NBC Connect aina mpya ya utoaji huduma za kibenki

Muktasari:
- Benki ya Taifa ya Biashara ya (NBC) imezindua huduma mpya ya kibunifu za kidijitali NBC Connect kwa lengo la kuwasogeza karibu huduma zake kwa wananchi.
Dar es Salaam. Katika mkakati wa kuwasogezea wateja huduma ya kifedha, Benki ya Taifa ya Biashara ya (NBC) imezindua huduma mpya ya kibunifu za kidijitali NBC Connect.
Ubunifu unalenga kuondoa usumbufu wa upatikanaji wa huduma na hivyo kuwarahisishia wateja huduma hizo kwa kutumia simu za mkononi na vifaa vingine vinavyotumia intaneti.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa huduma hiyo iliyofanyika jijini Mbeya, Mkurugenzi wa wateja wakubwa wa benki hiyo, James Metairon amesema kuwa mfumo huo mpya utampatia mteja fursa ya kufanya miamala yao ya kifedha na huduma za kibenki kwa urahisi zaidi.
“Huduma hii itawapa wateja wetu uwezo wa kufanya aina zote za malipo ikiwa ni pamoja na malipo ya ndani na nje ya nchi, malipo ya Serikali pamoja na mitandao mbali mbali ya simu za mkononi kwa kutumia simu kompyuta,” amesema.
Metairon alisema ubunifu huo umetengenezwa kwa teknolojia ya kisasa na yenye usalama wa hali ya juu ambayo imezingatia na kutoa kipaumbele kwenye usiri wa taarifa za mteja.
"Tunafuraha kutambulisha NBC Connect kwa wakazi wa Mbeya na maeneo ya jirani. Mfumo huu wa kibenki wa kidijitali ni uthibitisho wa dhamira ya kuwapatia wateja wetu huduma bora za kibenki ambazo ni rahisi, salama,’’ amesema.
Amesema pamoja na huduma rahisi na za kisasa, ujio wa huduma hiyo itakuwa inatoa usaidizi wa binafsi kwa wateja kupitia vituo vyao vya huduma kwa wateja ambapo kupitia mameneja katika vituo hivyo watawasaidia wateja kulingana na mahitaji yao.
"Tunawaalika wateja wetu wote wa Mbeya na maeneo ya jirani wajionee urahisi na usalama wa NBC Connect. Ni huduma ambayo inaleta mapinduzi mapya katika namna huduma za kibenki zinatolewa. Tuna uhakika kuwa wateja wetu watanufaika nayo kwa kiasi kikubwa,"ameongeza Metairon.
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Benno Malisa aliishukuru taasisi hiyo kwa ubunifu wao mzuri na kuwahimiza wateja kutumia mfumo huo mpya wa kibenki ili kurahisisha shughuli zao za kila siku.
“Uzinduzi wa NBC Connect jijini Mbeya unawakilisha mpango mkakati wa upanuzi wa benki ya NBC ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi,’’ Amesema.
Malisa alionyesha kuguswa zaidi na dhamira kubwa ya benki hiyo katika kuwajibika kwa jamii kupitia mipango mbalimbali, kama vile Mbio za Kimataifa za NBC Dodoma zinazohamasisha na kutibu saratani ya shingo ya kizazi.
“Kupitia udhamini wa Ligi Kuu ya NBC mbali na kuongeza ubora wa ligi yetu na kuongeza burudani kwa Watanzania udhamini huo umeongeza fursa za ajira kwa vijana na maofisa wengine wengi wa vilabu husika. Hakika napongeza juhudi hizi zinazofanywa na NBC” amesema Malisa.
Uzinduzi wa NBC Connect jijini Mbeya ulienda sambamba na uzinduzi wa tawi jipya lililofunguliwa katika Soko la Mwanjelwa litakalotoa bidhaa na huduma mbalimbali za kibenki, zikiwemo akaunti binafsi na za biashara, mikopo, akiba na uwekezaji, huduma za fedha za kigeni na kidijitali.