'Mapambano usawa wa kijinsia yasiwaache wanaume nyuma'

Dar es Salaam. Wakati wanawake wanapigania harakati za usawa wa jinsia, wametakiwa kutoacha kundi la wanaume nyuma kwani suala hilo linahitaji nguvu za pamoja.
Hayo yalisemwa leo Jumanne Novemba 7, 2023 na aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Afrika Kusini Dk Phumzile Mlambo Ngcuka, katika ufunguzi wa tamasha la 15 la jinsia linalofanyika kwa siku nne jijini humo.
Dk Ngcuka, amesema ushirikishwaji huo wa wanaume unatakiwa kufanywa hata katika matamasha mbalimbali na majukwaa ya kupigania usawa wa kijinsia ambapo huko wataweza kupata elimu na kwenda kuwaelemisha wanaume wenzao.
"Hatuwezi kupiga hatua mbele kama tutawaacha wanaume katika mapambano hayo, kinachotakiwa ni kuangalia mambo mengine ambayo walikuwa wanaonekana wao wanatuzidi basi wasituzidi wala kutuacha," amesema.
Dk Ngcuka ambaye pia amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mtendaji wa ‘UN Women’ kuanzia Agosti 2013 hadi Agosti 2021, ameupongeza Mtandao wa Jinsia (TGNP), kwa mchango wake katika kupigania usawa.
“Unapozungumzia harakati za usawa wa kijinsia nchini, huwezi kuacha kuutaja mchango mkubwa ulitolewa na TGNP ambao huwafikia hadi wananchi ngazi za shina kwa kuwaleta pamoja na kupaza sauti zao katika masuala mbalimbali ya kijinsia,” amesema.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, alisema tamasha la mwaka huu ni kusheherekea safari yao tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo ambapo wanapata fursa ya kutafakari mafanikio, changamoto, mambo waliojifunza pamoja na kubadilishana uzoefu.
"Pia kuja na mikakati ya namna ya kukuza ushiriki wa wanawake katika michakato ya utoaji wa maamuzi na nafasi za uongozi kupitia chaguzi zijazo,"alisema Lilian.
Aidha alisema tamasha hilo linalenga kujenga uelewa wa muktadha wa ufanyaji maamuzi hususani yale yanauohusu mgawanyo wa rasilimali katika ngazi ya dunia, kikanda na kitaifa kwa kuchota maarifa kutoka kwa wengine waliofanikiwa.
Naye Mwenyekiti wa TGNP, Gema Akilimali, amesema wakati wanasherekea miaka 30 ya kuanzishwa kwa taasisi yao wanajivunia mafanikio mballimbali ikiwemo kubadilishwa kwa miundo ya sheria iliyokuwa ikiuka hakinza wanawake.
Baadhi ya sheria hizo ni pamoja na ile ya makosa ya kujamiana(SOSPA) ,sheria ya vijiji ,kuwepo kwa miongozo ya bajeti ya kijinsia na uundwaji wa madawati ya kijinsia.
"Pia TGNP imeweza kufanya chambuzi mbalimbali za kijinsia ambazo zimekuwaa zikitumika katika mijadala mbalinbali ya nchi,"alisema Gema.
Tamasha la mwaka huu limeshirikisha zaidi ya watu 2000 huku kaulimbiu yake ikiwa ni 'Miaka 30 ya TGNP na Tapo la Ukombozi wa Wanawake'.