‘Kaweni waadilifu na Wazalendo’

Baadhi ya wahitimu wa chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Kigoma wakiwa katika maandamano kuingia katika kiwanja cha mwanga senta mjini Kigoma ambapo mahafali hayo yamefanyika.

Muktasari:

Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengeye amewataka wahitimu wa chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Kigoma, kuwa waadilifu na wazalendo katika kazi zao wanapoenda kuitumikia jamii .

Kigoma. Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengeye amewataka wahitimu wa chuo cha Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) kampasi ya Kigoma, kuwa waadilifu na wazalendo katika kazi zao wanapoenda kuitumikia jamii .

Akizungumza leo Ijumaa Desemba Mosi, 2023 kwenye mahafali ya 21  ya chuo hicho kwa niaba ya Andengeye, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli amesema uzalendo na uadilifu utasaidia kuboresha huduma katika jamii ikizingatiwa kada hiyo kuwa muhimu na kutegemewa

Amesema taaluma ya mambo ya  fedha ni taaluma  nyeti na inayotakiwa kuwa mzalendo, muadilifu na kutokuwa na tamaa kwani itasaidia kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali  na nchi kwa ujumla.

 “Taaluma hii imekuwa na changamoto kwa baadhi ya watu kushindwa kuishi katika miiko ya kazi yao na kujiingiza katika mambo yasiyo na maadili na wakati mwingine kuisababishia Serikali hasara hivyo niwasihi kuishi katika miiko ya kazi zenu,”amesema Andengenye

Amesema Serikali inakiangalia chuo hicho kwa karibu sana ndio maana kimekijumuisha  katika mradi unaokifadhili katika ujenzi wa chuo hicho mjini Kigoma  tawi la Kigoma kinachogharimu  Sh11 bilioni ambapo kwa sasa umefikia asilimia 26 ya ujenzi wake.

“Mradi huo ni fursa kwa jamii inayozunguka katika eneo la ujenzi wa chuo hicho ikiwemo kupata ajira rasmi na zisizo rasmi na kuweza kukuza kipato chao kwa mtu mmoja mmoja na mkoa wa ujumla,”amesema

Mkuu wa Chuo cha TIA, Kampasi ya Kigoma Profesa William Pallangyo amesema katika tawi la Kigoma jumla ya wanafunzi 910 wamehitimu huku idadi ya wahitimu wote wa chuo cha TIA kwa mwaka 2022/23 ni 13,218  kwa Dar, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Kigoma na Singida.

Amesema mahafali hayo ya kwanza kwenye kampasi hiyo yameenda sambamba na kutambulisha masomo mapya ya ngazi ya shahada katika uhasibu, ugavi na ununuzi, usimamizi wa biashara na uongozi wa rasilimali watu  zitakazotolewa chuoni hapo.

Amesema hatua hiyo ya kuwa na masomo hayo ngazi ya shahada  itawapa fursa wadau mbalimbali wa ndani ya Tanzania na nchi jirani kujiendeleza kielimu baada ya kusogezewa huduma hiyo karibu.

Mwenyekiti wa bodi ya TIA, Wakili Said Musendo amewasihi  wahitimu hao kwenda kuzitumia taaluma zao vizuri na kuwaletea matunda, bila kusahau kujiendeleza kielimu akidai elimu haina mwisho na hapo ni mwanzo wa elimu yao hivyo bado wanasafari ndefu.