Prime
Kashfa, kejeli vinapogubika talaka za mastaa

Muktasari:
- Mshauri wa uhusiano, Meridiana Kiwovela anasema ni ulimbukeni kumzungumzia vibaya mtu ambaye mmewahi kulala kitanda kimoja au hata mkatengeneza familia pamoja.
Umewahi kufanyiwa kejeli au kukashifiwa kama sio kutukanwa na mtu mliyekuwa na uhusiano ukiwamo ule wa ndoa?
Kama hujawahi, una bahati kwani kuna watu hukumbwa na masaibu, kiasi cha kujutia muda waliotumia pamoja na wenza wao waliogeuka maadui.
Kejeli, kashfa na hata matusi, vimekuwa vikishuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii kwa baadhi ya watu hasa wale maarufu wanapoachana. Wapo wanaokwenda mbali zaidi na kuanika mambo ambayo umma haukupaswa kufahamu.
Yao matukio kadhaa hapa nchini ambapo watu maarufu walipobwagana, kila mmoja kwa wakati wake aliingia mtandaoni kueleza dosari za mwenzake.
Huwa ni kama mashindano, kila mmoja anataka kuuelezea umma jinsi mwenza wake alivyokuwa mbaya na asiyefaa kwenye jamii.
Hali hiyo haiwatokei watu mashuhuri pekee, hata wale wa maisha ya kawaida wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kutumiana vijembe.
Pasipo kutaka kutajwa jina, mmoja wa waathirika wa kadhia hiyo akizungumza na Mwananchi anasema baada ya kuachana na mwenza wake, aliutangazia umma kuwa hana uwezo wa kukidhi haja zake za kimwili.
“Mwanamke nimekuwa naye kwa miaka miwili, hakuwahi hata siku moja kuniambia simridhishi lakini ikatokea tumegombana kwa sababu ya kitu kingine akaenda kuwaambia watu kwamba alikuwa ananivumilia tu hata sina uwezo wa kumridhisha.
“Maneno hayo yaliniumiza, lakini nilipiga moyo konde ila namchukia. Hata nikikutana naye siwezi kumsalimia, alinifanya nijiulize maswali mengi niliposikia ananitangazia hivyo. Kwa kiasi fulani nilipoteza hali ya kujiamini ingawa kwa sasa hayo yameshapita,” anasema.
Kwa upande wake, mkazi wa Mtoni Mtongani, Amina Nemelagani aliyefikwa na changamoto hiyo anasema:
“Niliolewa, nikaishi na mwanamume kwa miaka mitatu tukapata watoto wawili. Ikatokea changamoto tukaachana, siku naondoka aliniambia niache kila kitu zikiwamo nguo alizonunua akisema nilikwenda kwake nikiwa sina chochote.”
Anaongeza: “Alidai alinitoa kwetu nikiwa sina mbele wala nyuma, nikiwa kwake ndiko nimejifunza kuvaa nguo zinazoeleweka, nimeanza kuonekana mtu wa maana ndiyo maana nimekuwa jeuri, hivyo nirudi kwetu kama nilivyokuja.
“Sikuwa na namna zaidi ya kufuata maelekezo yake ikizingatiwa kuwa ni kweli sikuwa na shughuli ya kufanya, hivyo matumizi yangu yote yakiwamo mavazi aligharimia yeye. Jambo hilo liliniumiza, tangu wakati huo nimeacha mambo ya kumtegema mwanamume kwa kila kitu.”
Mkazi wa Toangoma jijini Dar es Salaam, Getrude Shija aliyeozesha binti yake hivi karibuni, anasema kejeli za namna hiyo ni sababu za wazazi kuwapatia mabinti zawadi za vitu muhimu vya ndani wanapoingia kwenye ndoa ili kuepuka masimango.
Anasema alimpa mtoto wake wa kike kila kinachohitajika ndani ya nyumba, ili mume wake asije kumnyanyasa kuwa alimtoa kwao bila kitu.
“Wanaume hubadilika, akishakuchoka ndani ya nyumba anaweza kukufanyia vituko utaondoka bila chochote, zaidi atakusimanga. Binafsi sikutaka hayo yamkute mwanangu, nimempa kila kitu ili ikitokea wameshindwana, anaweza kuvichukua na kwenda kuanza maisha mengine,” anasema.
Mtazamo wa kidini
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka anasema kejeli ni vitendo vinavyoonyesha namna jamii ilivyopotoka kwa kukosa maadili na malezi sahihi.
“Mwenye maadili na aliyelelewa vizuri hawezi kufanya hayo kwa sababu ni aibu kwake, familia yake na jamii kwa ujumla. Ndani ya Quran Mwenyezi Mungu anawasisitiza wenza wasisahau fadhila walizofanyiana.
