilika na kujipanga upya kila siku.
“Wahalifu wanaweza kutoka hata nje ya Tabora. Hivyo, juhudi za kudhibiti uhalifu zinapaswa kuendelea kwa nguvu zaidi,” amesema Nkumilwa.
Mjasiriamali, Ashura Mwazembe amesema hali ya usalama imeboreshwa kutokana na ushirikiano wa karibu na Jeshi la Polisi mkoani humo limeendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na namna ya kujilinda.
“Tunafanya biashara kwa amani na tunapewa elimu ya kujikinga na ukatili, hasa kwa watoto wetu. Tunahisi tunalindwa,” amesema Mwazembe.