Prime
IPOA itasaidia kuisafisha Serikali, Jeshi la Polisi

Chuki dhidi ya Polisi ni kubwa kutokana na kunyooshewa kidole kuhusu matukio ya utekaji, mauaji na kupotea kwa watu, lakini kama tungekuwa na chombo huru kama IPOA ya Kenya ingesaidia kuisafisha Serikali na Jeshi la Polisi.
IPOA - Independent Policing Oversight Authority ni mamlaka huru ya kiraia nchini Kenya iliyoundwa kwa sheria ya IPOA namba 35 ya mwaka 2011. Kifungu cha 6 cha sheria hiyo kimeainisha majukumu ya mamlaka hiyo.
Majukumu ya IPOA ni pamoja na kuchunguza vifo na majeraha mabaya yanayosababishwa na matendo ya baadhi ya polisi na kuchunguza utovu wa nidhamu wa polisi ambao ama umeripotiwa na raia au mamlaka za kiserikali.
Mengine ni kufuatilia uchunguzi unaofanywa na kitengo cha mambo ya ndani polisi, kukagua mahabusu za polisi kama zinakidhi viwango vya kisheria na kikatiba na kufuatilia operesheni za polisi ili kuzuia matumizi mabaya ya madaraka.
Afrika Kusini ina mamlaka kama hiyo inayojulikana Independent Police Investigative Directorate (IPID) na kama ilivyo IPOA, jukumu lake ni kuhakikisha Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake ndani ya sheria na kwa mujibu wa Katiba.
Siku zote nasema ukweli una sifa moja kuu, kwamba hata ukiuchukia au kuukataa haugeuki kuwa uongo. Ni ukweli ulio dhahiri chuki za baadhi ya raia ni kubwa, nina wasiwasi na usalama wa mmoja mmoja huko tuendako.
Bahati mbaya, wapo polisi ama wamejenga nyumba uraiani au wanaishi huko ambako chuki inayopandwa dhidi yao ni kubwa na inawezekana kuna genge la uhalifu ndani ya Polisi au nje linalotekeleza matukio haya.
Njia pekee ya kuwalinda askari Polisi wetu wema dhidi ya wanaokwenda kinyume cha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi au kubaini kama Polisi ndio wahusika au la, ni kuanzisha chombo huru cha kushughulikia malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi.
Taswira ya Jeshi la Polisi kwa wananchi si nzuri na hili lilisemwa katika ripoti ya Tume ya Haki Jinai kuwa kumekuwapo malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi hilo.
Ukisoma ripoti hiyo ya Julai 2023 iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan, ukurasa wa 31 kifungu 3.1.1 inasema malalamiko dhidi ya Jeshi la Polisi yanasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutotoa ushirikiano unaotakiwa.
Kwa mujibu wa Tume, malalamiko yalihusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio ya uhalifu.
Lakini sasa Polisi wananyooshewa kidole katika kila tukio la utekaji, kupotea kwa watu, mauaji na kushambuliwa kwa kipigo kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema waliokwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Aprili 24, 2025.
Viongozi na wanachama waliokamatwa na Polisi wenye sare siku hiyo, baadhi ikidaiwa walitupwa porini katika Msitu wa Pande, walikwenda kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema (Taifa), Tundu Lissu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amekana kuwakamata viongozi na wanachama hao isipokuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema, John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika.
Kauli hii katikati ya sintofahamu ni kama imechochea chuki dhidi ya Polisi kwa kuwa baadhi walionekana wazi wakiwakamata na kuwapiga baadhi yao, ukiacha wanadai walikwenda kutupwa msituni.
Kuna matukio kama ya kuuawa Ally Kibao aliyetekwa kwenye basi na kwenda kuuawa kikatili, kupotea kwa kina Deusdedith Soka na kushambuliwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima.
Pia kuvamiwa na kushambiliwa mwanaharakati, Mdude Nyagali mkoani Mbeya usiku wa kuamkia Mei 2, 2025. Polisi imejiweka kando na tukio hilo.
Ili kuisafisha Serikali na Jeshi la Polisi kutokana na mlolongo wa matukio hayo na mengine ya aina hiyo, njia pekee ni kuunda chombo kama IPOA ya Kenya.
Sababu ni moja, kama Rais Samia alivyowahi kusema akizungumzia tukio la maofisa wa Polisi kule Mtwara kutuhumiwa kumuua mfanyabiashara wa madini, kwamba hawawezi wakalalamikiwa na raia wakajichunguza wenyewe.
Kuna hisia ndani ya jamii kwamba, vitendo vya utekaji, utesaji na kupotea kwa watu havifanywi na Jeshi la Polisi bali chombo kingine lakini msalaba wanabebeshwa Jeshi la Polisi.
Pia kuna hisia za uwapo wa magenge ya kihalifu yenye mrengo wa kisiasa, ambayo yameundwa mahususi kushughulika na wakosoaji wa Serikali na kundi hili lina nguvu, lina rasilimali na vifaa kama magari ya kifahari, silaha na pingu za kipolisi.
Kutokana na uwapo wa udhaifu katika ukamataji usiozingatia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) na Kanuni za Utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO), magenge hayo yamekuwa yakijitambulisha kama Polisi yanapotekeleza uhalifu.
Mke na majirani katika tukio la kuvamiwa na kushambuliwa Mdude Nyagali, wanadai waliotekeleza uhalifu huo walijitambulisha kuwa askari Polisi, jambo lililokanushwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya. Swali linabaki ni nani waliofanya tukio hili?
Ni kweli yapo matukio polisi walikamata watu na wakatambuliwa, lakini ndugu jamaa na marafiki walipofuatilia katika vituo vya polisi walikana kuwashikilia, baadaye walikiri kuwashikilia. Katika mazingira hayo ukweli unapatikanaje bila IPOA?
Ninaamini kama IPOA ingekuwapo nchini, matukio ya Polisi kukiuka haki za binadamu yangepungua kwani wangekuwa wanajua kipo chombo huru cha uchunguzi ambacho hakitawabeba na kila mmoja anabeba msalaba wake.
Ilivyo sasa chuki zinazidi kumea dhidi ya Jeshi la Polisi hali inayojidhihirisha kwenye mitandao ya kijamii kama Club House na X baadhi wakitaka kuwadhuru askari na familia zao, haya hayana afya kwa Taifa.
Raia wanaweza wasifikishwe huko kama tu kutakuwa na chombo huru wanachokiamini kuwa kikichunguza kitaleta mrejesho wa kweli wa nani ni mhusika, ni Jeshi la Polisi, chombo kingine cha Dola au magenge ya kihalifu.
Sumu inayoenezwa mitandaoni si ya kupuuza kwani baadhi ya askari wanaishi uraiani.
Ni muhimu kuwa na chombo kama IPOA ili kuchunguza kila lalamiko dhidi ya Polisi. Kwa kufanya hivyo, tutawatendea haki Polisi wanaochukizwa na matendo ya kikatili dhidi ya raia lakini wanachanganywa kapu moja na wanaonyooshewa kidole katika kushiriki matukio ya kikatili dhidi ya raia.
Ni IPOA pekee itawaweka huru polisi wema na kuisafisha Serikali ili itakaposema haihusiki, umma uamini badala ya ilivyo sasa Polisi au kiongozi wa Serikali akipata matatizo ni furaha kwa baadhi ya watu mitandaoni.
Daniel Mjema anapatikana kwa namba 0656600900