Kizungumkuti cha kufufua uwekezaji viwanda vya dawa nchini

Muktasari:
Swali ambalo watafiti, wawekezaji na viongozi wa Serikali wanajaribu kulijibu hivi sasa ni, “Je, sekta hiyo inaweza kunyanyuka tena.”
Dar es Salaam. Kuna miaka sekta ya uzalishaji wa dawa nchini ilikuwa ya kutukuka na kuvutia, lakini sasa hali hiyo haitabiriki tena, wanasema wataalamu na wawekezaji.
Swali ambalo watafiti, wawekezaji na viongozi wa Serikali wanajaribu kulijibu hivi sasa ni, “Je, sekta hiyo inaweza kunyanyuka tena.”
Hatua hiyo inakuja katika wakati ambao Taifa linaangalia uwezekano wa kuifufua sekta hiyo ambayo kutetereka kwake kunasababisha wananchi waendelee kukosa huduma muhimu za afya huku Serikali ikiendelea kupoteza mabilioni ya fedha.
Kila mwaka Tanzania hupoteza zaidi ya Sh800 bilioni kwa uagizaji wa dawa na vifaa tiba kutoka nje. Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji.
Wawekezaji wanasema jambo linaloweza kubadili mwenendo huo ni kwa nchi kuwekeza katika mageuzi ya viwanda vya uzalishaji wa dawa.
Sera iliyopo ni muafaka?
Hapana, haiwezeshi, watafiti na wawekezaji wanasema.
“Sera iliyopo haiwawezeshi kabisa wawekezaji wa ndani katika uzalishaji wa dawa,” anasema Jayesh Shah, ambaye ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa aliyekuwa anamiliki kiwanda cha dawa cha Shelys, siku za nyuma.
“Naamini kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Tanzania kuja na sera isemayo suala la uzalishaji wa dawa ndani ya nchi ni la lazima, tofauti na sera ya sasa ambayo inasisitiza zaidi uagizaji kutoka nje,” anasema Shah ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Sumaria.
Tanzania ilipata mafanikio makubwa katika sekta hiyo katika miaka ya 1990 na hiyo ni kwa ripoti ya Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini (Repoa) iliyotolewa mwaka 2014 ikiwa na kichwa cha habari: Reversing Pharmaceutical Manufacturing Decline in Tanzania: Policy Options and Constraints.
Lakini mafanikio hayo sasa yamebaki kuwa historia.
Ripoti hiyo inasema hadi kufikia mwaka 2014, sekta ya uzalishaji wa dawa ilikuwa tayari imeporomoka.
Wataalamu wanakadiria kuwa hisa za soko la pamoja kati ya Serikali na sekta binafsi ilianguka kutoka asilimia 30 hadi 20 katika kipindi cha mwaka 2006 na 2013.
Licha ya anguko hilo, wadau hao wanabainisha kuwa hakuna juhudi zozote zilizochukuliwa ili kunusuru hali hiyo mpaka sasa.
Shah ambaye aliachana na uwekezaji katika sekta ya uzalishaji dawa nchini, anasisitiza kuwa hakuna njia nyingine ya mkato zaidi ya nchi kutengeneza mazingira rafiki ya kuwezesha wawekezaji wa ndani kushindana na wa nje.
“Gharama za uzalishaji zilikuwa juu tofauti na faida niliyokuwa nikitengeneza, hiyo ndiyo sababu kuu iliyonifanya niachane na biashara hii,” anasema Shah.
Hivi karibuni, Rais John Magufuli alihimiza umuhimu wa Taifa kuwawezesha wazawa kuanzisha viwanda vya dawa; hoja ambayo ameitoa katika wakati ambao sekta hiyo ikihitaji mageuzi makubwa.
“Ni asilimia sita tu ya dawa ndiyo inazalishwa nchini... kwa nini? Lazima tulitatue hili...” alisema Rais Magufuli katika hafla ya uzinduzi wa magari 181 ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Licha ya utashi wa kisiasa ulioonyeshwa na Rais, bado njia ya kuelekea katika uanzishwaji wa viwanda vya ndani haieleweki. Watafiti daima wamekuwa wakisisitiza juu ya mambo muhimu yanayohitaji kufanyiwa kazi.
“Hakuna sekta ya umma iliyo imara kuunga mkono viwanda vya ndani ikilinganishwa na nchi nyingine,” inasema ripoti moja iliyochapishwa katika mtandao wa www.repoa.or.tz.
Licha ya kwamba ripoti hiyo ilichapishwa mwaka 2014, bado mazingira ya uwekezaji hayajabadilika hadi sasa.
