Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Talaka ni janga, dawa ni hii

Tunajua fika kwa uzoefu wetu na hata kwa utafiti, kuwa hakuna binadamu wala mwanandoa anayependa wala kushabikia talaka, hata kama baadhi ya dini na sheria vimeiridhia kutokea ikilazimu.

Hivyo, katika kipengele hiki tutajadili talaka na madhara yake, hasa kwa wanandoa, familia, na jamii hata nchi kwa ujumla.

Kwa vile siyo kila kitu kinaweza kutafsiriwa au kueleweka kwa mujibu wa kamusi, tutaepuka kuwachosha na maana au tafsiri za talaka kwa mujibu wa mamlaka mbalimbali kama vitabu vya kidini na vya kisheria. Tunaamini kuwa talaka, kwa lugha, nyepesi ni kinyume cha ndoa. Kwa ufupi, talaka ni kifo cha ndoa.

Palipo na ndoa hakuna talaka na palipo na talaka hakuna ndoa na viwili hivi haviwezi kuishi kwa pamoja katika sehemu moja, yaani ndoa na talaka kwa wakati mmoja.

Pia, ifahamike, talaka, tofauti na ndoa, ina madhara makubwa kwa wanandoa binafsi, watoto, jamii na nchi. Mfano, chukulia wanandoa wanaomiliki mali kwa pamoja kama vile gari, nyumba, hata shamba.

Wanapotalikiana, huwa maskini, kwani, wakigawana mali zao, wanabakia watu wasio na vile walivyokuwa navyo kabla ya kuachana. Pia, ieleweke. Kuna vitu visivyogawanyika kama watoto ambao wazazi wakitalikiana, huchanganyikiwa kwa vile ni vigumu kugawana wazazi au kugawana mapenzi yao kwao kwa usawa.

Hapa, ndipo ilipo kadhia ya watalaka kuuana hata kuhujumiana kiasi cha kudhoofishana wao na watoto wao hata jamii. Zaidi, kesi za talaka hutumia muda na fedha nyingi kiasi cha kuathiri utendaji na uzalishaji wa wahusika.

Hivyo, ndoa ni sehemu ya kutunza mafanikio ya wawili na hata jamii kwa ujumla mbali na kuwapa watoto kinga na utulivu na mafanikio katika maandalizi ya maisha yao.

Athari na hasara za talaka ni nyingi mno, kiasi kwamba hatuwezi kuzielezea zote kwa ukamilifu katika kipengele kimoja. Cha msingi, ni kuiogopa, kuitahadhari, na kuiepuka kadiri iwezekanavyo, kwani, haijengi zaidi ya kubomoa.

Hata hivyo, upendo ukiwa wa kweli na kufanikisha lengo la ndoa, ni kinyume. Wahusika wataridhika, watafurahi, watafanikiwa, wataongeza upendo, na kuishi maisha marefu ikilinganishwa na walioharibikiwa au kutalikiana.

Tunapoongelea madhara ya talaka kuhusiana na uchumi na uhusiano wa wahusika, hatugusii vifo vitokanavyo na kuachana. Kwa mfano, kwa mujibu wa National Library of Medicine (2022), takwimu za mauaji ya watalaka katika nchi ya Ufini, zinaonyesha kuwa kati ya 2003 na 2013, yapata asilimia 65 ya wanawake waliouawa nchini humo, waliuawa na ama wenza wao wa sasa au wa zamani, iwe ni katika ndoa au mke na mume waishio kinyumba.

Mwaka 2007 pekee, chini Marekani, wanawake asilimia 45 waliuawa na wenza wao wa sasa au wa zamani. Hapa inaonyesha kuwa mauaji ya wanandoa yanayofanywa na wenzao ni janga la dunia na waathirika wengi ni wanawake.

Hii haina maana kuwa hakuna wake wanaoua waume zao, iwe ni wa sasa au wa zamani. Kwa mujibu wa jarida la Forbes (2024), idadi ya wanandoa waliouawa na wenzao ilikuwa 1,363 katika kila 100,000 kwa watalaka ikilinganishwa na 779 katika kila 100,000 kwa walio katika ndoa.

Kwa mujibu wa Forbes (2024), talaka huathiri wanawake kwa viwango tofauti na wanaume. Mfano, wanaume huathiriwa na janga la ndoa kwa uwiano wa 1,772 kwa kila wanandoa 100,000 ikilinganishwa na wanawake 1,095 kwa kila wanandoa 100,000 Hapa somo ni kwamba kuna wanandoa wanaaendelea kuishi kwenye ndoa hatarishi hadi kuua au kuuliwa.

Hali hii hatarishi inajenga maswali mengi juu ya ni kwa nini watu waliokutana wakaamua kupendana na kuoana huuana. Japo hatuna jibu na sababu zote, tunaamini kuwa mauaji ya namna hii, ama yanatokana na kulipizana visasi, kuchanganyikiwa au kukata tamaa ya kuishi.

Hivyo, namna ya kujiepusha na balaa hili ambalo linaweza kumkumba yeyote ni kujielimisha juu ya ndoa ili kulizuia hata kuliepuka. Kila gonjwa lina dawa. Na dawa ya kuimarisha na kufaidi ndoa ni kuielewa sawa na ambavyo tunapoumwa, huenda hospitali na kupata dawa na kupona, ingawa si kwa magonjwa yote.

Wahenga wanaasa kuwa ni heri kuzuia kuliko kutibu, japo kutibu si vibaya ila kuzuia bado ni bora, kwani humwezesha mhusika kuepuka baadhi ya magonjwa na hata kifo.