“Watu walioishi pamoja lazima kuna wema waliofanyiana, kama hivyo ndivyo basi wautumie huo wema kama nguzo ya kuwafanya waendelee kuheshimiana. Kutoleana siri baada ya kuachana si ubinadamu,” anasema.
Sheikh Mataka anasema ni jambo la kawaida kwa binadamu kumsaidia mwingine kwa kuwa viumbe hivyo vinategemeana.
“Binadamu kusaidiana ni jambo la kawaida, tumeumbwa kusaidiana. Hakuna anayejitosheleza, hivyo usijione mkubwa kumsaidia mwenzako. Vitabu vya dini vinatukataza kufanya kitendo chema au kutoa sadaka ambayo baadaye inafuatiwa na maudhi. Kumsimanga au kumuumbua uliyemsaidia ni kosa, hasa ikiwa ni mtu aliyekuwa mwenza wako wa maisha,” anasema.
Anasema ni muhimu kwa wanajamii kujifunza maadili mema, ikiwamo kutowasimanga au kuwazungumzia vibaya wanaowasaidia.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Hananja anasema wanaofanya hayo ni matokeo ya watu kutolelewa katika misingi ya kimaadili.
“Ukiwa na maadili huwezi kuzungumza vibaya dhidi ya mwenza wako, hapo inamaanisha kwamba una uchungu moyoni. Katika dini ya Kikristo tunakatazwa kuwa na uchungu.
“Biblia inasema hutakiwi kuishi na uchungu, ni kweli mwanadamu hawezi kukosa hasira lakini isikufanye utende dhambi kwa kulipa kisasi. Uchungu ni mbaya, kuanika madhaifu ya mwenzako na kumtendea mabaya ni dhambi,” anasema.
Kisaikolojia ikoje?
Mwanasaikolojia, Christian Bwaya anasema tabia ya kukejeli ni matokeo ya changamoto ambazo amepitia mtu kwenye ukuaji wake, zinazomfanya muda wote atake kuonyesha watu kuwa yuko sawa na bora kuliko wengine.
Bwaya anasema wengi wenye tabia hiyo ni wale ambao kuna vitu muhimu walikosa katika ukuaji wao, ukiwamo upendo. Pia manyanyaso na hata kudharauliwa, hivyo anapofikia utu uzima hutaka kuonyesha kila kitu kipo sawa kwake.
Kisaikolojia anasema tabia hiyo huchangiwa na hali ya mtu kutaka kuwa na mamlaka au kuwa juu kwenye kila kitu, ikiwamo katika uhusiano wa kimapenzi jambo linalosababisha usidumu.
“Inapotokea uhusiano huo ukavunjika, atataka kuonyesha yeye ni kila kitu na huyo aliyekuwa naye si chochote. Hili ni tatizo kubwa kwa sababu watu wa aina hii hawajui kupenda, wanachofanya ni kutaka kuonyesha uwezo wao.
“Hii ndiyo sababu anaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu si kwamba anampenda bali anataka kuonyesha watu kwamba yupo na huyo mtu. Kufanikisha hilo atatumia nyenzo zozote ikiwamo fedha, mali na hata kumpatia vitu vya thamani,” anasema.
Bwaya anasema: “Hili la kumzungumzia mwenza vibaya baada ya kuachana ni tatizo ambalo tunalo kwenye jamii, linaonekana kawaida ila kisaikolojia ni ugonjwa wa akili ambao huchangiwa na hiyo control (udhibiti) ambayo mtu anataka kuionyesha. Ukiingia kwenye mapenzi na control huwezi kufanikiwa kwa sababu hakuna anayepaswa kuwa juu kwenye mapenzi.”
Mshauri wa uhusiano, Meridiana Kiwovela anasema watu wanashindwa kuiishi dhana ya usawa kwenye uhusiano ndiyo sababu kuna mmoja anaona bila yeye hakuna ambacho mwenza wake angefanya.
“Hapa ndipo wengi hukosea, mkishaingia kwenye uhusiano lazima wote muwe sawa. Kuna tofauti ya majukumu kati ya mwanamke na mwanamume lakini inapokuja kwenye dhana nzima ya uhusiano wote mpo sawa.
“Sasa ikitokea mmoja akajiona yeye ndiye anayesababisha uhusiano uwepo ndipo changamoto inapoanzia, kumhudumia mwenza wako ni miongoni mwa vionjo vinavyonogesha uhusiano isiwe ni kama fimbo ya kumchapia pale jahazi litakapokwenda kombo,” anasema na kuongeza:
“Haya mambo ya baada ya kuachana kuanza kumsimanga mwenza hayakuanza leo, sema siku hizi yanaonekana sana kwa sababu yamekuja kwenye mitandao ya kijamii. Naweza kusema ni ulimbukeni kumzungumzia vibaya mtu ambaye mmewahi kulala kitanda kimoja au hata mkatengeneza familia pamoja.”