Utafiti uliofanywa na Mwananchi unathibitisha hilo baada ya kufanya mahojiano na wadau mbalimbali katika sekta hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Repoa, wazalishaji wa ndani wanaachana na biashara hiyo kwa sababu mbalimbali ikiwamo inayohusu masuala ya kuanguka kiuchumi.
Wengi wao wanahofu kucheleweshewa malipo, kukosekana kwa tarehe mahsusi ya uwasilishaji bidhaa na kutokuwapo kwa utekelezaji wa mikataba ya ununuzi.
Kubadili sera ndiyo suluhisho?
Ripoti ya kitaalamu iliyopewa jina la Making Medicines in Africa, inasema kuna mengi yanayopaswa kufanywa zaidi ya mageuzi ya kisera.
“Inahitajika mabadiliko ya kifikra kwa watunga sera wa Tanzania ili waangalie jinsi ya kuweka vipaumbele vya sekta,” inashauri ripoti iliyotolewa mwaka 2016 yenye kichwa cha habari: “Pharmaceutical Manufacturing Decline in Tanzania: How Possible Is a Turnaround to Growth?
Je, kuna fursa
Licha ya changamoto zinazoendelea kuikabili sekta ya uzalishaji wa dawa nchini, baadhi ya wawekezaji wanaona kwamba kuna fursa iliyoko mbele yao.
Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Limited (TPIL), Ramadhan Madabida anasema bado kuna fursa nyingi ambazo wawekezaji wa ndani wanapaswa kujikita nazo.
Anasema mahitaji ya dawa nchini kwa mwaka yanafikia Dola za Marekani 550 milioni sawa na Sh1.24 trilioni.
“Wazalishaji halisi wa dawa walioko nchini bado hawatoshi kuziba pengo la uhitaji lililopo,” anasema.
Ripoti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji iliyotolewa kwa Mwananchi inaonyesha kwamba kuna viwanda 13 pekee ambavyo vinajishughulisha na uzalishaji wa dawa nchini
“…Lakini ni vitano tu ambavyo vinaendelea na uzalishaji hadi sasa,” inasema ripoti hiyo.
Hata hivyo, inaonyesha kuwa viwanda vilivyokidhi ubora wa mazingira ya uzalishaji (GMP) na kupatiwa leseni ni vinne tu.
Madabida anasema Serikali inapaswa kushirikiana na wawekezaji wa ndani kusudi izibe pengo hilo lakini anashauri iunde sera itakayowezesha wawekezaji kupata fedha kutoka taasisi za fedha ili kuwezesha uwekezaji zaidi.
“Ni muhimu sasa kufikiria jinsi ya kuwapa motisha wawekezaji wa ndani kupata unafuu wa kodi na fursa nyingine katika ukopaji. Kwa mfano, wakati tunaponunua dawa kwa ajili ya kuuza kama wawekezaji, lazima tukutane na gharama za VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) kitu ambacho kinavunja morali ya wawekezaji,” anasema Madabida.
Kadhalika, anasema; “Hakuna barua inayotolewa (letter of credit) ambayo itamwezesha mwekezaji kupata fedha kutoka kwa taasisi za fedha tofauti na ilivyo kwa wageni.”
Kuna nuru mbele ya safari?
Kutokana na mwamko wa kisiasa wa kutaka wawekezaji wa ndani kuwekeza katika viwanda vya dawa, zaidi ya wawekezaji 10 wameonyesha nia, ripoti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji inasema.
Wizara hiyo inasema Serikali sasa inaandaa mpango mkakati wa kitaifa kwa ajili ya uzalishaji wa dawa ambao utatoa unafuu kwa wawekezaji wa ndani.
“Wakati utakapopitishwa na mamlaka, mkakati huu utatoa upendeleo wa bei kwa viwanda vya hapa nchini kwa asilimia 15 dhidi ya dawa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. Pia, kutakuwa na orodha ya dawa zitakazozalishwa nchini na mahitaji halisi ya nchi na kuondolewa kwa tozo ya kodi ya malighafi zinazoingizwa nchini,” inasema wizara hiyo.
Rais wa Chama cha Wazalishaji wa Dawa Nchini (PST), Issa Hango anasema aina hii ya uwekezaji inahitaji kazi ya ziada ikiwamo kuwaelimisha wawekezaji kuhusu fursa zilizopo katika sekta hiyo hapa nchini.
“Hakuna uelewa mpana miongoni mwa wataalamu wenyewe kuhusu fursa zilizopo katika uwekezaji wa sekta hii,” anasema Hango katika mahojiano maalumu yaliyofanyika katika ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Tabata Relini, Dar es Salaam, hivi karibuni.
Nyongeza ya ripoti hii na Asna Kaniki
INAENDELEA KESHO